• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
MWANAMKE MWELEDI: Sura ya taaluma ya Elimu nchini Kenya

MWANAMKE MWELEDI: Sura ya taaluma ya Elimu nchini Kenya

Na KENYA YEARBOOK

KWA miaka mingi amewakilisha sura ya taaluma ya elimu hapa Kenya.

Ni suala ambalo limemfanya Dkt Eddah Gachukia kutambuliwa kama mojawapo ya wataalam wa elimu wanaoheshimika nchini.

Mchango wake katika elimu umedhihirika kupitia uandishi wake wa vitabu vya watoto, kusaidia katika kuunda mtaala na pia kuratibu ustawi wa mpango wa Tujifunze Kusoma Kikwetu (TKK), uliohusika hasa katika kufunza kusoma kupitia lugha asili katika miaka mitatu ya kwanza.

Mwaka wa 2003 alikuwa mwenyekiti wa jopo kuhusu utekelezaji wa masomo ya shule ya msingi bila malipo.

Aidha, pamoja na mumewe, Daniel Gachukia, wao ndio waanzilishi wa msururu wa shule za Riara Group of Schools, vile vile Chuo Kikuu cha Riara.

Sio hayo tu, Dkt Gachukia pia ametambulika kutokana na mchango wake kama mwanaharakati wa ustawi wa kijinsia. Yeye ni mwanzilishi wa baadhi ya vyama maarufu kama vile Maendeleo Ya Wanawake ambapo alihudumu kama naibu mwenyekiti na katibu wa kitaifa. Pia, alihusika pakubwa katika kuanzishwa kwa chama cha Forum for African Women Educationists (Fawe), chama ambacho kwa sasa kiko katika mataifa 35, vilevile Baraza la kitaifa la wanawake, miongoni mwa vyama vingine.

Baadhi ya michango ya ustawi aliyochangia katika miaka ya 1970 na 1980 kama mwanachama wa Maendeleo ya Wanawake ilikuwa kuleta maji karibu na maboma, vilevile afya ya uzazi.

“Mamangu alifariki akijifungua. Hilo limekuwa chocheo langu kuu katika kupigania afya ya uzazi.”

Penzi lake katika masuala ya wanawake na watoto, liliendelea kupitia masuala aliyopigania katika kipindi cha miaka kumi aliyohudumu kama mbunge.

Safari ya Dkt Gachukia katika masuala ya ustawi wa elimu, jinsia na maendeleo ilianza akiwa bado mdogo kiumri.

Mojawapo ya sababu zilizomfanya kukita mizizi katika masuala ya elimu, ni kwamba wazazi wake wote pia walikuwa na kisomo.

“Babangu alikuwa na maono. Alikuwa mwalimu jijini Nairobi, kazi aliyojitolea kuifanya kwa moyo wote licha ya kwamba hakuwa na mshahara mwingi. Mamangu pia alikuwa ameenda shuleni ambapo wakati mmoja alikuwa mwanafunzi wa shule ya upili ya wasichana ya Mary Leaky na kupita mtihani wake, na nakumbuka akinifunza kuandika kwenye jivu,” akumbuka.

Japo mamake alifariki katika miaka yake ya awali shuleni, Dkt Gachukia aliweza kukamilisha mtihani wake wa Common Entrance Examination. Hii ilimaanisha kwamba angeendelea kwa kile kilichofahamika kama primary top school.

Kisha alijiunga na shule katika eneo la Kiambaa iliyokuwa mbali na nyumbani kwao.

Msomi maarufu Eddah Gachukia. Picha/ Maktaba

Ili kukabiliana na changamoto ya mwendo mrefu, babake alimpeleka katika shule ya mabweni ya Mambere School, (inayofahamika kwa sasa kama Musa Gitau Girls Secondary School) eneo la Kikuyu.

“Mwalimu mkuu aliniangalia na mwanzoni alikataa kuniruhusu kuingia akidai kwamba nilikuwa mdogo sana. Tayari dadangu alikuwa anasoma hapo na nilikuwa na kiu ya kutaka kuungana naye,” aeleza.

Lakini haukuwa mteremko kwake.

Kwa mshangao wa wengi, Dkt Gachukia alianguka mtihani wake wa shule ya msingi mara ya kwanza.

Hata hivyo, kutokana na sababu kwamba alikuwa akifurahia maisha ya shuleni sana, alifanyiwa majaribio ya kujiunga na kiwango cha ualimu cha P4 ambacho kilikuwa cha chini zaidi.

Hata hivyo alikataliwa kwani alikuwa mfupi sana kiasi cha kwamba hakuwa anaweza kuandika kwenye ubao. Kwa hivyo, ilimbidi kurudia mtihani huo ambapo alipita wakati huu.

Baada ya hapa, alijiunga na Shule ya African Girls High School inayofahamika kwa sasa kama Alliance Girls High School.

Shule hii ilikuwa ikichukua wanafunzi wawili pekee kutoka kila wilaya, na hivyo Dkt Gachukia alibahatika kuwa mmoja wao.

Ishara za uthabiti wake kama kiongozi zilianza kujitokeza hapa ambapo akiwa shuleni, alipewa jukumu la kuwapelekea wanafunzi wenzake barua.

Pia, alianzisha chama cha drama kilichoshiriki katika tamasha ya kitaifa ya muziki na kushinda kitengo cha muziki wa kitamaduni.

Mojawapo ya sababu zilizomfanya kuelekeza mawazo yake katika kuleta usawa kati ya wasichana na wavulana, ilikuwa majukumu aliyokumbana nayo nyumbani. Katika mazingira ya mashambani, alikumbwa na matatizo ya kufanya kazi za nyumbani.

“Nilijaribu sana kubeba maji lakini kila mara nilikumbwa na uchungu shingoni. Wavulana hawakuwa wanafanya kazi za aina hii. Ndugu zangu walikumbwa na jukumu la kupeleka ng’ombe malishoni pekee, ilhali wasichana walikumbwa na majukumu mengi. Ikiwa umepitia changamoto za aina hii, unakumbwa na ari ya kutaka kushiriki katika kuleta mabadiliko kwa wanawake na wasichana.”

Mwaka wa 1963 alijiunga na chuo kikuu cha Leeds kupitia ufadhili wa British Council scholarship, ambapo alipata hati ya kufunza Kiingereza.

You can share this post!

‘Miaka 60 ya kukupasha habari’

SHANGAZI AKUJIBU: Rafiki ya mpenzi ataka kuniona chemba

adminleo