• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Kaka zake Bashir nao wanyakwa Museveni akijitolea kumpa hifadhi

Kaka zake Bashir nao wanyakwa Museveni akijitolea kumpa hifadhi

Na AFP

SERIKALI ya Kijeshi nchini Sudan Alhamisi ilitangaza kwamba imewatia mbaroni ndugu wawili wa aliyekuwa Rais Omar al-Bashir aliyeondolewa mamlakani kupitia mapinduzi ya kijeshi wiki iliyopita.

“Tunawazuilia washirika waliosalia kwenye serikali iliyopita….na nduguze Bw Bashir kwa majina Abdallah na Abbas,” Msemaji wa jeshi Luteni Jenerali Shamseddine Kabbashi akawaeleza wanahabari.

Bw Kabbashi alisema kunyakwa kwa wawili hao ni sehemu tu ya operesheni inayoendeshwa ya kuwatia mbaroni washirika wote wa Bw Bashir aliohudumu nao wakati wa uongozi wake wa zaidi ya miongo mitatu.

Vile vile Bw Kabbashi pia alisema makundi ya wahalifu yanayohusishwa na chama tawala cha National Congress Party (NCP) kilichokuwa kikiongozwa na Bw Bashir yamedhibitiwa huku wengine wakiendelea kuandamwa na polisi.

Mabw Abbas na Abdallah walikamatwa siku moja tu baada ya familia ya Bw Bashir kufichua kwamba Rais huyo, aliyeondolewa mamlakani siku sita zilizopita, alipelekwa katika gereza la Kober mjini Khartoum.

Bw Bashir alikuwa akiwahukumu na kuwatesa sana wapinzani wake kwenye gereza hilo wakati alipokuwa mamlakani huku mashirika ya kimataifa ya kijamii yakimkashifu kwa ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu.

“Bashir alikamatwa usiku wa kuamkia jana na kupelekwa katika gereza la Kober lililoko mji wa Khartoum,” akasema mmoja wa jamaa zake ambaye hakutaka jina lake linukuliwe kutokana na sababu za kiusalama mnamo Jumatano.

Waandamanaji nchini humo hata hivyo wameapa kusalia barabarani hadi pale washirika wote wa Bw Bashir watapokamatwa na kushtakiwa kisha utawala wa sasa wa kijeshi ukabidhi mamlaka kwa raia.

Wakati uo huo Waziri wa Masuala ya Nchi za Kigeni wa Uganda Henry Okello jana alisema taifa hilo lipo tayari kumpa hifadhi Bw Bashir ambaye pia anaandamwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu(ICC).

“Tuko tayari kumpa hifadhi Bw Bashir iwapo uamuzi wa kumleta nchini utaafikiwa. Serikali ya Uganda inaendelea kufuatilia matukio nchini Sudan kwa jicho la ndani na tunaomba jeshi kuheshimu haki za raia na kuwapa mamlaka kwa amani.

“Bw Bashir alifanya jitihada kubwa katika kurejesha amani nchini Sudan Kusini na bado tunamheshimu kama kiongozi,” akasema Bw Okello.

You can share this post!

AKILIMALI: Siri ya kufanikisha kilimo cha michungwa ya...

AKILIMALI: Aina ya sungura bora na walio rahisi zaidi...

adminleo