• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
KILIMO MASHINANI: Tunda hili la jamii ya nyanya lina faida tele, litakupa laki kila mwezi

KILIMO MASHINANI: Tunda hili la jamii ya nyanya lina faida tele, litakupa laki kila mwezi

Na DUNCAN MWERE

HUKU idadi kubwa ya vijana wakihamia mijini kusaka ajira za hadhi, mambo ni tofauti kwa Michael Mwangi Mumbi.

Anaamini kwa dhati kuwa ukosapo kupata fedha kijijini usitarajie kufanikiwa mjini hasa kutokana na changamoto na pandashuka zinazotokana na gharama kubwa ya maisha siku hizi.

Mwangi aliyezaliwa miongo mitatu iliyopita ni kati ya mabarobaro wachache waliovalia njuga suala la kilimo na kuzidi kufanikiwa maishani.
Shamba lake limejaa matunda ya jamii ya nyanya (tunda-nyanya) au tree-tomato kwa lugha ya Kimombo.

Kilimo hiki kinatekelezwa kitaalamu katika shamba lake lililo eneo la Shauri Moyo kijijini Gikumbo eneobunge la Mathira, Gatuzi la Nyeri.

Mwangi anafahamisha Akilimali kuwa alikuwa na matumaini makuu ya kupata kazi ya hadhi na donge nono ila aliambulia patupu.

“Baada ya kuhitimu masomo yangu nilizuru kotekote hususan miji mikuu kutafuta kibarua chenye pato la haja ila sikufanikiwa,” aeleza.

Ni kutokana na sababu hii aliporejea kijijini na kuanza kilimo cha matunda aina ya nyanya na karakara.

Katika sehemu kubwa ya shamba lake amepanda matunda-nyanya na anaeleza kuwa kilimo hiki kinamzolea ngwenje maridhawa.

“Soko la bidhaa hii liko wazi kila wakati na mkulima hutia pesa nyingi mfukoni japo ni lazima awe na subira,” anadokeza.

Katika ekari moja, amepanda zaidi ya miti 1,800 ambayo anaungama fedha ambazo hutia kibindoni ni nyingi kuliko za wale walioajiriwa katika sekta nyingi nchini.

Cha msingi kumaizi katika zaraa aina hii ni kuwa mkulima anafaa kufuata utaratibu ufaao ili kuhakikisha anapata mavuno nomi na tunda-bora hususan kwa mtumizi.

Maji, mbolea na dawa ni nguzo muhimu zaidi. Hatua ya kwanza ni kuandaa shamba kikamilifu na kuhakikisha ameondoa magugu na maotea ya aina yoyote.

Pili mkulima analazimika kuchimba shimo lenye urefu wa futi mbili unusu hadi tatu kisha atenganishe kwa urefu mita tatu kwa tatu. Baada ya kuchimba shimo mkulima anashauriwa kuweka mbolea ya ng’ombe au mbuzi.

Katika shimo hilo, aweke maji kisha achanganye na fatalaiza aina ya DAP.

Mkulima anahimizwa kuchanganya mchanga uliochimbwa na mbolea. Hatua itakayofuatia ni kuweka maji baada ya kupanda. Mwangi anasisitiza maji ni muhimu katika mmea huu.

“Ili kuwa na mazao bora, mkulima anafaa kuyanyunyuzia maji kila mara kwani mmea unaweza kunyauka na kukaribisha magonjwa mbalimbali,” aeleza gwiji huyu anayeshirikiana na mkewe Lydia Wamuyu.

Baada ya mmea kukomaa mkulima aweke fatalaiza aina ya 17. Wiki kadhaa baadaye ni jambo aula kunyunyuzia dawa ya baridi ili kuangamiza viwavi aina ya Cutworm ambavyo ni kati ya vikwazo vikuu katika zaraa hii.

Kwa muda wa kati ya miezi minane na mwaka mmoja, mkulima anaweza kufurahia kazi ya jasho lake. Hata hivyo, hili hutegemea na namna anavyotunza mmea wake.

Mwangi anaambia Akilimali kuwa tunda lenyewe linafaa kuvunwa kati ya juma moja au majuma mawili.

“Baada ya kuvuna tunda la kwanza mimi huwa nachuma baada ya wiki mbili japo kuna wale hufanya hivi baada ya juma moja,” anaeleza.

Miaka saba

Faida kubwa ni kwamba mkulima atakuwa akivuna matunda kwa muda wa miaka saba mradi atunze hasa kwa kupalilia, kuweka maji na mbolea mara kwa mara.

Kwa mujibu wa matabibu wa mimea, tunda-nyanya ni kati ya matunda yanayofaa kuliwa kwani yana uwezo mkuu wa kuponya magonjwa mengi.

Kuhusu changamoto, Mwangi anasema kuwa mmea huu hukabiliwa na matatizo mengi lakini mkulima anafaa kuhudhuria makongamano ya kilimo ili kupata mbinu na suluhisho la kudumu.

“Kutangamana na wataalamu nyanjani hasa kituo cha kutoa mafunzo cha Wambugu Farm kila mara kutawezesha mkulima kupata maarifa ya kutosha,” anashauri.

Kuhusu soko, Mwangi anafichua kuwa wateja ni wengi, na kwake soko lake liko jijini Nairobi.

Kilo moja ya matunda haya hugharimu Sh100. Baada ya majuma mawili huvuna kilo 500.

Hii ina maana Mwangi hutia kibindoni Sh50,000 huku kwa mwezi mmoja akipokea Sh 100,000.

Jambo muhimu kung’amua hapa ni kuwa kilo hizi huongezeka namna mkulima anavyoendelea kuvuna na kutunza.

You can share this post!

Mtunze mbwa akufae zaidi

Chifu kizimbani kwa kuiba mbwa!

adminleo