• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
TNA wamkana mwasisi Moses Kuria

TNA wamkana mwasisi Moses Kuria

Na LEONARD ONYANGO

CHAMA kipya cha Transformation National Alliance Party (TNAP) sasa kimejitenga na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria.

Mwenyekiti wa TNAP, Ken Wachira Jumatatu alisema kuwa Bw Kuria si kiongozi wa chama hicho.

“Chama cha TNAP kilibuniwa kwa lengo la kusaidia Wakenya kujiinua kiuchumi hivyo wananchi ndio viongozi wa chama,” akasema Bw Wachira alipokuwa akihutubia wanahabari jijini Nairobi baada ya kuwasilisha nakala za nembo, rangi n katiba ya chama hicho kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Ann Nderitu.

Kulingana na orodha aliyokabidhiwa Bi Nderitu, viongozi wa chama hicho ni Wachira ambaye ni mwenyekiti wa kitaifa, Dkt Cyrus Njiru (mwenyekiti wa operesheni na mipango), Bw Yassir Noor (mwenyekiti wa sera), Bw Arnold Maliba (Katibu), Bw George Thuku (Mwekahazina) na Bi Agness Ibara ni Katibu Mtendaji.

Lakini wadadisi wa kisiasa wanasema kuwa huenda Bw Kuria ambaye tayari ametangaza kuwania urais 2022, huenda anahofia kutimuliwa na Jubilee kwa kujihusisha na chama kingine.

Sheria ya vyama vya kisiasa, mwanachama anaweza kutimuliwa endapo atatangaza kuunga mkono vyama pinzani.

Maafisa wa TNAP pia wamejitenga na TangaTanga na Kieleweke, makundi yaliyochipuka ndani ya Jubilee ambapo moja linapinga na jingine linaunga mkono Naibu wa Rais William Ruto kuwania urais 2022.

Jina la chama cha TNAP ambacho kaulimbiu yake ni ‘’Pesa Na Kazi”, liliidhinishwa mwezi uliopita na Msajili wa Vyama vya Kisiasa Bi Nderitu.

TNAP inachukuliwa kuwa chama kipya kitakachotumiwa na wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya kuwania nyadhifa 2022.

Wanaounga mkono chama hicho wanadai kuwa tayari chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta kimesambaratika.

Viongozi wa Mlima Kenya wakiongozwa na Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata, wabunge Peter Kimari (Mathioya) Ndindi Nyoro (Kiharu) na Kimani Ichungwa (Kikuyu), Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru na mwenzake wa Nyeri Mutahi Kahiga wamepuuzilia mbali chama hicho.

You can share this post!

Kirui, Kiplagat kuongoza timu ya Kenya kwa Riadha za Dunia

Si Waititu pekee, bajeti za Ngilu na Oparanya pia zina utata

adminleo