• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
KILIMO: Mataifa ya COMESA kunufaika na teknolojia ya kuondoa bidhaa feki sokoni

KILIMO: Mataifa ya COMESA kunufaika na teknolojia ya kuondoa bidhaa feki sokoni

NA FAUSTINE NGILA

WAKULIMA katika mataifa yote 19 ya Muungano wa Masoko ya Pamoja kwa Mataifa ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) watanufaika na teknolojia mpya ambayo inalenga kuwazima wafanyabiashara wa mbegu, dawa na fatalaiza feki kupitia mfumo wa kidijitali.

Hii ni baada ya kampuni ya teknolojia ya kutambua bidhaa feki mPedigree kushirikiana na COMESA kuwalinda wakulima katika mataifa hayo.

Hatua hii inaifanya COMESA kuwa muungano wa kwanza wa kibiashara kuzindua mfumo wa kutambua bidhaa feki duniani kwa kutumia teknolojia ya mPedigree ya kuhakikishia wakulima ubora wa bidhaa.

“Mfumo huu utasaidia mataifa haya kuzuia uuzaji wa bidhaa feki za kilimo kama mbegu, fatalaiza na dawa huku pia ukipiga jeki ubora wa kilimo kwani utawapa wakulima mbegu zinazofaa kwa upanzi,” akasema mkurugenzi wa mipango wa mPedigree, Bw Selorm Branttie.

Bw Branttie alikuwa akihutubu katika uzinduzi wa mafunzo kwa kampuni za mbegu ulioongozwa na wataalamu wa COMESA kuhusu uagizaji, matumizi na uuzaji kwa kutumia brandi za mbegu za COMESA jijini Lusaka, Zambia.

Wataalamu katika sekta ya kilimo wapigwa picha ya pamoja wakati wa mafunzo ya siku mbili kuhusu matumizi ya brandi za COMESA kwa bidhaa za kilimo jijini Lusaka, Zambia. Picha/ Hisani

Kupitia teknolojia hii ya kuthibitisha uhalali wa bidhaa, wakulima katika nchi moja wataweza kufuatilia kidijitali zilikotoka bidhaa na ubora wake kwa kutumia simu zao, hata bila muungnisho wa intaneti, na hivyo kuwahakikishia uzalishaji wa visivyo na madhara kwa mwili wa binadamu.

Ushirikiano na COMESA utaiwezesha mPedigree kusambaza teknolojia hii kwa mataifa yote wanachama ambayo yameachwa nyuma kama Ethiopia, Burundi na Eswatini.

“Hii ni mara ya kwanza ambapo vyeti vya mbegu na uthitbitisho wake utafanywa kidijitali na kumwezesha mkulima kufuatilia kampuni iliyotengeneza mbegu hizo na uhalali wake bila bughudha,” akaongeza.

Mbegu feki zimechangia kwa uzalishaji duni kwa wakulima zaidi ya milioni 80 wadogo wadogo na kuzua baa la njaa katika mataifa ya COMESA.

“Kwa kila mfuko wa mbegu au fatalaiza ambao utakuwa na stika ya COMESA, itamaanisha umethibitishwa kuwa halali. COMESA itashirikiana na halmashauri zote za mbegu na bidhaa za kilimo kuhakikisha bidhaa feki zimeondolewa kwa soko la kilimo,” akasema Mkurugenzi wa Viwanda na Kilimo, Bw Thierry Kalonji aliyemwakilisha Naibu Katibu Mkuu wa Mipango Dkt Kipyego Cheluget.

 

You can share this post!

SUDAN: Waandamanaji na jeshi kurejelea majadiliano

Messi aishauri Barca iwauze Coutinho, Rakitic na Umtiti

adminleo