• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Wanafunzi 2 wafa shuleni katika hali tatanishi

Wanafunzi 2 wafa shuleni katika hali tatanishi

STEPHEN MUNYIRI na VICTOR RABALLA

MWANAFUNZI wa Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Ruthagati iliyo eneo la Mathira Magharibi, Kaunti ya Nyeri, Jumamosi alipatikana amefariki katika hali isiyoeleweka ndani ya bweni.

Kisa hicho kilitokea siku moja tu baada ya kingine katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kisumu, ambako mwanafunzi alifariki Ijumaa asubuhi baada ya kuhudhuria masomo ya ziada alfajiri.

Kwenye kisa cha jana, Naibu Kamishna wa Kaunti anayesimamia Mathira Magharibi, Bw Charles Munari, alisema upelelezi wa mapema ulionyesha mwanafunzi huyo hakujitoa uhai kama ilivyokuwa imeshukiwa awali.

Kulingana naye, marehemu alipatikana na rafiki yake akiwa amelala sakafuni jana asubuhi ndipo akamwita mlinzi ambaye baadaye alifahamisha wasimamizi wa shule.

“Hakuwa amelalamika kuhusu ugonjwa wowote na alikuwa akisoma na wenzake usiku wa kuamkia jana. Bado tunaendelea na uchunguzi ili kubainisha kilichotokea,” akasema.

Mnamo Ijumaa, mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kisumu alifariki baada ya kuugua kwa wiki moja.

Ripoti ya mapema ya polisi ilionyesha kwamba msichana huyo alikuwa akipokea matibabu katika zahanati ya shule.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kisumu, Bw Benson Maweu, alisema msichana huyo aliondoka darasani saa kumi na mbili unusu alfajiri akaenda kwa bweni.

Wanafunzi wenzake waliingiwa na wasiwasi kwani alikaa katika bweni kwa muda mrefu na walipoenda kumtafuta, walikuta amedhoofika na hangeweza kusimama. Alithibitishwa kufariki alipokimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kisumu.

You can share this post!

Miili yazidi kupatikana mitoni jiji la Nairobi likisafishwa

RAMADHAN: Tusiwasahau wasiojiweza katika mwezi huu wa...

adminleo