• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Onyo mvua kubwa itanyesha juma hili

Onyo mvua kubwa itanyesha juma hili

Na BERNARDINE MUTANU

Mtabiri wa hali ya hewa ameonya kuhusiana na mvua kubwa na mafuriko ya gharika yatakayokumba baadhi ya maeneo nchini siku tatu zijazo.

Eneo la Pwani litaathirika zaidi kulingana na utabiri wa hivi punde kutoka kwa Idara ya Utabiri wa hali ya Hewa (KMD).

Mvua itaongezeka kuelekea Jumanne, ilisema idara hiyo katika ripoti. Jana, idara hiyo ilisema eneo la Pwani lingepokea mvua kufikia milimita 20. Leo, mvua itaongezeka kufikia milimita 30 na Jumanne, mvua itanyesha milimita 40 eneo la kusini mwa Pwani na maeneo ya karibu.

“Mvua inatarajiwa kupungua kuanzia Jumatano na huenda ikaandamana na upepo mkali na huenda ikasababisha mafuriko katika maeneo ya karibu na ufuoni na hifadhi za maji,” alisema mkurugenzi mkuu wa KMD Stella Aura katika ripoti hiyo. Jumatatu na Jumanne, mvua ya kiwango cha wastani hadi kiwango cha juu inatarajiwa Lamu, Kilifi, Mombasa, Kwale na kusini mwa Kaunti ya Tana River.

“Wakazi wa maeneo hayo wanashauriwa kuwa makini kuhusiana na mafuriko ya gharika,” ilionya KMD. Watu pia walionywa kuhusiana na kuendesha magari, kuogelea au kutembea kwenye maji yanayotiririka kwa kasi, “Mvua kubwa na upepo mkali huenda vikasababisha visa vya dhoruba Pwani, hivyo wavuvi na wote wanaofanya kazi katika sekta ya majini wanafaa kutahadhari,” ilisema ripoti hiyo.

Idara hiyo pia ilitabiri kuwa katika sehemu kadhaa za Magharibi, Kati, Bonde la Ufa na Kati zitapata mvua ya wastani mwezi huu wa Mei.

Katika upande wa kaskazini mwa Bonde la Ufa, kusini-mashariki, kaskazini-mashariki na eneo la Pwani patatokea mvua ya wastani au ya chini kuliko ilivyo kawaida mwezi wa Mei.

Mvua ya masika mwaka huu ilianza ikiwa imechelewa, hali iliyosababishwa na Kimbunga Idai kilichosababisha maafa nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe kulingana na ripoti ya KMD.

Lakini kimbunga kingine hivi majuzi- Kenneth, kilichoshuhudiwa Tanzania kilisababisha baadhi ya maeneo nchini kunyesha mvua mwishoni mwa Aprili, ilisema KMD awali.

Isipokuwa katikati mwa Bonde la Ufa (Nakuru, Nyahururu) na ukanda wa Pwani ambako mvua inatarajiwa kuisha Juni, msimu wa mvua ya masika unatarajiwa kukamilika wiki ya pili au ya tatu ya Mei katika maeneo mengi ikiwemo Wajir, Garissa, Mandera, Kitui, Machakos, Makueni, Narok, Kajiado na Magadi.

You can share this post!

NASAHA: Ni nini hekima ya Waislamu kulazimika kufunga...

Venezuela yasema iko tayari kukabili Amerika kivita

adminleo