• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Je, Ruto anajaribu ‘kumhonga’ Mungu?

Je, Ruto anajaribu ‘kumhonga’ Mungu?

Na MWANDISHI WETU

KUJITOLEA kwa Naibu Rais William Ruto kutumia makanisa kama mbinu ya kuingia Ikulu kunaonekana kuzidi viwango ikizingatiwa jinsi amekuwa akizuru maabadi. 

Licha ya kukejeliwa kuhusu hali yake ya kuchanga mamilioni kufadhili miradi ya makanisa, Naibu Rais hajaonekana kutishika kuhusu azimio lake la kuyatwaa upande wake, kila siku akinadi mbinu mpya ya kuyafurahisha.

Jumanne, Dkt Ruto alichapisha picha kadhaa katika akaunti zake za mitandao yake ya kijamii, akiwa katika kanisa la African Divine, ambalo lilikuwa likizindua shirika la hazina ya pesa, African Divine Church Sacco, mtaa wa Karen, Nairobi.

Katika picha hizo, Naibu Rais pamoja na kikundi cha watu wengine wamevalia kofia za kikanisa, huku wageni na wakuu wa kanisa wakiketi katika madhehebu.

Waumini wa kanisa la ADC walipotangamana na Dkt Ruto mtaani Karen, Nairobi. Picha/ Hisani

“Wakati wa kuzinduliwa kwa shirika la hazina na pesa la Kanisa la African Divine Karen, Kaunti ya Nairobi,” Dkt Ruto akasema kwenye maelezo ya picha hizo.

Lakini picha alizochapisha ndizo zinamwacha msomaji na taswira ya jinsi kiongozi huyo ameamua kutumia dini kama gari litakalomsaidia kufika ikulu, ikiwa si mara ya kwanza.

Mara kadhaa siku za mbeleni, Dkt Ruto amepigwa picha akivalia kanzu na mavazi mengine ya Kiislamu, akipiga magoti kuombewa kanisani, akiimba na hata kuhubiri.

Msururu wa mambo haya sasa unathibitisha kuwa Dkt Ruto amejitolea kikamilifu akiamini kuwa ‘treni la dini’ lina umuhimu mkubwa katika safari yake ya kuelekea Ikulu, kando na nadharia ya ‘uhasla’.

Mwenendo huu unawaacha Wakenya wengi na swali moja – Je, Naibu Rais anajaribu kumhonga Mola?

You can share this post!

Kitambue kikosi cha Twomoc FC

Vifo kutokana na ajali vyaongezeka

adminleo