• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Maambukizi ya HIV kutoka kwa mama hadi mtoto yaongezeka

Maambukizi ya HIV kutoka kwa mama hadi mtoto yaongezeka

 Na GEORGE MUNENE

BARAZA la Kudhibiti Maradhi ya Ukimwi (NACC) limeelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la maambukizi ya virusi vya HIV kutoka kwa mama hadi kwa mtoto kote nchini.

Kulingana na afisa wa NACC Caroline Kinoti, maambukizi ya virusi vya HIV kutoka kwa mama hadi watoto ambao wangali tumboni yameongezeka kutoka asilimia nane hadi 11 kote nchini.

Bi Kinoti alisema kuwa hali hiyo imechangiwa na migomo ya wahudumu wa afya ya mara kwa mara.

“Maambukizi ya virusi vya HIV kutoka kwa mama hadi mtoto yalianza kuongezeka wakati madaktari na wauguzi waligoma wakitaka kuongezewa mshahara,” akasema Bi Kinoti.

Akizungumza mjini Embu jana wakati wa warsha ya siku mbili ya wahudumu wa afya kutoka Kaunti za Isiolo, Meru, Tharaka-nithi na Embu, Bi Kinoti alisema kuwa NACC imeanza mikakati ya kutaka kupunguza maambukizi hayo hadi asilimia tano.

“Wakati wa migomo ya wahudumu wa afya, akina mama wajawazito hukosa huduma muhimu ambazo zingezuia watoto walio tumboni kuambukizwa virusi vya HIV,” akasema Bi Kinoti.

Alisema kuwa migomo ya wahudumu wa afya ya mara kwa mara aghalabu hutatiza juhudi za serikali kutaka kuhakikisha kuwa watoto wote wanazaliwa salama bila kuambukizwa virusi vya HIV.

Afisa huyo wa NACC pia aliwataka Wakenya kuzingatia matumizi ya mipira ya kondomu wanapofanya tendo la ngono ili kuzuia maambukizi mapya ya HIV.

“Ili kupunguza maambukizi mapya kuna haja ya kuongeza juhudi za kuhimiza watu kutumia kinga kama vile kondomu wakati wa ngono. Watu pia wanafaa kuhamasishwa kuhusu matumizi sahihi ya kondomu,” akasema.

Mjumbe wa bodi ya NACC, Lattif Shaban, alishutumu wanaume kwa kuwa kizingiti katika vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya HIV.

Alisema baadhi ya wanaume, haswa kutoka maeneo ya Kaskazini Mashariki ya Kenya hawataki kupimwa HIV na wanakataza wake zao kupimwa kutokana na mila za kitamaduni zilizopitwa na wakati.

You can share this post!

SGR: Hisia mseto zaibuka Magharibi Rais akikosa mkopo

Nanok aomba chakula cha kuvutia watu kujisajili Huduma...

adminleo