• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Maskwota wa Shifta wahofia kulaaniwa kwa kutotunza makaburi

Maskwota wa Shifta wahofia kulaaniwa kwa kutotunza makaburi

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa jamii ya Wabajuni waliofurushwa kutoka kwa makazi yao wakati wa vita vya Shifta mnamo miaka ya 1960 kaunti ya Lamu sasa wanahofia huenda wakaadhibiwa kwa kulaaniwa na mababu zao waliofariki zamani eneo hilo kwa kukosa kutunza makaburi yao.

Katika kikao na wanahabari mjini Lamu Jumapili, wakazi hao ambao walionekana kujawa na hofu walisema makaburi ya mababu zao yamekuwa yakikojolewa na mbwa, paka na wanyama wengine wa porini hasa tangu walipohama vijijini mwao baada ya magaidi wa Shifta kuvamia makazi yao.

Wakazi hao kutoka vijiji vya Kiunga, Ishakani, Mvundeni, Mwambore, Rubu, Sendeni na Ashuwei wanasema makaburi ya watu wao yamekosa ulinzi, jambo ambalo nio kinyume na tamaduni zao.

Wanasema tangu kuhama kwao kutoka vijiji husika, wao hawajaweza kuzuru makaburi ya wazee wao kufanya matambiko na maombi mbalimbali ya kutafuta radhi kutoka kwa wazazi wao.

Maskwota hao wanasema tangu walipohama vijijini mwao hawajaona amani.

Wanasema wanaamini huenda maisha yao ya kiufukara yanatokana na laana hizo za wazazi wao waliowaacha bila ya kutunza makaburi yao.

Maskwota wa vita vya Shifta wakiongozwa na msemaji wao Mohamed Mbwana (kati) wakati wa kikao cha awali. PICHA/KALUME KAZUNGU

Msemaji wa waathiriwa wa vita vya Shifta Kaunti ya Lamu, Mohamed Mbwana, aliitaka serikali ya kitaifa kupitia Rais Uuru Kenyatta kuharakisha kutolewa kwa ripoti ya Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC) ambayo wanaamini itapelekea waathiriwa wa vita vya Shifta kupata haki yao.

Bw Mbwana alisema furaha yao ni kuona haki imetendeka na iwapo watarudishwa vijijini mwao.

“Ukiangalia jamii yetu imekithiri uchochole. Haya yote yanatokana na laana ya wazazi wetu. Tulitoroka vijiji vyetu kufuatia uvamizi wa mara kwa mara wa Shifta. Makaburi ya wazazi wetu yakabaki bila ulinzi na utunzi wowote.

“Kwa sasa mbwa, paka na wanyama wengine wa porini wanaendelea kukojolea makaburi ya wazazi wetu na kuyachafua. Tulihitajika kufanya matambiko na maombi ya mara kwa mara kwenye makaburi hayo.

“Hii inamaanisha wazazi wetu hawako radhi na sisi na huenda tayari tumepokea laana ambayo inatufanya kutotulia mahali tulipo. Ripoti ya TJRC itolewe ili haki itendeke,” akasema Bw Mbwana.

Bi Tima Amin alisema itakuwa bora kwa serikali kufyeta vichaka kwenye ardhi za waathiriwa wa vita vya Shifta na kufadhili ujenzi wa nyumba za maskwota hao kabla ya kuwasafirisha kuwarudisha kwenye makazi yao.

Bi Amin aidha alipinga vikali usoroveya wa ardhi za maskwoya wa Shifta ambao ulikuwa umeanzishwa na serikali ya kaunti, akisisitiza kuwa shughuli hiypo haijahusisha wenjeji.

“Cha msingi ni serikali itufadhili sisi waathiriwa wa vita vya Shifta kwa kufyeka na kujenga nyumba tutakazoishi vijijini mwetu. Wakitujengea nyumba itakuwa rahisi kwetu kurudi kule kuishi kama zamani.

“Kaunti iache kukimbilia kufanya usoroveya wa ardhi zetu ilhali sisi wenyerwe hatupo huko. Wanataka kugawanyia ardhi hizo akina nani na sisi hatupo,” akasema Bi Amin.

Bw Mahmoud Sharif alishikilia kuwa lazima ardhi za maskowota wa Shifta ziheshimiwe, hivyo akaiomba kaunti kushirikiana na Tume ya Ardhi nchini (NLC) ili kuhakikisha hatimiliki za ardhi husika zinapatikana.

“Tutashukuru iwapo kaunti na NLC itafikiria kutupa hatimiliki ya ardhi yetu ili tuilinde badala ya usoroveya kufanywa na ardhi zetu kupewa watu wengine wasiostahili. Ardhi zetu haziheshimiwi kutokana na kwamba hakuna hatimiliki kwa ardhi hizo,” akasema Bw Sharif.

Bi Mwanase Kale alisema huenda wakaelekea kortini hivi karibuni kuishinikiza serikali kutoa ripoti ya TJRC.

You can share this post!

Wawili hawajulikani waliko baada ya boti kuzama

Kenya yazoa medali 46 Riadha za Afrika

adminleo