• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Kang’ata na Gavana Wa Iria warushiana cheche mbele ya Seneti

Kang’ata na Gavana Wa Iria warushiana cheche mbele ya Seneti

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Murang’a Mwangi wa Iria na Seneta wa kaunti hiyo Irungu Kang’ata wamerushiana cheche za maneno mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (CPAIC).

Bw Wa Iria ambaye alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo Ijumaa kujibu maswali yaliyoibuliwa katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Edward Ouko kuhusu jinsi ambavyo kaunti hiyo ilitumia pesa za umma katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018.

Gavana huyo alimshambulia Bw Kang’ata kwa kuchochea wakazi wa Murang’a dhidi yake saa chache kabla ya yeye (Wa Iria) kufika mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay Moses Otieno Kajwang’.

“Ni makosa kwa Seneta wangu Irungu Kang’ata kunichafulia jina katika runinga bila ushahidi wowote. Mbona alinihukumu mbele ya watu wangu wa Murang’a hata kabla ya kamati hii kunipa nafasi ya kutoa ufafanuzi kuhusu maswali yaliyoibuliwa katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali? Koma koma kuingiza siasa katika masuala muhimu kiasi hiki!” Bw Wa Iria akafoka.

Akijibu, Bw Kang’ata alijitetea akisema alikuwa akiwafahamisha wakazi wa Murang’a kuhusu masuala muhimu yaliyoibuliwa na Bw Ouko kuhusu shughuli za kifedha katika serikali hiyo.

“Sikuwa na nia mbaya. Kama kiongozi aliyechaguliwa na wananchi na kulingana na wajibu wangu wa kutetea ugatuzi, ni wajibu wangu kuzungumzia utendakazi wa kaunti yangu ya Murang’a katika majukwaa yote, ikiwemo runinga,” akasema Bw Kang’ata.

Katika ripoti yake ya mwaka wa kifedha wa 2017/2018 Bw Ouko ametaja visa kadha ambapo serikali ya kaunti ya Murang’a iltumia pesa za umma visivyo.

Kwa mfano, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anabaini kuwa madiwani wa kaunti hiyo walisafiri kwenda Mombasa mnamo Oktoba 2017 kwa gharama ya Sh80 milioni.

Hata hivyo, kaunti hiyo haikutoa stakabadhi za kuonyesha jinsi pesa hizo zilitumiwa.

“Na inashangaza kuwa ziara hiyo ilipiwa na Afisi Kuu ilihali bunge la kaunti ya Murang’a huwa na bajeti ya kugharamia shughuli zake, zikiwemo safari za madiwani na maafisa wa bunge hilo,” ripoti hiyo ikasema.

Bw Ouko pia anaibua maswali kuhusu matumizi ya Sh4,063,900 kufadhili safari za maafisa wa serikali ya Murang’a huku serikali ikifeli kutoa stakabadhi husika, kwa mfano risiti za ndege.

Uhasama kati ya Bw Kang’ata na Gavana Wa Iria unatokana na sababu kwamba seneta huyo anadaiwa kumezea mate kiti hicho ifikapo mwaka 2022 ikizingatiwa kuwa gavana huyo anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho.

You can share this post!

DAU LA MAISHA: Bidii yake yatambuliwa kazini

Rais Kenyatta aagiza shughuli ya usajili wa Huduma Namba...

adminleo