• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:55 AM
NGILA: Tusikubali kutekwa na wajuzi ‘majambazi’ wa mitandao

NGILA: Tusikubali kutekwa na wajuzi ‘majambazi’ wa mitandao

Na FAUSTINE NGILA

AKILI zetu za leo zinaonekana kulemewa kushughulikia jambo moja, kwani zinaruka kutoka shughuli moja hadi nyingine kwa muda mfupi.

Watu wengi waliohojiwa katika utafiti wa hivi majuzi nchini Uingereza walikiri kupata ajali ndogo ndogo huku macho yakiwa yamekwama kwenye simu zao na kusahau kuna visiki njiani.

Mitandao ya kijamii, matangazo katika intaneti, YouTube na programu za simu ni kati ya teknolojia ‘zinazoiba’ wakati wetu, huku kampuni husika ziking’amua mbinu za kurina hela kutokana na akili za wanadamu kunaswa na teknolojia.

Cha kustaajabisha ni kuwa wengi wetu hawajui kwamba jambo hili inafanyika kila siku. Yaani wanadamu wametekwa na uraibu wa teknolojia mpaka wakajisahau wenyewe.

Akili zao zimekuwa kama roboti. Muulize tu mtu jambo fulani asilolijua, badala ya kutumia akili zake kufikiria na kukupa jibu, atakimbia kwenye Google kusaka jibu. Hatuwezi kufikiria tena.

Mwenendo huu umewaingia wanadamu hadi kwenye afisi za ajira.

Katika mikutano mingi ya kikazi, utawaona baadhi ya wafanyakazi wakirambaza kwenye WhatsApp, Facebook, Twitter, Instagram huku wengine wakitazama video ibuka kwenye YouTube. Hawataki kupitwa na jambo.

Ingawa teknolojia ina manufaa tumbi nzima, pia kuna madhara yake.

Kutumia asilimia 40 ya wakati wako kazini ukijiburudisha kwenye intaneti hatimaye kutakuwa na athari mbaya katika utendakazi wako kwa jumla.

Dhamira ya kampuni za teknolojia ni kuwaletea wateja wake trafiki ya tovuti kwa kuongeza idadi ya wasomaji kwenye bidhaa zao mbalimbali, na hii ‘huiba’ dakika au saa kadhaa za kazi ya watu.

Kampuni hizi ni majambazi wa mitandaoni wanaotumia mbinu hasi kutulazimisha kusoma au kutazama matini ambazo hutushawishi kuacha tunachofanya.

Muda na wasaa ni nguzo muhimu katika maisha ya kila mja, na iwapo tutauachia kampuni hizi kunufaika, basi itakuwa sawa na kuishi tukizisaidia kutimiza maslahi yazo huku maendeleo yetu yakikwama.

Ikiwa tutaendelea kuwa na uhusiano huu wa karibu na simu zetu kusaka picha, vibonzo au video zitakazotuongoa au kutufurahisha, basi tutapoteza saa nyingi kila siku, kila wiki na kila mwaka wa maisha yetu kwa vitu ambavyo hatimaye tutagundua havitusaidii.

Kwa kuwa hatutarajii serikali kuweka sera au sheria za kudhibiti tunavyotumia wasaa wetu, tunafaa kujiepusha na ‘vurugu’ hizi za teknolojia kwa kuzitengea muda wake, hasa baada ya kazi.

Tunafaa kuzima tovuti inayotutumia jumbe kuhusu habari tunazofaa kusoma, au tunachopaswa kufanya. Aidha, tuwaheshimu wengine wanaohutubu wakati wa mikutano muhimu.

Kumbuka kwamba wewe una malengo yako ya kufanya maamuzi muhimu, lakini nyuma ya kila programu ya simu yako, kuna kundi la wataalamu wa teknolojia na wanasaikolojia wanaotumia kila mbinu kuiba wakati wako.

Njia pekee ya kuwazima majambazi hawa wa mitandaoni ni kuwanyima muda wako.

You can share this post!

Tutazidi kuanika washukiwa mitandaoni, DCI yaambia korti

ONYANGO: Idadi kubwa ya vijana waliopo magerezani inashtua...

adminleo