• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
BONGO LA BIASHARA: Alistaafu ualimu ila mipapai inampa ‘malipo’ kuliko ajira

BONGO LA BIASHARA: Alistaafu ualimu ila mipapai inampa ‘malipo’ kuliko ajira

Na BENSON MATHEKA na JOHN MUSYOKI

ALIPOANZA kilimo cha mapapai akiwa mwalimu, watu wengi walidhani hangefaulu kwa sababu ya hali ya hewa katika eneo kame la Masinga, Kaunti ya Machakos.

Na baada ya kustaafu mwaka wa 2016, wengi walidhani Bi Eunice Muthini Kimuya hangetoboa kuendeleza kilimo cha papai aina ya SP.
Walikuwa wamekosea kwani aliendelea na akaanza kupanda aina tofauti za mboga.

Mkulima huyu anasema mwanzoni dhamira ya kujihusisha na kilimo ilikuwa kuimarisha afya yake hasa uzeeni kwa kupata matunda na mboga za kutosha kwa matumizi yake ya nyumbani.

Miaka mitatu baadaye, amekuwa mkulima wa kutajika katika kijiji cha Kaewa eneobunge la Masinga.

“Nilipoanzisha kilimo cha mapapai, kwanza watu walisema sitatoboa kwa sababu mimi ni mwanamke na singeweza kufanikisha ukulima huu kama watu wengine kwa sababu umri wangu ulikuwa umesonga lakini madhumuni yangu yalikuwa ni kupata matunda ya kula tu ili niwe na afya bora,” anasema Bi Muthini.

Baadaye aligundua kilimo cha papai kinaweza kumletea mapato pia. Hii ni baada ya kupata mavuno mengi mara ya kwanza. Kwa kuwa hakuwa na mimea mingi, alipata miche zaidi kutoka kwa kampuni ya Meru Greens na kuipanda katika shamba lake la ekari tatu.

“Mara ya kwanza nilipata mavuno mengi ya mapapai katika shamba la ekari moja. Niliamua kuongeza mimea shambani kwa sababu mbali na kupata matunda kwa matumizi ya nyumbani pia ilikuwa ni biashara inayoleta faida,” aeleza Bi Muthini.

Faida aliyopata mara ya kwanza ilikuwa Sh40,000 baada ya kuvuna mapapai katika shamba la ekari moja.

Anasema kuna sababu ya kukuza mapapai aina ya SP.

“Mapapai aina ya SP huchukua muda mfupi kukua, kati ya miezi saba na tisa kabla ya kuanza kupata mavuno na huzaa kwa wingi. Pia kwa sasa nimegundua kwamba ukiuza mapapai utapata pesa za kugharamia mahitaji mengine ya nyumbani,” aeleza Bi Muthini.

Mavuno anayopata kwa mwaka mmoja kutokana na mapapai yanampa faida ya Sh480,000.

Bi Eunice Muthini Kimuya anayeendeleza kilimo cha papai aina ya SP katika eneo la Masinga, Kaunti ya Machakos. Picha/ Benson Matheka

Anaeleza kwamba tangu alipogundua umuhimu wa kukuza mapapai alitafuta wataalam wanaompa ushauri wa kufanikisha kilimo hiki.

“Kwa sasa nimegundua kilimo cha mapapai kina faida tele kuliko nilivyodhania. Mimi sijabobea sana lakini niliwatafuta wataalam wa kunipa ushauri na nimefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana. Mapapai aina ya SP huwa na soko sana na hununuliwa kwa wingi,” aeleza.

Ili kuimarisha kilimo cha mapapai Bi Muthini anaeleza kwamba kuna utaratibu unaofaa kufuatwa.

Kwa watu wengi huenda wakakata tamaa kuendeleza kilimo cha mapapai kwa kukosa shamba lakini Bi Muthini anaeleza kwamba mtu anaweza kukodisha shamba na ahakikishe mchanga una udongo mzuri.

“Mimea ya mipapai huwa hahiitaji maji mengi. Mipapai inahitaji kunyunyuziwa maji kwa njia ya utaratibu kwa sababu maji mengi husababisha mimea kunyauka. Mtu anaweza kuongeza mbolea kidogo ili mimea izae na kuwa na matunda mengi,” aeleza Bi Muthini.

Mifugo wala mapapai

Mbali na kuwa mapapai ni chakula cha binadamu, Bi Muthini anaeleza kwamba mapapai ni chakula cha mifugo kama vile nguruwe, batamzinga na kuku. Pia mapapai hutengeneza sharubati.

Hata hivyo, anasema kuna changamoto zinazokuba ukulima wa mapapai.

“Kuna changamoto chungu nzima katika kukuza mimea ya mipapai kama kutokuwa na mbinu nzuri za kuhifadhi matunda, matunda kuoza haraka na ndege kuvamia matunda yakiwa shambani,” aeleza Bi Muthini.

Kwa sasa Bi Muthini ameanza kulima sukuma wiki na spinaji kwenye mahema.

“Sukuma wiki na spinachi huwa zinahitajika kila siku na nimepiga hatua kuhakikisha nimekuza mboga safi na isiyokuwa na kemikali kwa matumizi ya hapa nyumbani na kuuza,” asema Bi Muthini.

Anasema mboga anayopanda kwenye vifungulio huwa inaleta faida pia. Gunia moja huwa anauza Sh15,000 na huvuna magunia mawili kila wiki na kuwa na zaidi ya sh 60,000 kila mwezi kutoka kwa mauzo ya mboga.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Adai kunipenda lakini naogopa mkewe...

KILIMO NA BIASHARA: Mradi eneo kame umewapa wakazi riziki

adminleo