• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Wafanyabiashara Thika walia kuhangaishwa

Wafanyabiashara Thika walia kuhangaishwa

Na LAWRENCE ONGARO

WAFANYABIASHARA mjini Thika wamelazimika kusitisha biashara zao kwa saa tatu ili kuwasilisha matakwa yao kwa afisi kuu ya gavana.

Walifanya maandamano ya amani wakizunguka mji wote wa Thika na baadaye kumalizia nje ya afisi kuu ya gavana mjini Thika.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wao Bw Alfred Wanyoike, wafanyabiashara hao walikuwa na orodha ya malalamishi yao waliyotaka kuwasilisha kwa gavana Bw Ferdinand Waititu.

Baadhi ya malilio waliyowasilisha ni kwamba askari wa kaunti walioajiriwa walikuwa kila mara wakiwahangaisha kwa kuwatoza ada isiyoeleweka.

Walizidi kuteta kuna rundo la taka linaloshuhudiwa sehemu nyingi na halitolewi na wafanyakazi wa kaunti.

Walidai  ada za kuegesha magari ilikuwa Sh60, lakini ilipandishwa hadi Sh100, jambo walilodai ni dhuluma kwao.

Wafanyabiashara hao walizidi kuteta ya kwamba wachuuzi wengi ambao hufurika mjini Thika majira ya jioni hutoka jijini Nairobi na wakati mwingi wao huchukua maeneo ya wachuuzi kamili wa Thika.

“Mimi kama mwenyekiti wenu nitahakikisha nimewasilisha matakwa yenu kwa gavana wenu Waititu ili aelewe ukweli wa mambo. Sisi hatupo hapa kupiga siasa yoyote lakini ukweli ni kwamba tunataka ukweli ueleweke,” alisema Bw Wanyoike.

Karani wa mbunge wa Thika, ambaye pia ni mfanyabiashara Bw John Mwangi alisema ni vyema Kaunti ya Kiambu iheshimu matakwa ya wafanyabiashara kwani wanalipa ushuru kwa njia inayostahili bila kuchelewa.

“Kile tunachosema ni kwamba tutendewe haki na hakuna mtu yeyote anayetaka kuleta siasa kwa wakati huu. Tukitendewa haki yetu hatutakuwa na shida na kaunti,” alisema Bw Mwangi.

Alisema wakazi wa Thika wanataka kuvutiwa umeme katika mji wote wa Thika ili waweze kuendesha biashara zao kwa masaa 24.

Alisema kaunti ya Kiambu inastahili kurekebisha mambo mengi ili wananchi wapate huduma bora.

Afisa msimamizi wa Kaunti ndogo ya Thika, Bw Christopher Wanjau alipokea mapendekezo yote yaliyowasilishwa na wafanyi biashara hao huku akiahidi kurekebisha baadhi ya malalamishi hayo.

“Kaunti ya Kiambu itakuwa mstari wa mbele kuona ya kwamba inashirikiana na kila mmoja ili kazi ifanyike kwa njia ya uwazi. Tutahakikisha hakuna anayenyanyaswa ,” alisema Bw Wanjau.

Bw Zablon Omollo ambaye ni mfanyabiashara alitaka barabara zilizoko mjini zifanyiwe ukarabati.

“Sisi hatuna ubaya na mtu yeyote bali tunataka tufanyiwe haki ili tuweze kujiendeleza kibiashara,” alisema Bw Omollo.

You can share this post!

Wanga, Kasumba sako kwa bako vita vya kuibuka mfungaji bora...

ANNE CHESEREM: Uvimbe huu uliolemea madaktari umefanya...

adminleo