• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Msisimko Ingwe na Gor zikionana tena debi ya KPL

Msisimko Ingwe na Gor zikionana tena debi ya KPL

Na JOHN ASHIHUNDU

MAHASIMU wa jadi, AFC Leopards na Gor Mahia watakutana Jumapili kwa mara ya mwisho msimu huu katika mechi ya mkondo wa pili katika uwanja wa kimataifa wa Moi, Kasarani.

Mechi hii itakayoanza saa tisa alasiri itakuwa mara ya 91 kwa timu hizo kukutana kwenye ligi hiyo kuu ya taifa.

Zilipokutana katika mkondo wa kwanza pia uwanjani humo, Gor Mahia waliibuka na ushindi wa 2-0, lakini Leopards wameapa kulipiza kichapo hicho ambacho kilikuwa cha mara ya tano tangu Ingwe iwashinde 1-0 mnamo Mei 2016 kutokana na bao la Lamine Diallo.

Makocha wa pande zote mbili, Hassan Oktay wa Gor Mahia na Andrea Cassa Mbungo wanarejesha vikosi vyao uwanjani baada ya timu hizo kupoteza mechi zao katikati mwa wiki.

Leopards walibwagwa na KCB kwa 1-0 mjini Machakos, Jumatano, wakati Gor Mahia wakichapwa 1-0 na Nzoia Sugar katika mechi iliyochezewa Mumias Complex.

Gor Mahia wataingia uwanjani kutafuta ushindi ambao utawawezesha kutawazwa mabingwa wa msimu huu, kwani watakuwa wamefikisha pointi 60 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine.

Iwapo watafanikiwa, huu utakuwa ushindi wao wa mara ya 18 wakati Leopards ikijivunia taji hilo mara 13.

“Wapinzani wetu kwa sasa wanaongoza jedwalini, lakini kuhusu mechi ya Jumapili, wasitarajie mteremko. Walitushinda katika mkondo wa kwanza, lakini raundi hii watashangazwa jinsi tutakavyowakabili kuanzia dakika ya kwanza,” Mbungo alisema.

Kupoteza

Leopards wamepoteza mara tatu katika mechi 13 wakati Gor Mahia wameshindwa mara moja pekee katika mechi 10 za karibuni.

Kwa upande mwingine, wasimamizi wa mechi hiyo wamewahakikishia mashabiki usalama wa kutosha huku wakitoa mwito kwa kila mtu atakayekuwa uwanjani humo kuchangia kwa njia yoyote ile kuhakikisha kuna usalama wa kutosha.

Mkuu wa kitengo cha usalama katika kampuni ya SportPesa, Mathews Waria alitoa hakikisho hilo kwa mashabiki wote watakaofika uwanjani Jumapili katika mechi hiyo ambapo kocha Mbungo anatarajiwa kumuanzisha Whyvonne Isuza akishirikiana na Paul Were.

Gor Mahia kwa upande wao wanafurahia kurejea mastaa Jacques Tuyisenge, George Odhiambo, Francis Kahata na Kenneth Muguna kikosini.

Mashabiki watalipa Sh500 na Sh200 kushuhudia mechi hiyo.

Tiketi zitapatikana katika maeneo ya Kenya Cinema, Thika Road na nje ya uwanja wa Kasarani katika milango nambari 2 na 12.

You can share this post!

Yafichuka familia ya Moi iliogopa Huduma Namba

MWANAMKE MWELEDI: Mkondo wa maisha yake ulibadilika ghafla

adminleo