• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
MBURU: Mazoea ya serikali kulazimishia wananchi mambo yanakera

MBURU: Mazoea ya serikali kulazimishia wananchi mambo yanakera

Na PETER MBURU

SERIKALI imekuwa na mtindo wa kuwawekelea Wakenya mizigo ya kiuchumi kila inapotaka, bila kuwaomba ushauri wala kujali wanavyoathirika.

Kwa mara kadhaa sasa, serikali imetekeleza ama kupanga kutekeleza mambo ambayo yanamwathiri mwananchi kiuchumi kwa viwango vikubwa, huku ikiziba masikio kwa vilio vya Wakenya wanaposema kuwa wanaumia.

Mwaka jana, serikali ilipandisha ushuru wa bidhaa za mafuta kwa asilimia nane, hali ambayo ilisababisha bei za bidhaa nyingi kupanda.

Hii ilikuwa licha ya wananchi pamoja na wengi wa wabunge kupinga hatua hiyo, ambayo waliilalamikia kuwa ingeharibu zaidi hali ya maisha kwa mwananchi wa kawaida. Ni hali ambayo ilipelekea wabunge kuandamana bungeni na raia nje ya bunge.

Lakini Rais Uhuru Kenyatta licha ya hayo aliendelea kuiidhinisha kuwa sheria na tangu wakati huo, Wakenya wamekuwa wakilipa ushuru huo.

Vilevile, Wakenya wamekuwa wakikosoa serikali kuhusu hali ya kukopa mabilioni ya pesa kila wakati, ilhali pesa hizo zinaishia kuporwa na maafisa wake, badala ya kutumiwa kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo itafaa nchi na kuikuza.

Licha ya malalamiko ya wananchi, serikali, ikiongozwa na Rais imejitia hamnazo na kuendelea kukopa, huku kila uchao habari kuhusu jinsi pesa za umma zinaibiwa zikizidi kufichuliwa na asasi za uchunguzi.

Hata wiki hii, Rais pamoja na kiongozi wa ODM walisafiri hadi nchini China kwa ajili ya kutafuta mkopo wa Sh360 bilioni wa kugharamia ujenzi wa reli ya SGR ya kutoka Naivasha hadi Kisumu.

Serikali aidha imeshtakiwa na wafanyakazi na waajiri, kuhusu mpango wake wa kutaka kuwatoza pesa, kwa madai kuwa inataka kufadhili ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.

Hata hivyo, Wakenya wamepinga vikali mpango huo wa serikali, kwa kuwa unaonyesha kutoka mwanzo kuwa kuna mapengo makubwa yatakayopelekea aidha pesa za umma kuporwa, ama watu kutopata nyumba ambazo serikali inawalazimisha kulipia.

Serikali inadai kuwa itakuwa lazima kwa mtu kukatwa mshahara kulipia nyumba hizo, lakini wakati wa kupewa itawabidi watu kushiriki mfumo wa Kamari ambapo watakaoshinda pekee ndio watamiliki.

Tabia hii ya serikali kutumia kifua kila inapotaka kufanya jambo inachukiza, kuiharibia sifa mbele ya macho ya wananchi na kuiletea aibu.

Sharti serikali iwe ikiwahusisha wananchi katika mambo inayotaka kufanya, haswa ikiwa yanawahusu, badala ya kuwalazimisha kwani nyakati nyingi watu wanaishia kulia na kuumia.

You can share this post!

WANDERI: Umoja ni nguzo kuu kwa wanaotetea mapinduzi

TAHARIRI: Sheria kuhusu Naibu Gavana irekebishwe

adminleo