• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Tathmini ya asili na miundo mbalimbali ya methali

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Tathmini ya asili na miundo mbalimbali ya methali

Na WANDERI KAMAU

METHALI ni kifungu cha maneno yanayotumiwa pamoja kisanii kwa njia ya kufumba au kutolea mfano na huchukua maana pana kuliko maneno yaliyotumiwa katika methali hiyo.

Methali huwa na maana ya juu na maana batini (ya ndani).

Methali hupokezanwa kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine. Ni kipera mojawapo cha semi.

Kwa kutumia methali moja tu, msimulizi huweza kutoa hadithi ndefu sana kudhihirisha maana na matumizi ya methali hiyo.

Muundo

Methali huwa na mpangilio wa maneno ambao hudhihirisha pande mbili za fikra.

Upande mmoja huonyesha hali, tendo au masharti. Hiki ndicho kisehemu cha kwanza katika methali. Kipande cha pili huonyesha matokeo ya tendo, hali au sharti hilo.

Kwa mfano, methali, ‘Zinguo la mtukutu ni ufito.’

Methali hii inatufahamisha ya kwamba njia ya kuondoa utundu (utukutu) ni kumwadhibu mtoto ili aache ubaya wake.

Hapa kuna hali na pia matokeo. Kuna methali za aina nyingi. Kuna methali zinazoonyesha falsafa za watu katika maisha yao, kuna za kuonya au kushauri na kutia moyo. Methali huelimisha na hupamba lugha inavyotumiwa ili ivutie.

Zinazofanana kimaana

Pia, kuna zile zinazofanana kimaana.

Kwa mfano:

(i) La kuvuna halina ubani. (Maana hapa ya kuvunda ni kuoza).

(ii) La kuvunda halina rubani. (Maana ya kuvunda hapa ni kuharibika).

(iii) Chombo cha kuzama hakina usukani.

(iv) Sikio la kufa halisikii dawa.

(v) Uso wa samaki hausikii viungo.

(vi) Liandikwa ndilo liwalo mja hana hiari.

(vii) Ajali haina kinga wala kafara.

(viii) Maji yakimwagika hayazoleki

Methali hizi zote zinatoa maana ya kuwa mtu ambaye ameharibika tabia hata ukijaribu kumrekebisha kwa kiasi kipi, unajisumbua bure tu.

Hutafanikiwa kwani ameota sugu.

Kwa kujaribu kumrudi, unaharibu wakati wako bure. Kuna methali zingine zinazotoa maana zilizo kinyume.

Kwa mfano, methali ‘Ivushayo ni mbovu’ ambayo hutoa maana ya kuwa mtu mwenye kusaidia watu hudharauliwa na watu hao, wasimwone kuwa ni mtu baada ya kufanikiwa kwa sababu ya msaada wa mtu huyo.

Wao hujigamba hata kama wasingalisaidiwa wangalifaulu tu. Kinyume cha methali hii ni methali, ‘Wema hauozi.’ Methali hiyo inamaanisha kwamba ukimtendea mtu mambo mazuri, wema wako utalipwa kwa njia moja ama nyingine siku moja.

Zinazokinzana

Mifano zaidi ya methali zenye maana zinazokinzana ni:

(i) Haraka haraka haina baraka na Ajizi ni nyumba ya njaa (Pole pole ndio mwendo, Chelewa chelewa utakuta mwana si wako)

(ii) Asante tupu haijazi chungu na mcheza kwao hutunzwa (Asante ya punda ni mateke).

(iii) Kutangulia si kufika

(iv) Mtoto wa nyoka ni nyoka. Mtoto wa simba ni simba. Msafiri ni aliye bandarini na moto hauzai moto.

(v) Ushikwapo shikamana na mwenye nguvu mpishe.

(vi) Mwenye kovu sidhani kapoa na kisima cha kale kisifukiwe.

(vii) Wa sitara hasumbuki, wa mbili havai moja na mgaagaa na upwa hali wali mkavu.

(viii) Juhudi si pato na jitihada huleta hekima.

(ix) Akutendaye mtende, mche asiyekutenda na adui mpende. Aidha, utajua asili ya methali fulani kulingana na msamiati uliotumiwa.

Kwa mfano:

(a) Kila mwacha samboye huenda alimwanamaji

(b) Sione tanga la nguo kasahau la miaa

(c) Dunia mwendo wa ngisi usiliwale Methali ya kwanza imetaja neon ‘samboye’ na mwanamaji’.

Neno ‘sambo’ hutoa maana ya chombo na hasa cha majini na neno ‘mwanamaji’ ni mtu anayefanya kazi katika chombo cha baharini kama vile meli, jahazi na kadhalika. Huyu huwa ni baharia.

Methali ya pili imetaja neno ‘tanga’ ambalo huhusishwa na vyombo vya majini.

Neno ‘tanga’ lamaanisha kitambaa kinachokingamishwa kwenye mlingoti wa chombo kama vile jahazi, kinachoteka upepo wa kikiwezesha chombo kwenda. Neno ‘miaa’ hutumiwa sana na watu wa Pwani.

Katika methali ya tatu, neno ‘ngisi’ ni aina mojawapo ya samaki wa baharini mwenye rangi nyeupe na anayetoka katika maeneo ya bahari kuu.

Kwa msingi huu basi, linalojitokeza ni kwamba muundo wa methali huathiriwa na masuala mengi. Tutaendeleza uchambuzi huu katika makala yajayo.

[email protected]

You can share this post!

AFC Leopards warukia nafasi ya 10 baada ya kutoka sare

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uhusiano uliopo kati ya...

adminleo