• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Bajeti ya Baba Yao yaacha maseneta vinywa wazi

Bajeti ya Baba Yao yaacha maseneta vinywa wazi

Na PETER MBURU

GAVANA wa Kiambu Ferdinand Waititu Alhamisi aliacha maseneta kwenye hali ya mshangao, ilipobainika kuwa kaunti yake mwaka uliopita ilitenga bajeti ya kufadhili miradi ya kitaifa na kimataifa.

Walipokuwa wakidurusu nakala za ukaguzi wa matumizi ya pesa ya kaunti ya Kiambu mwaka wa 2017/18, wakati Bw Waititu alifika mbele yao, wanachama wa Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu matumizi ya pesa za umma walishangaa kuona kuwa serikali ya Gavana Waititu ilitumia zaidi ya Sh1 bilioni kufadhili miradi ya ikulu na serikali kuu.

Katika nakala za kuonyesha jinsi kaunti hiyo ilitumia bajeti yake mwaka jana, maseneta waligundua kuwa kaunti ilitumia Sh902 milioni kufadhili shughuli za ikulu, Sh180 milioni kuwalipa marupurupu Marais Wastaafu, Sh573 milioni kwa shughuli za ushauri kwa mashirika ya serikali, Sh58 milioni kwa huduma za kutafuta amani nchini Sudan Kusini na Sh804 milioni zikatengwa (Sh493 milioni zililipwa), kufadhili mfumo wa elimu bila malipo wa shule za msingi.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa matumizi ya pesa za umma kuhusu kaunti hiyo vilevile ilionyesha kuwa, kulikuwa na tofauti kati ya kiwango cha pesa zilizotumiwa na kaunti na rekodi za mfumo wa malipo kwa njia ya kielektroniki (IFMIS), kwa kiwango cha Sh800 milioni.

Matukio hayo yaliwalazimu maseneta kwa sauti moja kutaka ukaguzi mpya ufanyiwe matumizi ya serikali ya kaunti hiyo mwaka jana, baada ripoti ya afisi ya Mkaguzi Mkuu kudai kuwa matumizi ya pesa kaunti hiyo yalikuwa sawa (qualified opinion).

“Tunakataa ripoti ya Mkaguzi Mkuu kuwa matumizi ya pesa za kaunti Kiambu yalikuwa sawa, haiwezi kuwa hivyo. Mkaguzi Mkuu afanye ukaguzi spesheli wa Kaunti ya Kiambu kuhusu matumizi ya pesa mwaka wa 2017/18 ndani ya siku 45,” mwenyekiti wa kamati hiyo Moses Kajwang akasema.

Gavana Waititu, hata hivyo, alijitetea kuwa hafahamu lolote kuhusu matumizi hayo ya pesa, licha ya kuwa nakala zilizowasilishwa mbele ya kamati, na pia aliyokuwa akitumia zilikuwa na habari hizo.

“Naona kama kulikuwa na mpango wa kuingiza nakala hizi katika ripoti ili kunichafulia jina. Hakuna pesa zozote zimelipwa kwa shughuli za ikulu, kugharamia mfumo wa elimu bila malipo ama kutafuta amani Sudan Kusini,” akasema gavana huyo.

Lakini nakala za matumizi hayo zilikuwa zimetiwa sahihi na maafisa wa kaunti yake na ndizo ziliwasilishwa kwa Mkaguzi Mkuu.

You can share this post!

Ndani siku 14 kwa kuua mkewe Leba Dei

Polisi wanaoshukiwa kuiba hela ATM za Barclays kizimbani

adminleo