• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Wanasoka wa Gor Mahia kutemwa kwa utundu wao

Wanasoka wa Gor Mahia kutemwa kwa utundu wao

Na JOHN ASHIHUNDU na CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa Gor Mahia, Ambrose Rachier amewashutumu wachezaji wake kwa kusaliti timu hiyo wakati wa mechi za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) huku akitishia kuwatimua baadhi yao kutokana na ukosefu wa nidhamu.

Rachier alikuwa akiwahutubia waandishi jana katika hoteli moja jijini Nairobi kufuatia madai kwamba afisi yake imeshindwa kuendesha shughuli za klabu hiyo ipasavyo.

Ilipokuwa ikijiandaa kucheza na RS Berkane ya Morocco, Gor Mahia ilikumbwa na masaibu ya kila aina kabla ya kubanduliwa nje katika hatua ya robo-fainali kwa jumla ya mabao 7-1.

Mwenyekiti huyo anadai kuwa wachezaji walikataa kufanya mazoezi kwa siku mbili kabla ya kucheza mechi ya mkondo wa kwanza kabla ya kufanya visanga vya kila aina walipokuwa safarini kuelekea Morocco kwa pambano la marudiano.

“Cha kushangaza zaidi ni kwamba baada ya kukataa kufanya mazoezi hapa nchini, baadaye walisisitiza lazima walipwe malimbikizi ya marupurupu yao kabla ya kuingia uwanjani,” aliongeza kiongozi huyo anayefahamika kutokana na ufanisi wake mkubwa tangu achukue usukani wa klabu hiyo zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Wachezaji hao, ambao Rachier hakuwataja, alidai, kadhalika kuwa walilala nje ya hoteli ya timu kabla ya kujitokeza saa chache kabla ya mechi kuanza ugani Kasarani, lengo lao likiwa kuaibisha usimamizi wa klabu mbele ya watu mashuhuri akiwemo Waziri wa Michezo, Amina Mohammed.

Gor Mahia walipoteza mechi hiyo kwa 2-0.

Autetea uongozi

Wakati huo huo, Rachiel ametetea vikali uongozi wake kufuatia matatizo ya usafiri wa ndege kutoka Nairobi kuelekea Berkane kwa mechi ya marudiano ambayo waliingia uwanjani wakiwa wamechelewa.

Mwenyekiti huyo aliwashutumu Francis Kahata na Philemon Otieno kwa kusambaza picha za uongo za mateso ili wahurumiwe.

Wakati huo huo, Gor Mahia wamejipata pabaya kwa mara nyingine baada ya kupigwa faini ya Sh1.5 milioni na Shirikisho la Soka la Afrika(CAF) kutokana na matukio mawili ya ukosefu wa nidhamu wa mashabiki wake.

Hata hivyo, Gor imepewa siku 60 kukata rufaa kuhusu uamuzi huo wa CAF.

Kupita barua iliyotoka kwa CAF, mashabiki wa K’Ogalo walipigwa faini ya Sh500,000 kwa kurusha chupa ndani ya uwanja wa Kasarani walipokuwa wakisherehekea bao la pili walilofunga dhidi ya Na Hussein Dey ya Algeria.

Kisa cha pili kilichovutia K’Ogalo adhabu kali ya Sh1 milioni ni hatua ya mashabiki kuingia uwanjani kusherehekea ushindi wa 1-0 dhidi ya Petro de Atletico ya Angola katika uga uo huo wa Kasarani.

You can share this post!

HAPA KITANUKA: Patachimbika Barca, Reds wakionana

KIPWANI: Usistaajabu wasanii tele wa injili, ni Neno

adminleo