• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Bei ya unga yapanda mahindi yakizidi kuadimika

Bei ya unga yapanda mahindi yakizidi kuadimika

Na BERNARDINE MUTANU

WATENGENEZAJI wa unga wamepandisha bei ya unga huku upungufu wa mahindi ukiendelea kushuhudiwa nchini.

Kampuni ya Unga Limited sasa inauza kilo mbili za brandi ya Jogoo kwa Sh117 kutoka S109 wiki iliyopita ilhali kilo mbili za unga wa brandi ya Soko unaotengenezwa na kampuni ya Capwell ni Sh120.

Lakini baadhi ya wauzaji wanauza bei ya chini kuliko iliyopendekezwa na watengenezaji hao. Kwa mfano, katika duka la rejareja la Naivas, kilo mbili za unga wa Soko ni Sh118 badala ya Sh120.

“Hatuwezi kuwaambia wauzaji wa unga bei wanayofaa kuuza unga nayo, ni chaguo lao,” alisema Rajan Shah, Mkurugenzi Mkuu wa Capwell.

Mamlaka ya Ushindani ilimuunga mkono. Mkurugenzi wake alisema maduka ya rejareja yamo huru kuuza unga kwa bei wanayotaka ikiwa hawashirikiani kuuza bei moja.

Bei ya unga imeongezeka kwa asilimia 28 katika muda wa wiki mbili hadi Sh117 kwa kilo mbili.

Ongezeko hilo limetokana na ongezeko la bei mahindi ambapo gunia la kilo 90 limeongezeka kutoka Sh2,000 Machi hadi Sh3,200. Bei inatarajiwa kupanda zaidi katika muda wa miezi kadhaa ijayo kutokana na upungufu zaidi wa mahindi sokoni.

Hata hivyo, serikali ilionya watengenezaji na wauzaji wa unga wa mahindi dhidi ya kupandisha bei ya unga.

You can share this post!

Utazimiwa simu ukikaidi kujisajili kwa Huduma Namba

Thika Queens kuvaana na Gaspo KWPL

adminleo