• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Ruto amtetea Baba Yao kuhusu bajeti tata ya kaunti

Ruto amtetea Baba Yao kuhusu bajeti tata ya kaunti

Na PETER MBURU

NAIBU Rais William Ruto Jumapili alimtetea Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu kutokana na kashfa na wito kuwa ajiuzulu, kuhusiana na habari katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa matumizi ya pesa za umma kuwa serikali ya kaunti yake ilitumia zaidi ya Sh1 bilioni kugharimia miradi isiyoruhusiwa.

Katika ripoti hiyo ya Mkaguzi Mkuu, ilibainika kuwa kwenye bajeti ya serikali ya Kaunti ya Kiambu, Sh58 milioni zilitumiwa kufadhili shughuli za kutafuta amani nchini Sudan Kusini, Sh973 milioni kufadhili shughuli za ikulu, Sh180 milioni kulipa marais wastaafu marupurupu na Sh804 milioni kugharimia elimu ya bure kwa shule za msingi.

Lakini Dkt Ruto jana alimtetea Gavana Waititu akisema hana makosa yoyote, na kuongeza kuwa serikali kuu itajibu maswali kuhusu matumizi hayo.

“Mambo ya marais wastaafu, mambo ya ikulu tutajibu. Huyu Baba Yao asibebeshwe msalaba ambao sio wake, aulizwe ya Kiambu, nayo ya serikali kuu sisi tuulizwe. Kwa hivyo, wewe Baba Yao usiwe na wasiwasi, hiyo ya Sudan Kusini na marais wastaafu sisi tutajibu, wewe pambana na hii ya Kiambu,” Naibu Rais akasema alipokuwa akihutubu katika hafla eneo la Githunguri, Kaunti ya Kiambu.

Matamshi hayo ya Dkt Ruto yalikuja wakati shinikizo zikiwa juu dhidi ya Gavana Waititu kuwa ajiuzulu, baada ya habari kuhusu muundo wa bajeti hiyo kuwekwa wazi mnamo Alhamisi, wakati gavana huyo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu Uhasibu, kujibu maswali kuhusu matumizi ya pesa ya mwaka wa Fedha 2017/18.

Bw Waititu naye aliendelea kujitetea kuwa hakuna matumizi kama hayo yaliyofanywa na serikali yake, akidai kuwa kujihusisha kwake na kikosi cha Tanga Tanga ndiko kunawafanya baadhi ya watu kumwinda.

“Mimi ‘nachorewa’ kwa kila njia kwa sababu ya kuonekana niko Tanga Tanga lakini nakuhakikishia Naibu Rais kuwa sikuachi,” akasema gavana huyo jana.

Baadhi ya Wakenya, hata hivyo, hawakufurahishwa na hali ya Naibu Rais kumtetea Gavana Waititu, nao wakazi wengine wa Kiambu wakaendeleza wito kuwa gavana huyo ajiuzulu kwa kushindwa kuendesha serikali yake.

“Sasa Dkt Ruto akiwa Rais na Waititu naibu wake si wizara ya Fedha itatoa pesa kufadhili mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia kati ya (Donald) Trump (Rais wa Amerika) na Korea Kusini,” akashangaa Erick Atitwa.

You can share this post!

Raila arejea kwa Moi

Karani wa korti auawa kwa njia ya kusikitisha

adminleo