• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
DHAHABU: Mshukiwa mkuu hutangamana na wanasiasa vigogo

DHAHABU: Mshukiwa mkuu hutangamana na wanasiasa vigogo

Na VINCENT ACHUKA

MSHUKIWA mkuu wa sakata ya dhahabu feki ambapo mwanamfalme wa Milki ya Kiarabu (UAE) alitapeliwa zaidi ya Sh400 milioni ni mwanasiasa kutoka Kaunti ya Kisii, Zaheer Merhali Zhanda.

Zaheer anajigamba kuwa na uhusiano wa karibu na Naibu Rais William Ruto na Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi.

Katika ukurasa wake wa Facebook ameweka picha akiwa na Bw Ruto, Rais Kenyatta, viongozi wa upinzani Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula.

Akiwa na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga. Picha/ Hisani

Pia kuna picha akiwa na Waziri wa Teknohama Joe Mucheru, na aliyekuwa naibu spika wa bunge Farah Maalim miongoni mwa watu wengine mashuhuri.

Alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliosafiri Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) wakati wa kesi dhidi ya Rais Kenyatta na Bw Ruto ambapo alionekana akisimama karibu na Bw Sudi na kiongozi wa wengi katika bunge Adan Duale, japo sio watu wengi waliomtambua.

Zhanda aligombea kiti cha ubunge cha Nyaribari Chache kwa tiketi ya Jubilee mnamo 2017 lakini akashindwa na Richard Tongi.

Akiwa na Naibu Rais Dkt William Ruto na Gavana wa Nairobi Mike Sonko. Picha/ Hisani

Anafahamika kama “mheshimiwa” kwa sababu ya kugombea kiti hicho na kushirikiana na wanasiasa.

Kwa kawaida, huwa anasafiri kwa helikopta au gari la kifahari la Lexus LX570. Anapenda maisha ya umaarufu na simu za kisasa aina ya iPhones na huwa anajishasha mitandaoni alivyo na pesa nyingi huku akisambaza picha akishika mamilioni ya pesa anazotoa katika harambee kaunti ya Kisii anazoalika wanasiasa.

Ushirika wake na wanasiasa wakuu sasa umeanza kumsumbua baada ya kubainika alihusika kupanga sakata ambapo mwanamfalme wa Miliki ya Kiarabu alitapeliwa mamilioni ya pesa.

Akiwa na Rais Uhuru Kenyatta. Picha/ Hisani

Matapeli hao walikuwa na ujasiri wa kujifanya waziri mwenye ushawishi mkubwa aliyedai kuwa na uwezo wa kuachilia dhahabu isafirishwe hadi Dubai.

Hata hivyo chuma chao kiliingia motoni mlalamishi alipomwandikia waziri huyo moja kwa moja akimtaka aachilie dhahabu hiyo.

Jumanne, seneta wa Bungoma Moses Wetangula alinukuliwa akijitenga na sakata hiyo ambapo Bw Zaheer na washirika wake wanadaiwa kumlaghai Bw Ali Zandi mamilioni ya pesa.

Akiwa na mwanahabari wa Citizen TV Hussein Mohammed na Gavana Sonko. Picha/ Hisani

Msaidizi wa kibinafsi wa Bw Wetangula, Chris Mandu alisema seneta huyo pia alipoteza pesa kwenye sakata hiyo.

Wapelelezi walisema Bw Zaheer ana marafiki wakubwa wa kibiashara na huenda yatakayofichuka yakashtua wengi.

You can share this post!

Tulizika vidoli kuwazima waliotaka kunyakua ardhi yetu,...

MAFUTA: Gharama ya maisha kupanda zaidi

adminleo