• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
GWIJI WA WIKI: Shisia Wasilwa

GWIJI WA WIKI: Shisia Wasilwa

Na CHRIS ADUNGO

TAALUMA ya uanahabari imemwagiwa maji siku hizi. Wanahabari wengi wanavuruga lugha. Jambo hili hunikera sana. Hakuna umbuji wowote katika nyingi za ripoti na habari tunazosomewa. Taarifa ni chapwa, zikiongozwa na falsafa ya ‘sukuma twende’ au ‘mwaga filamu’.

Kisha kuna suala la taarifa ambazo hazijibu maswali nyeti na kugusia mambo mazito ambayo msikilizaji au mtazamaji anatamani kuangaziwa. Wanahabari hawafanyi utafiti wa kutosha.

Ninawashauri wanahabari chipukizi kuwa na subira. Umbuji na utaalamu katika uandishi huchukua muda mrefu wa kusoma, kutafiti na kuhoji kila kitu unachokiona na unachokisikia.

Leo, watazamaji na wasikilizaji wote wa habari ni werevu. Hivyo, mwanahabari lazima afahamu kuwa kuna njia nyingi za kupata taarifa, si kama zamani. Hivyo, anapopata nafasi ya kutoa maelezo, lazima awe na ufahamu wa kutosha kuhusu jambo hili.

Kisha taaluma hii ni kama moshi. Wala usiingiwe na kiburi, maanake wanazaliwa wanahabari kila siku. Mwisho wa siku, utarejea kwa jamii. Iwapo ulikuwa na kiburi, utashindwa kutangamana vyema na watu. Ndio maana wajuzi wa lugha husema, aliye juu mngojee chini!

Nawahimiza wanahabari wa zamani wasipotee. Bado wanahitajika sana kuwaelekeza chipukizi ipasavyo.

Wanastahili kuhudhuria makongamano mengi ya wanahabari ili kuwashajiisha wanaoibukia kitaaluma na kuwaathiri kwa njia chanya.

Tueleze kwa ufupi kukuhusu

Shisia Wasilwa ni mwanahabari, mwandishi na mcha Mungu. Napenda filosofia. Hupenda kuwauliza marafiki zangu na pia kujiuliza maswali mengi kuhusu maisha. Utasikia nikiwauliza watu, “Nini maisha? Kwa nini tunaishi? Hatima ya mwanadamu ni ipi?” Kuuliza huko hunisaidia kusalia kwenye njia ya uongofu.

Mwisho wa mwanadamu ni kaburini. Lakini awapo hai, husahau sana hatima yake, ndipo utapata anadhulumu na hata kuua almuradi atimize kusudio lake. Pindi mwanadamu atakapogundua hatima yake ni ipi, atajifunza kukinai na siku zote atatenda haki.

Tufafanulie kuhusu maisha yako ya awali

Mimi ni mzaliwa wa Nakuru. Familia yetu ilihamia Eldoret, mama alipopata uhamisho wa kuhudumu katika Hospitali ya Rufaa ya Moi (MTRH). Nilianzia kule masomo ya chekechea, kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Kapsoya walikosomea ndugu zangu.

Hatimaye nilijiunga na Shule ya Upili ya Bro Delany Memorial wakati huo ikiitwa Eldoret Harambee. Nilipofanya mtihani wa KCPE na kufaulu, mwanzoni sikutaka kabisa kujiunga na shule hiyo.

“Vipi nijiunge na shule ndogo ya kutwa ilhali nimefaulu? Iweje na ndugu zangu walisomea shule za bweni?” Niliuliza mamangu (Mungu ailaze roho yake pema penye wema). Jibu alilonipa lilibadilisha mawazo na mtazamo wangu kuhusu maisha.

Alinisaili, “Wamjua Zacchaeus Chesoni?” Nikamjibu, “Ndio, ni Jaji Mkuu wa Kenya.”

Ndipo akaniambia kwamba Chesoni alikuwa akipita kwao akielekea shuleni huku akitembea peku bila viatu miguuni. Chesoni alikuwa Jaji Mkuu wa Kenya wakati huo. Alinifahamisha kuwa haijalishi nitakaposomea, almuradi nina bidii, basi nitafaulu.

Niliondoka shuleni Bro Delany Memorial nikiwa mwanafunzi bora zaidi baada ya kuongoza katika masomo ya Kiingereza, Kiswahili, Historia na Jiografia kwenye mtihani wa KCSE 1998.

Maamuzi ya kusomea Historia na Jiografia ni zao la kushauriana na walimu Navade, Lugado, Yego, Owour na Ongeti niliowafichulia mapema kuhusu azma yangu ya kuwa mwanahabari.

Nitakuwa mchache wa fadhila nisipomtaja Bro Mcarthy – Mwalimu Mkuu mzaliwa wa Ireland aliyeniruhusu kusoma licha ya kukosa karo. Alijitolea kuwaelimisha watoto werevu waliotokea katika familia masikini. (Mola airehemu roho yake pema penye wema).

Nilijiunga baadaye na Taasisi ya Mawasiliano ya Kenya (KIMC) kusomea uanahabari.

Nani aliyekuchochea zaidi kukipenda Kiswahili?

Mamangu alikuwa mhubiri. Alinishika mkono kila alipohudhuria makongamano. Alikuwa msemaji mzuri wa Kiswahili na akanichochea pakubwa kupenda lugha.

Ilhamu zaidi ilichangiwa na Bi Mwaura aliyenifundisha katika shule ya msingi. Bi Mercy Juma, Bi Ongeti, Mwalimu Njenga na marehemu Javan Navade (Mola airehemu roho yake pema penye wema) walinipokeza malezi bora zaidi ya kiakademia.

