• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Uhuru atamtema Raila 2022, ‘Tangatanga’ sasa wasema

Uhuru atamtema Raila 2022, ‘Tangatanga’ sasa wasema

GERALD BWISA na JOSEPH WANGUI

MZOZO kuhusu muafaka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga Jumapili uliendelea kuzua hasira miongoni mwa wanasiasa wa Jubilee huku baadhi yao wakidai kuwa Rais atamtema kiongozi wa ODM uchaguzi wa 2022 utakapokuwa unakaribia.

Katika eneo la Mlima Kenya, wabunge wa Jubilee walitofautiana vikali kuhusu ikiwa muafaka huo unalenga kusambaratisha ndoto ya Naibu wa Rais William Ruto kutaka kuwa rais 2022 au la.

Mbunge wa Mukurweini Anthony Kiai alimtaka Rais Kenyatta kuachana na Bw Odinga ili kunusuru ndoto ya Dkt Ruto kuongoza nchi hii baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Kulingana na Bw Kiai, kuna dalili kwamba Rais Kenyatta huenda akamhepa Bw Odinga kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 na kuunga mkono Dkt Ruto.

Bw Kiai alisema mgawanyiko unaoshuhudiwa ndani ya Jubilee kwa sasa umesababishwa na handisheki baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Chama cha Jubilee tayari kimegawanyika, na tunamtaka Rais Kenyatta kufutilia mbali handisheki ili kunusuru chama,” akasema Bw Kiai.

Mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni, hata hivyo, alitofautiana naye huku akisema kuwa handisheki inafaa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua alisema kuwa eneo la Mlima Kenya litamuunga mkono Dkt Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.

“Katika eneo la Kati, tunajali sana urafiki kwani Dkt Ruto amekuwa rafiki yetu tangu 2012. Tuna imani kwamba atashinda vikwazo vyote ambavyo amewekewa na atakuwa rais 2022,” akasema Bw Gachagua.

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa alishutumu kundi la Kieleweke linalopinga Dkt Ruto kuwa wanalenga kuzua vurugu ndani ya Jubilee ili kupata mwanya wa kujiunga na vyama vingine.

Wabunge Githinji Gichimu (Gichugu) na Samuel Gachobe (Subukia), hata hivyo, walishikilia kuwa hakuna mgawanyiko ndani ya Jubilee.

Wawili hao walisema kuna baadhi ya wanasiasa, ambao hawakuwataja, ambao wamegawanya wanachama wa Jubilee katika makundi mawili; TangaTanga na Kieweleke. Katika Kaunti ya Trans Nzoia, wanasiasa wa Jubilee wakiongozwa na Spika wa Seneti Ken Lusaka, Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito, Mwakilishi Mwanamke wa Trans Nzoia Janet Nangabo walisema kuwa ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga ni mwiba kwa Dkt Ruto kuwania urais 2022.

Wakizungumza wakati wa mkutano wa kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia wafanyabiashara wa Jua Kali mjini Kitale, wanasiasa hao walisema ushirikiano kati ya viongozi hao unatishia kusambaratisha chama tawala cha Jubilee.

Seneta Mbito alidai kuwa Naibu Rais Dkt Ruto ametengwa katika handisheki na akataka ajumuishwe.

“Handisheki kati ya Rais Uhuru na Raila ilisaidia kuleta utulivu na kuunganisha Wakenya, lakini sasa tunaona kuna ubaguzi na baadhi ya viongozi wametengwa,” akasema Dkt Mbito.

Spika Lusaka alisema Dkt Ruto ndiye kiongozi anayestahili na aliyehitimu kumrithi Rais Kenyatta 2022.

You can share this post!

Mashabiki wafurahia mechi za Super 8 Nairobi

Patashika leo K’Ogalo wakiwashukia Bandari katika KPL

adminleo