• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:20 AM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Makosa tufanyayo wakati wa mfungo

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Makosa tufanyayo wakati wa mfungo

Na HAWA ALI

WENGI kati yetu Waislamu tunaofunga hushughulishwa mno na faida zinazopatikana kwa kufunga pamoja na thawabu zake.

Lakini kwa kufanya hivyo mara nyingi tunafanya makosa kiasi ambacho badala ya kupata faida na fadhila tunapata kinyume chake.

Makosa yetu huwa ni yale ambayo yanatufanya tuifanye Ramadhan kuwa ni msimu wa biashara kama ilivyo kwa watu wengine kwenye masiku yanayohusiana na Imani zao.

Hapa tunajaribu kukumbushana na kujikumbusha sisi wenyewe pia juu ya namna ya kufanya ili kukwepa kurudia kuyafanya makosa hayo ya kuifanya Ramadhan kuwa ni msimu wa biashara za kuongeza kipato badala yake kuwa ni msimu wa biashara lakini ya kuchuma thawabu na fadhila kutoka kwa Mola wetu ndani ya Mwezi huu wa Ramadhan.

Kuufanya mwezi wa Ramadhan kuwa ni sherehe ya kidini

Wengi wetu Mwezi wa Ramadhan umepoteza kwetu ile faida yake ya kiroho na badala yake Mwezi wa Ramadhan umekuwa zaidi kwetu ni sherehe ya kidini badala ya kuwa ni sehemu ya Ibada.

Tunafunga kuanzia Asubuhi mpaka Jioni kwa mazoea tu au kwa sababu waliotuzunguka wanafunga na tunasahau kwamba huu ni wakati wa kusafisha nafsi zetu na roho zetu kutokana na maasi na kujiweka mbali na yale yanayomuudhi Mola wetu.

Tunasahau kufanya wingi wa Dua ndani ya mwezi huu pamoja na kumuomba sana Mwenye ezi Mungu msamaha ili atuepushe na Adhabu ya Moto wa Jahannam.

Ni kweli tunakaa mbali na Chakula na Vinywewa lakini ni hivyo tu ndivyo tunavyokaa navyo mbali. Ijapokuwa kuna maneno ya Bwana Mtume s.a.w. amesema; Malaika Jibreel ameniambia Imesuguliwa chini ya vumbi pua ya Mtu ambae Ramadhan imekuja na yeye hayakusamehewa madhambi yake, nami nikasema Ameen.

Kisha akasema tena Imesuguliwa chini pua ya Mtu ambae amepata fursa ya kuishi na wazazi wake (wawili au mmoja) mpaka wakazeeka lakini akakosa kuingia peponi (kwa kushindwa kuwahudumia), nami nikaitikia Ameen.

Kisha akasema tena Imesuguliwa chini pua ya mtu ambae wewe umetajwa mbele yake na kisha hakukuswalia, na nikaitikia tena Ameen.
Tirmidhi, Ahmad.

Kushughulika mno na vyakula pamoja na vinywewa

Kuna watu wengine Ramadhan yote wao wanashughulika na vyakula tu.

Wanatumia muda mwingi kupanga juu ya vyakula, kupika, kununua vitu madukani, na kufikiria sana juu ya vyakula badala ya kushughulika na Swala na kusoma Qur’ani pamoja na mambo mengine ya kujikurubisha kwa Mola wetu.

Fikra zinalalia kwenye vyakula kiasi ambacho wanaugeuza mwezi wa Ramadhan kuwa ni mwezi wa sherehe za vyakula.

Watembelee wakati wa kufuturu utaona milima ya aina kwa aina ya vyakula, wanapoteza msingi na makusudio ya funga ya Ramadhan.

Tunatakiwa kutafuta namna ya kujizuia na ulafi na kamwe haifai kuutumia mwezi huu kuendeleza matamanio ya nafsi zetu kwa kuziwacha nafsi zetu ziendelee kutusukuma kwenye kupapia vyakula.

Anasema Mwenye ezi Mungu ; “Na kuleni na kunyweni na wala msifanye Israfu” (Al aaraf;31)

Kushughulika na kupika tu

Baadhi ya mama zetu na dada zetu wanatumia muda mwingi kupika tu asubuhi na jioni.

Wanazama kwenye hilo la kupika kiasi kwamba hata Swala zinawapita au inapofika wakati wa Swala ya Taraweeh wanakuwa wamechoka sana kiasi kwamba hawezi kuswali Taraweeh lakini wakati mwingine hata Swala ya Isha inawapita kwa uchovu. Wanakuwa wamechoka kiasi kwamba hawawezi kusoma Qur’ani au hata kujishughulisha na Nyiradi.

Huu ni mwezi wa rehma na ni mwezi kuomba Msamaha kwa hiyo inapendeza “Uzime jiko na Uwashe Imani yako!”

Kula sana

Baadhi yetu miongoni mwa makosa tunayoyafanya ni kula sana daku au futari mpaka wanakaribia kupasuka matumbo. Kwa sababu wanadhani kwa kufanya hivyo ndio wanajihakikishia kutoshughulishwa na njaa wakati wa mchana wa Ramadhan. Wengine wanakula sana wakati wa kufuturu kwa namna ambayo utadhani wanalipa kisasi cha mlo uliompita kutokana na kuwa wamefunga.

Kufanya hivi ni kinyume kabisa na mwenendo wa Bwana Mtume s.a.w. Kwani kufanya kitu kwa kiasi ndio ufunguo wa kheri zote. Amesema Bwana Mtume s.a.w.

“Mwanadamu hajapata kujaza kitu cha shari kuliko kujaza tumbo lake, inamtosha Mwanadamu vijitonge ambavyo vitasimamisha mgongo wake (ale kiasi cha kuondoa njaa tu), ikiwa hapana budi basi (na ale) thuluthi kwa ajili ya chakula, na thuluthi kwa ajili ya maji, na awache thuluthi kwa ajili ya hewa. (Tirmidhi na Ibn Maajah.)

Kula sana kunamtia au kunamfanya mtu awe mvivu wa kutekeleza matendo mengi ya kiibada na pia kula sana kunafanya moyo wa mtu upumbae.

Imepokewa kuwa Imam Ahmad amewahi kuulizwa; Je Inawezekana mtu kuwa mnyenyekevu na mpole ndani ya Moyo wake wakati tumbo lake limejaa? Akajibu “Sidhani kama ataweza”.

Kulala Kutwa

Watu wengine miongoni mwetu kwa sababu ya kuwa wamefunga hutumia siku nzima wakiwa wamelala kwa kufanya hivi huona ndio wanailaza funga yao.

Hivi hilo ndilo kusudio la funga aliloliweka Mola wetu kwa kutuletea funga ili tulale wakati wote wa mchana?

Hapana shaka yeyote watu hawa wanakosea ile maana hasa iliyokusudiwa na Mwenyezi Mungu katika kutufaradhishia funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Na kwa maana hiyo tumekuwa watumwa wa kupenda raha na wepesi kwenye kila jambo. Hawawezi kabisa kuwa macho na kukutana na njaa kidogo au kujizuia na matamanio yao.

You can share this post!

KRA yamulika wafanyabiashara wa mitandaoni

SHANGAZI AKUJIBU: Nilitarajia harusi baada ya miaka 3, sasa...

adminleo