Walinielekeza ipasavyo, wakanihimiza kujitahidi masomoni na kupanda ndani yangu mbegu zilizootesha mapenzi ya dhati kwa Kiswahili.

Aliyegundua kipaji changu cha uanahabari ni mwalimu Omolo Oricho. Zaidi ya kukuza kipawa changu cha ulumbi, alinihimiza mara kwa mara kushiriki mashindano ya utunzi wa mashairi. Ubunifu wangu ulinipandisha kwenye majukwaa mengi ya tuzo za haiba kubwa katika Mkoa wa Bonde la Ufa.

Mbali na kuwa mwanasoka, nilikuwa pia Spika wa Chama cha Mijadala shuleni. Mambo hayo yalinisaidia kuwa jasiri zaidi kila nilipopanda jukwaani.

Nikiwa KIMC, nilianzisha Chama Cha Kiswahili mnamo 2000. Nilipenda kuwasikiliza marehemu Daniel Njuguna Gatei wa Kitengo cha Habari cha Rais, Ramadhan Ali wa Deutsche Welle (DW), marehemu Zeyena Seif wa BBC, Khadija Ali, Willy Mwangi na Khamisi Themor wa KBC. Hawa ni miongoni mwa watangazaji walioamsha ari yangu ya kupenda uanahabari.

Upi mchango wako katika makuzi ya Kiswahili kitaaluma?

Bali na kuwa mwasisi wa Chama cha Kiswahili KIMC, nimeandika riwaya ‘Dunia Tambara Bovu’ iliyoidhinishwa na Taasisi ya Ukuzaji Mitaala (KICD) kusomwa na wanafunzi katika Kidato cha Pili humu nchini. ‘Makovu ya Uhai’ ni riwaya niliyowasilisha kwa minajili ya mashindano ya Fasihi ya Afrika ya Mabati Cornell mnamo 2018. Kwa sasa nasubiri kuchapishiwa riwaya ‘Kinamasi cha Usaliti’.

Bali na kutafsiri sehemu ya Katiba ya Kenya, nilihariri kazi yake Prof Ken Walibora ‘Ndoto ya Almasi’ miongoni mwa kazi nyingi ambazo nimezishughulikia. Katika uanahabari, nimekuwa mhariri wa siku nyingi, nikitegemewa sana kulainisha taarifa na kupiga msasa lugha ya Kiswahili.

Nimetoa mihadhara mingi kuhusu makuzi ya Kiswahili kwenye makongamano, shule za upili, taasisi na vyuo vikuu mbalimbali vya humu nchini. Nimewachochea wanafunzi si haba kusomea uanahabari na kwa sasa hawajutii maamuzi hayo. Ni wengi mno, siwezi kuwataja hapa. Tayari nimealikwa nchini Tanzania mwezi ujao kuhudhuria Kongamano la Kimataifa la Wanahabari.

Una maazimio gani ya baadaye maishani na kitaaluma?

Naazimia kufungua kituo changu cha Radio na kuwa mkulima msifika. Natarajia kuanza ufugaji wa mifugo mbalimbali na kushiriki kilimo cha mboga na matunda.

Ni kipi cha pekee unachokifanya tofauti na wenzako kitaaluma?

Sidhani kama kunacho, maanake hakuna kitu kipya chini ya jua. Lakini kile wengi hawakijui ni kwamba mimi ni mkalimani mahali ambapo huwa nahudhuria ibada.

Umewahi kutambuliwa na kutuzwa kutokana na mapenzi au mchango wako kwa Kiswahili?

Naam. Mnamo 2011, Kituo cha WASTA cha Guru Ustadh Wallah Bin Wallah kilinitambua kwa upekee wa mchango wangu katika tasnia hii ya uanahabari. Namhongera sana Guru Ustadh kwa kuwa ndiye wa pekee miongoni mwa wasomi wa Kiswahili kutoka humu nchini anayewatia ari wapenzi wa Kiswahili kwa kuwatambua na kuwatuza wangali hai.

Mbali na kazi uifanyayo kwa sasa, unajishughulisha na nini kinginecho?

Nahubiri injili na kujishughulisha na kilimo.

Unajivunia nini kikubwa katika taaluma yako?

Ninajivunia kuwahi kufanya kazi katika televisheni, radio na kwenye vyombo vya machapisho. Nimefanya kazi KBC, Citizen Tv, China Radio Kimataifa, BBC na DW. Nimetimiza ndoto zangu za tangu udogoni. Niliwahi kuwaambia marehemu mamangu na babangu kuwa ipo siku nitasikika nikisoma taarifa kwenye vyombo vya habari vya humu nchini na vya kimataifa.

Siku zote nitakumbuka kipindi ‘Ninapobanwa’ nilichokiendesha kwa muda mfupi baada ya Waweru Mburu aliyefahamika sana kwa kipindi ‘Yaliyotendeka’ kulazwa hospitalini na hatimaye kuaga dunia. (Mola ailaze roho yake pema wenye wema).

Kwa muda huu mfupi, nilianza kupokea simu za kunitishia maisha kwa kuwa ‘Ninapobanwa’ ililenga kutumbua majipu na kubainisha uozo katika jamii. Nusura niuawe ama kutoweka jinsi wanahabari wengine wametoweka wasipatikane tena katika sehemu mbalimbali duniani humu.

Zaidi ya kuandika matopa ya vitabu, utangazaji umeniwezesha kuzuru mataifa yote ya Afrika Mashariki, Tunisia, Misri, Uturuki na Ujerumani.

You can share this post!

ONYANGO: Idadi kubwa ya vijana waliopo magerezani inashtua...

KAULI YA WALIBORA: Lugha kwenye vyombo vya usafiri...

adminleo