• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
AKILIMALI: Ufugaji ng’ombe kwa makini na kuwapa lishe bora matokeo ni kiwanda cha maziwa gururu

AKILIMALI: Ufugaji ng’ombe kwa makini na kuwapa lishe bora matokeo ni kiwanda cha maziwa gururu

Na BRIAN OKINDA na FAUSTINE NGILA

WAKATI Margaret Kamande alijitosa katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa mwaka 2014 hakutarajia kuwa uwekezaji wake siku moja ungemletea faida kubwa na kubuni nafasi za ajira kwa vijana.

Shamba lake, analoliita Hakikisha Farm, ni la ekari nne na liko karibu na mji wa Limuru, Kaunti ya Kiambu ambapo anafuga ng’ombe 65 wa maziwa na ambao ni wa aina ya Friesian katika ardhi ya ekari tatu.

Anaeleza kuwa wakati alianza ufugaji, ng’ombe wake walikuwa wanampa maziwa kidogo mno ambayo alikuwa anauzia majirani.

Baadaye, aliwekeza katika ng’ombe wa maziwa wa Friesian na lishe ya ubora wa juu.

Alianza pia kuwapeleka ng’ombe hao kwa vijisehemu vya malisho kwa zamu, hatua ambayo anasema imemsaidia kupunguza uwezekano wa ugonjwa wa maziwa kuwa na damu kuvamia mifugo wake.

“Mbinu hii pia inahakikisha mifugo wametulia bila bughudha ya kuvamiwa na kupe. Ni rahisi kuwapa mazingira safi,” anaeleza Bi Kamande.

Hii ilichangia kiwango cha maziwa kuongezeka katika miaka iliyofuata. Awali alikuwa anakama lita 7 kwa kila ng’ombe, lakini kwa sasa anapata lita 17 kwa kila ng’ombe huku ng’ombe anayempa maziwa mengi zaidi akitoa lita 40 kwa siku.

Anafichua kuwa matokeo haya ni kutokana na mpango wa lishe bora alioweka, huku akinunua lishe kutoka kwa kampuni tajika ya utengenezaji wa lishe ya Better Feeds Nutrition, mjini Thika.

Mike Kamau, mwasisi wa kampuni hiyo anasema kuwa biashara ya kufuga ng’ombe wa maziwa hunawiri kulingana na ubora wa lishe mfugaji anayowalisha ng’ombe wake.

“Ukiwapa chakula kibovu, utapata hata lita tano. Ukiwapa chakula bora, hautakosa lita 15,” anashauri.

Bi Kamande anasema kuwa mumewe, Dkt George Kamande, ambaye ni mtaalamu wa lishe bora katika kampuni ya Diamond V, alichangia pakubwa kuchochea mabadiliko ya mipango ya lishe. Kampuni hiyo hufanya utafiti kuhusu teknolojia ya kuboresha lishe na afya ya mifugo.

Baada ya kushuhudia kuongezea kwa maziwa hapo 2017, Bi Kamande aliamua kukoma kuwauzia majirani na kuwekeza kwa uhifadhi wa maziwa na kuongezea ubora na thamani.

Katika shamba lao, akishirikiana na mumewe, walianzisha kiwanda cha kuunda maziwa gururu na icecream.

Pia wanatengeneza jibini (cheese) na siagi, ila kwa kiwango cha chini.

Bidhaa zote huuzwa kupitia brandi ya Daileys.

Wanauza maziwa gururu katika ladha nne, ambazo wanasema wanaziagiza kutoka Arizona, America.

“Flava zetu za maziwa gururu ni vanilla, stroberi, embe-stroberi na nanasi-ndizi. Isikrimu ina ladha tatu- vanilla, siagi ya njugu na embe,” anasema Bi Kamande.

Kiwanda hicho huunda lita 450 za maziwa gururu kwa siku, na kuuzia maduka ya jumla katika kaunti za Kiambu, Nairobi, Nakuru na Nyeri.

“Kwa sasa ndio mwanzo tu. Hatujapenyeza kwa soko vizuri kutokana na ushindani mkali wa kampuni ambazo tayari zinatambulika na wateja. Lakini kwa muda usiokuwa mrefu, bidhaa zetu zitapatikana katika maduka tajika ya jumla,” anasema Bi Kamande.

Bidhaa ya maziwa gururu huwekwa kwa mikebe ya mililita 100, robo lita, nusu lita, lita moja na lita tano, ambayo wanasema bei yake ni nafuu ikilinganishwa na brandi zingine licha ya kuwa na ubora sawa.

Uwekezaji huu ambao umesajiliwa kwa jina Terrestria Foods Ltd, kwa sasa una wafanyakazi 10 wa kudumu, watano kwa shamba na watano wa kuzalisha bidhaa za maziwa.

Vibarua

Hata hivyo, meneja wa kampuni Monica Mwaura anasema kuwa wao huajiri vibarua wakati kazi imezidi.

Hata hivyo, wao hukumbana na changamoto za ushindani, matangazo, maajenti bandia wanaowauzia shahawa feki za kutunga ng’ombe mimba.

“Uwepo wa lishe bora ya mifugo na uwezo wetu wa kuzuia magonjwa na wadudu, huku tukimiliki ardhi yetu ya malisho kumetusaidia kupunguza gharama katika biashara hii.

“Kwa kuwa ng’ombe wetu hawatangamani na ng’ombe wa mazizi ya nje, pamoja na usafi tunaodumisha hapa, ni rahisi kukama faida kubwa kwani tunazingatia mbinu zote za ufugaji bora,” anasema.

You can share this post!

AKILIMALI: Mkulima analala pazuri kwa kufuga kondoo kwa...

Mwathethe awataka waliofuzu KMA kujizatiti kuifaa nchi

adminleo