• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Mutyambai atoa onyo kali kwa maafisa wa Knut wanaovuruga mafunzo ya mtaa kuhusu mtaala mpya

Mutyambai atoa onyo kali kwa maafisa wa Knut wanaovuruga mafunzo ya mtaa kuhusu mtaala mpya

Na CHARLES WASONGA

INSPEKTA Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai amewaonya viongozi wa  Chama cha kitaifa cha Walimu (Knut) dhidi ya kuvuruga mafunzo yanayoendelea kuhusu mtaala mpya wa elimu akisema watakamatwa na kushtakiwa.

Kwenye taarifa, Mutyambai amesema polisi hawataruhusu yeyote kuvuruga shughuli hiyo muhimu ya serikali.

Mutyambai amewaagiza makamanda wa polisi katika ngazi ya kaunti na kaunti ndogo, chini ya usimamizi wa washirikishi wa kimaeneo, kuhakikisha mafunzo hayo yaliyozinduliwa rasmi Jumanne na Waziri wa Elimu Profesa George Magoha yanaendelea bila kutatizwa.

Aidha, Mutyambai alitoa wito kwa wale wanaopinga mafunzo hayo kufuata utaratibu uliowekwa katika kuwasilisha malalamishi yao badala ya kuchukua sheria mikononi mwao.

Mnamo Jumatano, maafisa kadhaa wa Knut walikamatwa walipojaribu kuwachochea walimu kususia mafunzo hayo.

Kiongozi mmoja wa chama hicho alikamatwa  na kufikishwa mahakamani katika kaunti ya Makueni na wengine wanne wakakamatwa katika kaunti ya Kakamega.

Wakati huo huo, Waziri wa Elimu Prof George Magoha amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale waliovuruga vikao vya mafunzo kwa walimu kuhusu mtaala huo wa 2-6-3-3 katika baadhi ya vituo mnamo Jumanne.

Akiongea mjini Mombasa, Waziri Magoha alisema kwamba mafunzo hayo yamefanikiwa kwa asili mia 99.9 katika vituo mbalimbali nchini.

Profesa Magoha alisema lengo lake ni kuhakikisha walimu wamepata mafunzo ya kutosha ili kuwaelimisha wanafunzi ipasavyo.

Waziri aliongeza kuwa serikali imewekeza pakubwa katika mtaala mpya wa elimu, ambapo mafunzo hayo ya siku nne yatagharimu Sh900 milioni.

Walimu katika kaunti za Vihiga na Makueni Jumanne walipuuza mafunzo hayo.

Hata hivyo, shughuli hiyo iliendelea baraara katika vituo vingi humu nchini.

Serikali inalenga kutoa mafunzo kwa walimu 91,000 ambao watatekeleza mtaala huo katika madarasa ya chini, yaani Gredi ya 1 hadi Gredi ya 3.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya Kiswahili katika...

Raila kuwania urais 2022, asema Sifuna

adminleo