• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Kalonzo ataka sheria kuhusu utajiri wa viongozi ibuniwe

Kalonzo ataka sheria kuhusu utajiri wa viongozi ibuniwe

Na BENSON MATHEKA

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Jumatano aliwataka wabunge watunge na kupitisha sheria ya kulazimisha watumishi wote wa umma kuchunguzwa mitindo yao ya maisha.

Akihutubu jijini Nairobi wakati wa sherehe za mwaka huu za Leba Dei, Bw Musyoka alisema kukosekana kwa sheria hiyo kulizima agizo la Rais Uhuru Kenyatta la kutaka mitindo ya maisha ya watumishi wa umma ichunguzwe.

“Tukisema kila mara watu wafanyiwe uchunguzi wa mitindo yao ya maisha, tutakuwa tukifanya kazi ya bure bila sheria ya kulazimisha maafisa wa umma wafanyiwe uchunguzi huo. Hiki ndicho kizingiti ambacho Rais alikumbana nacho,” alisema Bw Musyoka.

Alisema inasikitisha baadhi ya watu huwa wanapata utajiri wa haraka baada ya kupata wadhifa wa umma na ipo haja ya kuwepo kwa sheria ya kulazimisha kila anayejiunga na serikali kukaguliwa. “Watu wanafaa kujua kiwango cha pesa ambacho watu huwa nacho kabla ya kupata wadhifa wa umma na jinsi wanavyopata mali wakijiunga na utumishi wa umma,” alieleza Bw Musyoka.

Alisema sheria hiyo itawamlika maafisa wa serikali jinsi wanavyopata mali wakiwa ofisini.

“Nimesikia watu wakisema wanataka uchunguzi wa mitindo ya maisha lakini tusipokuwa na sheria ya kueleza uchunguzi wa mitindo ya maisha, hatutafanikiwa,” alisema Bw Musyoka.

Alisifu wanaharakati walioandamana jijini Nairobi Jumanne kutaka ufisadi uangamizwe akisema mahakama zinapaswa kuhakikisha wanaoshtakiwa wanaadhibiwa vikali wakipatikana na hatia. “Tunataka kuona watu wakitupwa jela kwa kuiba mali ya umma,” alisema.

Alisema hayo baada ya kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi ambaye pia alihudhuria sherehe hizo katika bustani ya Uhuru Park, kusema mitindo ya maisha ya watumishi wote wa umma inafaa kuchunguzwa ili kujua wanaopora mali ya umma.

Kulingana na Bw Mudavadi, maafisa wa serikali wamekuwa wakitajirika kwa kupora mali ya umma na uchunguzi huo utafichua wanaohusika badala ya kusifu muafaka kati ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga na Rais Kenyatta ambao viongozi wanadai ulifanikisha vita hivyo.

“Tumesikia mengi ya kusifu handisheki, hata hivyo hiyo haitoshi kupiga vita ufisadi, tunataka kuona watu wakuu serikalini wakitiwa pingu. Tumechoka, Wakenya wamechoka kunyonywa jasho lao licha ya kufanya kazi kwa bidii,” alisema Bw Mudavadi.

Bw Musyoka aliyesimama kuhutubia wafanyakazi baada ya Bw Mudavadi alisema uchunguzi wa mitindo ya maisha hauwezi kufaulu bila sheria ya kuufanikisha.

Mwaka jana, baadhi ya viongozi, wakiwemo wabunge walipinga vikali agizo la rais kwamba mitindo ya maisha ya maafisa wote wa serikali ichunguzwe kama njia moja ya kutambua wale wanaohusika na ufisadi.

Alisema uchunguzi huo ungeanza na yeye binafsi, naibu wake William Ruto, mawaziri na maafisa wote wa serikali yake.

Wabunge wanaomuunga Naibu Rais William Ruto walipinga agizo hilo wakisema lililenga baadhi ya maafisa wa serikali na kwamba halina msingi wa kisheria.

You can share this post!

Wachache wajitokeza kuadhimisha siku ya Leba Dei

Wakazi wakatakata chifu na kuchoma mwili wake

adminleo