• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 8:27 PM
WASONGA: Kaunti zinaua ndoto ya ugatuzi Wakenya wakitazama

WASONGA: Kaunti zinaua ndoto ya ugatuzi Wakenya wakitazama

Na CHARLES WASONGA

SABABU kuu ya kupitishwa kwa katiba ambayo Kenya inatumia sasa na kuundwa kwa serikali za kaunti ilikuwa kupeleka huduma za serikali karibu na mwananchi, baada ya miaka mingi ya Wakenya kuteseka.

Ugatuzi ulikuwa matunda ya maono ya miaka mingi ya baba zetu, ambao waliishi kupigania uongozi wa serikali kumkaribia mwananchi, kinyume na mbeleni ambapo watu walipotaka misaada fulani muhimu walilazimika kuitafuta Jiji kuu la Nairobi.

Ni kwa sababu hiyo ndipo viongozi mbalimbali, wa kisiasa, kibiashara na hata kidini waliungana mnamo 2010 kuhakikisha kuwa Wakenya wameipitisha katiba hii, angalau mwananchi naye ajivunie matunda ya ushuru anaolipa.

Lakini karibu miaka kumi baadaye, serikali za ugatuzi bado zinakumbwa na changamoto si haba, nyingi zikiwa zinazosababishwa na viongozi ambao wananchi wamewaaminia kuwawakilisha kutunza rasilimali zao.

Licha ya serikali kupelekwa karibu na wananchi, bado Wakenya wengi wanaishi kwa matatizo waliyokuwa nayo hata kabla ya katiba mpya kupitishwa.

Cha kushangaza zaidi ni baadhi ya masuala yanayoshuhudiwa katika serikali za kaunti, ambapo magavana wanaripotiwa kutumia pesa za mlipa ushuru isivyofaa, na katika mambo ya kuchukiza.

Kisa cha Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu ambaye alishindwa kueleza Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu Uhasibu jinsi zaidi ya Sh1 bilioni zilitumiwa na kaunti yake wiki iliyopita ni mfano mzuri.

Licha ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya Pesa za Umma Edward Ouko kuonyesha kuwa serikali ya Gavana Waititu ilitumia mamilioni ya pesa kugharamia shughuli za serikali kuu kama Elimu ya Shule za Msingi bila malipo na juhudi za kutafuta amani Sudan Kusini, Gavana Waititu hakufafanua jinsi pesa hizo zilitumika.

Serikali za kaunti zingine aidha zimekosolewa na afisi ya Bw Ouko kwa kutumia vibaya pesa za walipa ushuru, wiki jana aidha serikali ya kaunti ya Embu ikilaumiwa kuwa zaidi ya Sh3 bilioni hazikuelezeka jinsi zilitumika.

Magavana zaidi wanatarajiwa kufika mbele ya kamati hiyo ya Seneti leo na siku zijazo na Wakenya watazidi kushtuka, wakisikia jinsi pesa zao zilitumika.

Sharti viongozi wote katika kaunti wawajibike ili kutimiza maono yaliyolengwa wakati ugatuzi ulipoletwa, ya kuwaletea karibu zaidi matunda ya serikali wananchi, na kutumia kila shilingi ya mlipa ushuru ipasavyo.

You can share this post!

Raila apongeza kanisa la ACK kwa kukataa pesa za ufisadi

Amlima mwenzake aliyefichulia mume siri

adminleo