• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
SHANGAZI AKUJIBU: Adai kunipenda lakini naogopa mkewe ananiwinda

SHANGAZI AKUJIBU: Adai kunipenda lakini naogopa mkewe ananiwinda

Na SHANGAZI

SHANGAZI nakuomba unishauri kuhusu jambo linalonitatiza. Nimekuwa kwenye uhusiano na mwanamume ambaye ana mke. Nina mtoto ingawa bado ninasoma, huu ndiyo mwaka wangu wa mwisho katika shule ya upili. Mwanamume huyo amekuwa akinisaidia kwa karo na pia kugharamia mahitaji ya mtoto wangu. Kwa bahati mbaya, mke wake aligundua uhusiano wetu mwaka jana. Alianza kuniwinda na nikaamua kuachana na mumewe. Kwa upande wake mwanamume huyo anataka tuendelee na urafiki ili aendelee kunisaidia. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mbali na mapenzi, ninajua pia umekuwa katika uhusiano huo kwa sababu ya msaada ambao umekuwa ukipata kutoka kwa mwanamume huyo. Ninapinga uhusiano wa aina hiyo kwa sababu ni haramu. Kuendeleza uhusiano huo ni kuhatarisha maisha yako kwani unasema kuwa mkewe anakuwinda. Kama ni lazima uwe na mpenzi, ni heri utafute wako mwenyewe.

Nimemvumilia kwa miaka miwili sasa lakini tabia ni ile ile

Mambo shangazi? Nina umri wa miaka 20 na nimekuwa na uhusiano na kijana fulani kwa miaka miwili sasa. Lakini uhusiano huo umeanza kunishinda kwa sababu tumekuwa tukikosana mara kwa mara bila sababu za maana. Nimemvumilia nikidhani kuwa atajirekebisha lakini sijaona mabadiliko na nimeamua kumuacha. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Unasema kuwa umefanya uamuzi wako huo kwa sababu huoni dalili za mpenzi wako kujirekebisha. Ninaamini pia anajua unavyohisi kuhusu tabia yake hiyo. Mapenzi yanahitaji maelewano kati ya wahusika la sivyo hayawezi kudumu. Kama umeamua kumuacha, hiyo ni haki yako na hakuna anachoweza kufanya ila kujilaumu mwenyewe.

 

Shangazi, nivumilie kwa muda gani kubaini penzi la dhati?

Vipi shangazi? Umewahi kusema katika ukumbi huu kuwa mapenzi ya dhati huanza kwa urafiki, uhusiano na hatimaye ndoa kwa wanaovumilia. Je, mtu anafaa kuvumilia kwa muda gani katika harakati za kutafuta mapenzi ya dhati?

Kupitia SMS

Mapenzi ya dhati hutegemea wahusika wala hakuna muda maalumu wa kusubiri ili kuyatambua. Unaweza kugundua kuwa mpenzi wako anakupenda kwa dhati miezi michache baada ya kujuana na pia inaweza kuchukua miaka kadhaa. Wapenzi wanapofikia kiwango cha kufunga ndoa huwa wamefikia kilele cha mapenzi yao na bila shaka hatua hiyo ni thibitisho la mapenzi ya dhati.

 

Mie maskini nimepata mchumba tajiri, sijui wazazi watanipokea?

Kwako shangazi. Nimependana na msichana tunayefanya kazi pamoja na tumefikia hatua ya kuanza maisha pamoja. Tatizo ni kwamba anatoka familia iliyo na uwezo mkubwa kifedha na nahofia wazazi wake wataniwekea vikwazo kwa sababu ninatoka familia maskini. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Nimesema mara nyingi hapa kuwa mapenzi ya dhati hayajui tajiri wala maskini. Kuna usemi kuwa mapenzi ni sawa tu na majani, yanaweza kuota popote pale. Iwapo msichana mwenyewe amekupenda na ameamua kuwa utakuwa mwenzake maishani, wazazi wake hawafai kuwa kizuizi kwa sasa yeye ni mtu mzima sasa na ana haki ya kujichachagulia mpenzi.

 

Raha najipa mie mwenyewe, nitawahi kuwa na hamu ya kupata mpenzi?

Shangazi nina tatizo na naomba unisaidie. Nina umri wa miaka 28 na sijawahi kuwa na uhusiano na mwanamume. Nimezoea kujishughulikia mwenyewe kila nikihisi haja. Hofu yangu ni kuwa mazoea hayo yatanifanya nisione haja ya kuwa na mpenzi. Nishauri.

Kupitia SMS

Mtu wa umri wako anafaa kuwa na mpenzi ingawa si lazima kwani kila jambo lina wakati wake. Ukweli ni kuwa mazoea yako hayo yametokana na hali kwamba huna mpenzi. Pili, mazoea hayo hayawezi kukuzuia kuwa na mpenzi bora tu uwe na nia.

You can share this post!

Matumaini tele kikosi cha riadha kitanogesha Japan

BONGO LA BIASHARA: Alistaafu ualimu ila mipapai inampa...

adminleo