• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Nzoia kualika Stima, Leopards ikichuana na Sharks gozini KPL

Nzoia kualika Stima, Leopards ikichuana na Sharks gozini KPL

Na CHRIS ADUNGO

NZOIA Sugar watakuwa na kocha mpya watakaposhuka dimbani hii leo Jumatano kuvaana na Western Stima katika mchuano wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) uwanjani Sudi, Bungoma.

Kwa mujibu wa Yappets Mokua ambaye ni Mwenyekiti wa Nzoia, kubwa zaidi katika maazimio yao msimu huu ni kuwa miongoni mwa vikosi vitakavyofunga orodha ya tisa-bora jedwalini.

Kulingana naye, nafasi yoyote katika mduara huo itakuwa fahari na tija zaidi kwa kikosi chake ambacho kimelazimika kukabiliana na panda-shuka za kila sampuli msimu huu.

Baker Lukoya wa AFC Leopards (katikati) awapiga chenga wachezaji Geoffrey Shiveka (kulia) na James Mazembe katika mchuano wa awali wa Ligi Kuu ya KPL uliowakutanisha na Kariobangi Sharks ugani Kenyatta, Machakos mnamo Desemba 2018. Picha/ Kanyiri Wahito

Mbali na changamoto za kifedha, Nzoia wameathiriwa pakubwa na pigo la kubadilisha makocha mara kwa mara tangu kubanduka kwa mkufunzi Bernard Mwalala ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Bandari FC.

“Azma yetu ni kutinga mduara wa tisa-bora msimu huu. Hili halimaanishi kwamba hatuna msukumo wa kufanya vyema zaidi na kukabiliana vilivyo na ukubwa wa viwango vya ushindani. Ni malengo yaliyo na uhalisia hasa ikizingatiwa pandashuka zetu kufikia sasa,” akasema Mokua.

Nzoia wanashuka dimbani kuvaana na Stima wakijivunia alama 28 zinazowaweka katika nafasi ya 12 kutokana na mechi 23 zilizopita.

Baada ya kubanduka kwa Mwalala, Nzoia walimpokeza mikoba kocha Nicholas Muyoti aliyeagana na Thika United.

Katikati ya msimu, usimamizi ulimwajiri mkufunzi Godfrey ‘Solo’ Oduor aliyejaza nafasi ya Muyoti aliyeyoyomea kambini mwa Kakamega Homeboyz.

Kocha mshikilizi

Hadi Oduor alipopokezwa rasmi mikoba ya Nzoia, Edwin Sifuna aliaminiwa kuwa kocha mshikilizi wa kikosi hicho.

Oduor ambaye amewahi pia kuwatia makali vijana wa Kibera Black Stars alitambulishwa rasmi kwa wachezaji na mashabiki wa kikosi chake mnamo Aprili 22 na kibarua chake cha kwanza ni mechi ya leo dhidi ya Stima.

Nafuu zaidi kwa Oduor ni marejeo ya nyota Elvis Ronack na Stephen Etyang ambao kwa sasa wamepona majeraha. Wawili hao wanatarajiwa kuunga kikosi cha kwanza cha Nzoia.

Thomas Wanjala ambaye alikuwa mkekani awali, pia anatarajiwa kuwa tegemeo kubwa la Nzoia baada ya kuwaongoza waajiri wake kuwakomoa Mathare United 3-2 mwishoni mwa wiki.

Katika mchuano mwingine unaotarajiwa kuwasisimua zaidi mashabiki ni kivumbi kitakachowakutanisha Kariobangi Sharks na AFC Leopards uwanjani MISC Kasarani.

Mabingwa mara nne wa KPL, Ulinzi Stars watakuwa wenyeji wa Vihiga United ugani Afraha, Nakuru huku Chemelil Sugar wakipimana ubabe na wanabenki wa KCB uwanjani Kenyatta, Machakos.

Alhamisi itakuwa zamu ya Gor Mahia kuvaana na Mount Kenya United waliopo katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa muhula huu.

Ratiba ya KPL (Leo Jumanne):

Sharks na Leopards (3:00pm, MISC Kasarani)
KCB na Chemelil (3:00pm, Machakos)
Ulinzi Stars na Vihiga Utd (3:00pm, Nakuru), Nzoia Sugar na Stima (3:00pm, Sudi Bungoma)
(Kesho):
Mt Kenya Utd na Gor (3:00pm, Kenyatta, Machakos)

You can share this post!

Liverpool imani tele itatwaa ufalme Uingereza

KAULI YA WALIBORA: Kazi za Fasihi husemezana na kuathiriana

adminleo