• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Huenda Mugabe akaitwa bungeni kueleza zilikoenda pesa za Almasi

Huenda Mugabe akaitwa bungeni kueleza zilikoenda pesa za Almasi

Na AFP

HARARE, ZIMBABWE

Ikiwa tutalazimika kumwagiza Bw Mugabe kufika mbele yetu, lazima atufafanulie kuhusu zilikoenda fedha hizo. Lazima atwambie kuhusu hatua ya serikali kuzifukuza kampuni za kibinafsi za uchimbaji madini, ilhali zilikuwa zikiiletea nchi faida kubwa ya kifedha – Temba Mliswa

HUENDA aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, akafika Bungeni kuelezea alikopeleka zaidi ya Sh1.5 trilioni anazodaiwa kupora kupitia biashara ya Almasi.

Hilo linatokana na ripoti maalum iliyoandaliwa na kamati moja ambayo inachunguza kashfa ya biashara ya uchimbaji wa madini hayo, wakati Bw Mugabe akiwa uongozini.

Mbunge Temba Mliswa ambaye anaiongoza kamati hiyo, anadai kwamba Bw Mugabe alikuwa mhusika mkuu katika biashara hiyo haramu. Bw Mliswa alikuwa mwanachama wa chama tawala cha Zanu-PF, ila akakigura.

Biashara hiyo ilikuwa ikiendelea katika migodi ya Chiadzwa, mashariki ya taifa hilo.

Mnamo 2016, Bw Mugabe aliliambia shirika la habari nchini humo kwamba nchi hiyo ilipata chini ya Sh200 bilioni kutokana na mauzo ya almasi. Hata hiyo, wachunguzi wanadai kwamba Bw Mugabe alinufaika kwa hadi Sh1.5 trilioni, kwani ndiye pekee aliyeidhibiti.

Mkewe, Grace, pia aliwahi kuhusishwa na biashara hiyo kupitia kwa kampuni moja ya kisiri.

Aidha, Mliswa alisema kuwa licha ya umri wake mkubwa, Bw Mugabe atahojiwa kuhusu hatua kuu ya serikali kuzifurusha kampuni zilizokuwa zikichimba madini hayo kutoka migodi hiyo mnamo 2006. Baada ya kuondolewa kwa kampuni hizo, ambazo nyingi zilikuwa za kibinafsi, serikali ilianza kusimamia uchimbaji wake.

 

Ufafanuzi

“Ikiwa tutalazimika kumwagiza Bw Mugabe kufika mbele yetu, lazima atufafanulie kuhusu zilikoenda fedha hizo. Lazima atwambie kuhusu hatua ya serikali kuzifukuza kampuni za kibinafsi za uchimbaji madini, ilhali zilikuwa zikiiletea nchi faida kubwa ya kifedha,” akasema Bw Mliswa, kwenye mahojiano na mtandao wa ‘New Zimbabwe.’

“Hatukuona manufaa yoyote ya biashara hiyo, licha ya nchi kupata mabiloni ya fedha,” akasema. Mugabe alishinikizwa kuondoka uongozini mnamo Novemba 2017 na jeshi.

Licha ya hayo, ingali kubainika ikiwa kiongozi huyo mkongwe atafika mbele ya kamati hiyo.

Hiyo itakuwa kashfa ya kwanza kumkabili yeye binafsi, baada ya kashfa za hapo awali kuwakabili mawaziri wake.

Miongoni mwa wale waliofunguliwa mashtaka ya kashfa za rushwa ni mawaziri wa zamani Samuel Undenge (Kawi) na Walter Nzembi, aliyehudumu kama waziri wa Mashauri ya Kigeni.

Wanawe Bw Mugabe; Bellarmine Chatunga na Robert Junior pia ni miongoni mwa watu ambao wanalengwa na serikali ya Rais Emmanuel Mnangagwa, kwa madai ya kuipora nchi hiyo mabilioni ya fedha kupitia kandarasi ghushi walizopata kwa mlango wa nyuma.

Alipochukua mamlaka mapema mwezi Desemba mwaka uliopita, Bw Mnangagwa aliapa kufanya kila awezalo “kulainisha utawala” wan chi hiuo, kwa kuhakikisha kuwa wale wote walioipora wamekabiliwa kisheria.

 

You can share this post!

Waititu amshtaki Ngilu kwa dai la kueneza chuki

Vitabu vilivyopewa wanafunzi na Serikali vimejaa makosa...

adminleo