• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Raila kuwania urais 2022, asema Sifuna

Raila kuwania urais 2022, asema Sifuna

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM Jumatano kilitoa dalili za waziwazi kwamba kiongozi wake Raila Odinga huenda akawania uraia kwa mara ya tano katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna alisema hakuna kinachomzuia Waziri huyo Mkuu wa zamani kuwania urais ikiwa Wakenya wangali wanamuunga mkono.

“Ikiwa nyota ya Bw Odinga itang’aa mnamo 2022 atakapowania urais kwa mara ya tano, bado atatawazwa kuwa Rais wa tano nchini,” akasema Bw Sifuna.

Lakini, Bw Sifuna anasema hilo litategemea “mapenzi ya Wakenya”.

“Jakom (Bw Odinga) amesema ikiwa Wakenya wamechoshwa naye watamwambia aende nyumbani. Hata hivyo, kufikia sasa hawajamwambia hivyo. Amesema mara kadhaa kwamba ikiwa Wakenya watamtaka kuwania, atafuata agizo lao,” Bw Sifuna akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Katiba ya chama

Alisema uamuzi wa Bw Odinga kuwania urais hautakuwa kinyume na Katiba ya ODM licha ya manaibu wake wawili Magavana Hassan Joho (Mombasa) na Wycliffe Oparanya (Kakamega) pia kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho.

“ODM ni chama cha kidemokrasia kinachoongozwa na Katiba na kina kanuni za uteuzi. Wale wote waliotangaza kuwa watawania urais kwa udhamini wake sharti washiriki shughuli ya mchujo,” akasema Bw Sifuna.

Akaongeza: “Hata katika uchaguzi wa chama uliopita, Raila hakuchaguliwa bila kupingwa. Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati alishindania kiti cha kiongozi wa chama.”

Kauli ya Sifuna inajiri siku chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumtetea Bw Odinga dhidi ya madai kuwa anatumia muafaka kati yao kama ngazi ya kuwania urais 2022.

Madai hayo yamekuwa yakitolewa na Naibu Rais William Ruto pamoja na wandani wake ambao pia wanadai Bw Odinga anatumia muafaka huo kuvunja chama cha Jubilee kwa “manufaa yake kisiasa”.

Akiongea katika mkutano wa kujadili masuala ya miundo msingi katika ukumbi wa Bomas, Nairobi wiki jana, Rais Kenyatta alisema Bw Odinga hajawahi kumwambia kuwa anapania kuwania urais.

“Raila hajawahi kuniambia kwamba anatakuwa kuwania urais 2022. Na mimi pia sijamwambia kuwa nitasailia kitini baada ya 2022. Letu limekuwa ni ushirikiano unaolenga kuwasadia Wakenya,” akasema Rais Kenyatta akiwataka wanaopinga handisheki kutafuta kazi nyingine muhimu ya kufanya.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakihoji wajibu wa Bw Odinga katika serikali wakimtaka Rais Kenyatta kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo.

Tangu wawili hao wasalimiane nje ya Afisi ya Rais katika Jumba la Harambee mnamo Machi 9, 2018, Bw Odinga amekuwa akionekana kuwa na nafasi kuu serikalini.

Na kwa mara si moja amewahi kuwakilisha Rais na serikali ya Kenyatta katika shughuli mbalimbli nje ya nchi huku akipokelewa kwa taadhima na heshima na mabalozi wa Kenya katika mataifa husika.

Wiki hii ameshirikishwa katika ujumbe wa Serikali ya Kenya ulikwenda China kuhudhuria mkutano kuhusu miundo msingi na pia kuomba mkopo wa kiasi cha Sh363 bilioni za kufadhili ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Kisumu.

You can share this post!

Mutyambai atoa onyo kali kwa maafisa wa Knut wanaovuruga...

Taswira ya ukora wa polisi ulioishia mauti ya mshukiwa...

adminleo