• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:38 AM
Bunge laruhusu Rais wa Togo atawale hadi 2030

Bunge laruhusu Rais wa Togo atawale hadi 2030

Na MASHIRIKA

BUNGE la Togo limeidhinisha mageuzi ya Katiba yanayoruhusu Rais Faure Gnassingbe ambaye familia yake imeongoza nchi hiyo tangu 1967, kugombea urais mara mbili zaidi na kubakia mamlakani hadi 2030.

Mageuzi hayo ya Katiba pia yanawapa kinga marais wa zamani.

Mnamo 2005, Gnassingbe alimrithi baba yake Jenerali Gnassingbe Eyadema, ambaye alitwaa mamlaka kupitia mapinduzi ya kijeshi zaidi ya miaka 50 iliyopita na kutawala hadi kifo.

Wabunge wote 90 waliohudhuria kikao Jumatano waliidhinisha mageuzi hayo.

Mbunge mmoja hakuwemo.

Sheria hiyo mpya sasa inaruhusu marais kutawala kwa vipindi viwili lakini pia inamaanisha kwamba Gnassingbe anaweza kugombea urais katika chaguzi mbili zijazo 2020 na 2025.

“Rais wa Jamhuri atachaguliwa kwa kipindi cha miaka mitano na anaweza kugombea kwa miaka mitano zaidi pekee,” inasema sheria hiyo.

Kifungu kingine katika sheria hiyo kinapatia marais wa zamani kinga dhidi ya kushtakiwa, kukamatwa, kuzuiliwa kwa vitendo walivyotekeleza au kutekelezwa wakiwa mamlakani.

Chama cha Gnassingbe kina thuluthi tatu ya idadi ya wabunge lakini hata vyama vingine vinashirikiana na rais. Chama kikuu cha upinzani kilisusia uchaguzi mwaka 2018.

Nchini Togo, mageuzi ya katiba huwa yanakubaliwa yakipitishwa na zaidi ya wabunge 73 au zaidi.

Miaka sita kila kipindi

Wabunge pia walibadilisha sheria zinazowahusu kumaanisha kwamba sasa wanaweza kushikilia viti vyao kwa vipindi viwili vya miaka sita kila kipindi.

Awali, walikuwa wakihudumu kwa kipindi cha miaka mitano bila kuwekewa idadi mihula wanayopaswa kuhudumu.

Upinzani ulipinga mageuzi hayo mwaka jana na kuandamana ukitaka Gnassingbe kujiuzulu. Lakini muungano wa vyama 14 vya upinzani ulikataa kushiriki uchaguzi wa Disemba mwaka jana ukisema hakukuwa na usawa na ukaachia bunge mikononi mwa chama cha Gnassingbe.

Kulingana na Brigitte Adjamagbo-Johnson, ambaye ni mshirikishi wa muungano wa upinzani, walishtushwa na mageuzi hayo.

“Ameonyesha watu wa Togo kwamba kitu cha pekee anachojali ni kubaki mamlakani,” aliambia wanahabari Alhamisi jijini Lome.

Togo, nchi inayopatikana katikati ya Ghana na Benin, imekuwa nchi ya hivi punde barani Afrika kubadilisha katiba kuruhusu Rais kubaki mamlakani.

Katika hatua tofauti, serikali ya Togo Alhamisi ilitangaza kuwa uchaguzi wa mabaraza ya miji utafanyika Juni 30 ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika tangu 1987. Kuna nafasi 1,527 zitakazojazwa. Mameya wa miji huwa wanateuliwa na Rais.

You can share this post!

Waziri akiri serikali ilitoa hati kimakosa

NASAHA ZA RAMADHAN: Chakula cha daku humpa nguvu mfungaji...

adminleo