• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uhusiano uliopo kati ya Isimujamii na taaluma nyinginezo

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uhusiano uliopo kati ya Isimujamii na taaluma nyinginezo

Na MARY WANGARI

Uhusiano kati ya Isimujamii na Saikolojia

TAALUMA za isimujamii na saikolojia hushughulikia swala la mielekeo (attitudes) kuhusu aina fulani
za lugha.

Japo wanaisimujamii wanachunguza kwa kina swala la mielekeo kuhusu lugha ukweli ni kwamba ni jambo la kisaikolojia kwa kuwa lipo katika akili ya mtu.

Uchunguzi huu ni muhimu katika kueleza mabadiliko ya kiisimu yanayojitokeza katika lugha.

Aghalabu sababu hii hutumiwa kueleza kwa nini lahaja inabadilika, itabadilika lini na itabadilika kwa jinsi gani.

Nchini Kenya kwa mfano neno mama ‘mother’ hutamkwa kama mathe ili kuafikiana na mielekeo ya vijana kuhusu matamshi ya maneno fulani hasa mijini.

Wanasaikolojia hutueleza jinsi mtoto anavyojifunza lugha kupitia kwa uwezo maalumu anaozaliwa nao (innate capacity).

Hata hivyo, ni sharti tufahamu jinsi tofauti za kimazungumzo mathalan kijinsia zinavyokuzwa katika mchakato wa kuingiliana kijamii.

Uhusiano kati ya Isimujamii na Anthropolojia

Ni taaluma inayohusika na elimu inayohusu habari za asili na maendeleo yake ya awali. Taaluma hii inachukuliwa kuwa jinsi binadamu huyu alivyokuwa katika kikundi alikuwa anazungumza lugha fulani.

Wanaanthropolojia kadha wamefanya tafiti kadha zenye misingi ya kiisimu jamii.

Kwa mfano, kwa kuchunguza mfumo wa aila hujitokeza katika msamiati.Jamii nyingi za Kiafrika kwa mfano zina msamiati mpana unaoeleza uhusiano wa kiaila kuliko lugha za wazungu.

Kutokana na jambo hili tunaweza kufahamu mengi zaidi kuhusu jamii hizo. Lugha ya Kiingereza kwa mfanohuzungumzia aina moja tu ya shangazi (aunt) lakini katika lugha nyingi za Kiafrika kuna maneno ya uhusiano huu kwa upande wa baba na wa mama.

Uhusiano kati ya Isimujamii na Elimu

Wasomi hutarajiwa kutoa maamuzi kuhusu maswala yanayohusu lugha mathalan ufundishaji wa lugha sanifu.

Wanaisimu jamii wamekuwa na kibarua cha kuwashawishi wasomi kubadili mielekeo yao kuhusu lugha fulani zinazozungumzwa na watoto fulani shuleni mathalan lugha zao za kwanza.

Ni muhimu kwa wapangaji lugha kuwa na ufahamu fulani wa kiisimu ili waweze kutoa uamuzi unaofaa kuhusu aina ya lugha inayotakiwa kukuzwa na kuhimizwa katika miktadha anuai mathalan daraja, shule, dawati, ubao na kadhalika.

Uhusiano wa Isimujamii na Utamaduni

Wanaanthropolijia hushughulikia utamaduni ili kuweza kufafanua tabia za watu za kiisimu.

Jukumu la wanaisimu jamii ni kuoanisha lugha na utamaduni kwa kuzingatia sarufi.

Uhusiano kati ya taaluma hizi mbili unatokana na haja ya kuyaelewa makundi mbalimbali ya watu.

Hii ina maana kwamba ni muhali kwa wanaanthropolojia kuchunguza jamii za kale pasipo kutilia maanani lugha za watu husika. Aidha, ni vigumu kuchunguza lugha bila kuzingatia uamilifu wa mazungumzo fulani katika jamii.

Kwa muktadha wa lugha, maana ya ujumbe ni lile jambo linalowasilishwa kila mara mwanajamii anapozungumza.

Kwa upande mwingine, tunapoangazia tabia za kijamii, maana ni kitu ambacho kimewasilishwa wakati mwanajamii fulani ametenda jambo fulani kitendo cha kitamaduni.

Hivyo basi, lugha na utamaduni ni tabia za binadamu. Mtazamo wa kipragmatiki hutupa zaidi ya ile maana ya maneno.

Unaangazia vikwazo vya kijamii vilevile anavyoafikiana navyo mtumiaji wa lugha ikiwemo athari nyinginezo za kijamii katika matumizi ya lugha.

Uhusiano kati ya Isimujamii na Sosholojia (Elimu jamii)

Wanaisimu jamii hutalii miundo ya kijamii na namna miundo hiyo inavyoathiri lugha.

Kuna nguvu fulani za kijamii ambazo husababisha wanajamii kutaka kuongea au kutamka maneno kwa njia fulani.

Mkondo unaochukuliwa na kibadala (variant) fulani cha kiisimu katika jamii si jambo linalojitokeza kiholela tu bali ni kitu kinachotokana na tathmini za kijamii.

Uchaguzi wa kipashio fulani cha kiisimu unatokana na jinsi jamii inavyochukulia kipashio hicho. Lugha hutueleza mengi kuhusu mtu katika jamii.

Ni vyema kutilia maanani kwamba kwa kuwa jamii ni taaluma na inayohusika na jamii moja kwa moja, ina uwezo wa kuhusiana na taaluma chungu nzima.

Wasomi anuai mathalan Greenberg (1957), Hymes (1974) , Dik (1978) na kadhalika, wanaangazia lugha kwa mitazamo miwili ambayo ni mtazamo wa kiisimu na mtazamo kiisimu jamii.

Mtazamo wa kiisimu – lugha inaelezwa kuwa ni mfumo wa sauti nasibu zinazotumiwa na watu wa jamii fulani wenye utamaduni unaofanana ili kuwasiliana.

Mtazamo huu unachukulia lugha kuwa kitu halisi ambacho kinaweza kuainishwa katika vipande sauti vidogo vidogo ambavyo kwa pamoja huunda mfumo wa lugha wa mawasiliano.

[email protected]

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Tathmini ya asili na miundo...

AKILIMALI: Migomba 220 ya ndizi imekuwa mbinu thabiti ya...

adminleo