• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Hofu muungano unapendekezwa kumzima Ruto

Hofu muungano unapendekezwa kumzima Ruto

Na VITALIS KIMUTAI

KAMBI ya Naibu Rais William Ruto imepata pigo kufuatia pendekezo la kundi la wabunge wa Jubilee, kubuni muungano mpya na chama cha ODM, kulenga uchaguzi mkuu wa 2022.

Pendekezo hilo limemweka Dkt Ruto katika hali ngumu kwani linajiri miezi miwili baada ya kiongozi huyo kupinga uwezekano wa vyama hivyo kuungana “sasa au miaka ijayo kwa sababu manifesto zao ni tofauti sawa na sera.”

Aidha, pendekezo hilo linajiri wakati ambapo baadhi ya wabunge wa Jubilee wanamlaumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kukosa kuitisha mkutano wa kundi la wabunge wa Jubilee (PG), tangu uchaguzi mkuu uliopita, huku wabunge hao wakiendelea kuchukua misimamo tofauti kuhusu masuala ya kitaifa.

Mbunge maalum Maina Kamanda, Nduati Ngugi (Gatanga) na aliyekuwa mbunge wa Mukurwe-ini Kabando wa Kabando, wamekubaliana kuwa muungano unalenga kuwaleta pamoja, kisiasa, Rais Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, huku ukimtenga Dkt Ruto.

Ingawa wabunge kadhaa wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais wamepuuzilia mbali pendekezo la kubuniwa kwa muungano wa Jubilee na ODM, wamesisitiza kuwa hawatakihama chama hicho tawala hata kama muungano huo utafaulu.

Walisema kuwa watasalia ndani ya Jubilee na kuendelea “kupigania haki yetu kutoka ndani”.

Mbunge wa Kipkelion Magharibi, Bw Hillary Koskei na mwenzake wa Belgut, Bw Nelson Koech walisema wandani wa Dkt Ruto na wafuasi wao hawatagura Jubilee licha ya dalili za kusambaratika kwake kabla ya uchaguzi mkuu ujao kuendelea kuonekana.

“Sisi ni wadau wakuu wa Jubilee kilichobuniwa baada ya kuvunjwa kwa chama cha United Republican Party (URP) na The National Alliance (TNA) na vyama vinginevyo kwa lengo la kuunda chama kimoja ambacho hatuna nia ya kukihama,” akasema Bw Koech.

Bw Koskei alisema kuwa mazungumzo kuhusu miungano na misimamo tofauti miongoni mwa wanachama wa Jubilee na viongozi ni ishara ya kupanuka kwa nafasi ya demokrasia ndani ya Jubilee.

“Kwa wale mnaopania kumrithi Rais Kenyatta katika Ikulu mnamo 2022, mwapaswa kujua kuwa gari moshi tayari limeondoka stesheni na tunalisubiri kukamilisha safari huku dereva wake akiwa Naibu Rais,” akasema Mwakilishi wa kike wa kaunti ya Laikipia, Bi Catherine Waruguru.

Kauli yake inalingana na ya mwenzake wa Isiolo, Bi Rehema Jaldesa, kuwa jamii ya wafugaji itaunga mkono azma ya Dkt Ruto kumrithi Rais.

Kinachojitokeza ni kwamba wandani wa Dkt Ruto hawako tayari kushiriki katika muungano na Bw Odinga kwa sababu ya yale waliyopitia ODM kabla ya URP kubuniwa.

“Bw Odinga ni ndumakuwili ambaye hupenda kusababisha mzozo na hana ajenda yoyote kwa taifa hili. Kuna watu nchini ambao sharti wafahamu kwamba watawasaidia wengine kuongoza lakini wao hawatawahi kuongoza,” akasema Mbunge wa Bomet ya Kati, Bw Ronald Tonui.

You can share this post!

Karani wa korti auawa kwa njia ya kusikitisha

NASAHA: Ni nini hekima ya Waislamu kulazimika kufunga...

adminleo