• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
JAMVI: ‘Masimbajike’ wa Pwani walivyogeuka mahasimu wa kisiasa

JAMVI: ‘Masimbajike’ wa Pwani walivyogeuka mahasimu wa kisiasa

Na SAMUEL BAYA

SIASA ziliwaleta pamoja na inaonekana siasa hiyo hiyo sasa inawatenganisha. Hiyo ndiyo taswira kamili katika mienendo ya kisiasa ya mbunge wa Malindi Bi Aisha Jumwa na mwenzake wa Likoni Bi Mishi Mboko.

Ingawa wabunge hawa wawili ni maarufu sio tu Pwani bali kote nchini kutokana na siasa za makabiliano, matukio ya hivi karibuni yameonyesha kwa kina jinsi uhasama kati yao wao unaoendelea kukolea.

Wakati wa hafla ya mazishi ya Mzee Edward Kingi, ambaye ni babake naibu gavana wa Mombasa Dkt William Kingi huko Kilifi, Bi Jumwa ambaye alikuwa akiwatambua wabunge waliohudhuria hafla hakumtambua Bi Mboko, ila aliendelea tu kutaja wengine waliohudhuria.

Wote wawili wako ndani ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) lakini kwa sasa wamegawanyika kisiasa.

Bi Jumwa tayari ameamua kwamba atamuunga mkono naibu Rais Bw William Ruto kuwania Urais wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022 ilhali Bi Mboko kwa upande wake amewekeza imani yake kwa mrengo wa Bw Raila Odinga na Gavana wa Mombasa Bw Hassan Joho.

Tukio hilo la juzi ambalo lilifanyika mbele ya Gavana wa Kilifi Bw Amason Kingi lilionekana kumshtua hata gavana huyo ambaye hakusita kuliongelea alipofika jukwaani.

Na ili kutilia pondo umuhimu wa umoja wa viongozi wa Pwani, Gavana Kingi alitumia mazishi hayo kueleza ni kwa nini viongozi hao wawili wanafaa kushirikiana.

“Mimi kwa muda wote nimewajua Bi Jumwa na Bi Mboko kuwa dada wa karibu na ambao walikuwa katika dau moja katika safari ya ukombozi wa Pwani.

Wawili hawa walikuwa karibu mno hivi kwamba ungeligusa mmoja, mwengine angekurukia. Walikuwa pamoja ila leo hii ni masikitiko kwamba Bi Jumwa anaelekea huku na Bi Mboko anaelekea kule.

Ni aibu kubwa wakati tunapoanika hadharani ukosefu wa umoja (Pwani) kama viongozi,” akasema Gavana Kingi akihutubia waombolezaji.

Ingawa hatukuweza kupata maoni ya viongozi hao wawili maarufu, tulifanikiwa kuongea na washirika wao wa karibu kutaka kujua endapo wawili hawa wamekosana kiukweli.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini Bw Owen Baya ambaye ni mshirika wa karibu sana na Bi Jumwa alikana madai kwamba wawili hao wametengana.

“Mimi ninajua wako pamoja kama viongozi wa Pwani ila kila mtu sasa amechukua mkondo tofauti wa kisiasa. Hilo pekee ndilo linanoonekana kuwagawanya lakini hii pia ni demokrasia,” akasema Bw Baya

Aidha alikana madai kwamba Bi Jumwa alikosa kumualika Bi Mboko kimaksudi, akizingatia kwamba halikuwa jukumu lake kumualika mwenzake huyo.

Bi Mboko alikuwa amefika kumwakilisha Gavana wa Mombasa Bw Hassan Joho kwa hivyo basi alijua kwamba mtu tu ambaye angemualika Bi Mboko ni Gavana wala sio yeye,” akasema Bw Baya.

Naye Bw Mwambire ambaye ni mshrika wa karibu wa Bi Mboko alikana kuwa wawili hao hawapiki chungu kimoja, akisistiza kwamba kila mmoja analenga upande tofauti lakini wao ni viongozi wa Pwani kwa hivyo lazima waongee kwa sauti moja.

“Mmoja yuko katika kundi la ‘Kieleweke’ na mwengine yuko katika kundi la ‘Tangatanga’. Wacha tuwapatie nafasi kila mmoja aonyeshe fursa yake ila hakuna uhasama wowote kutoka kwa wawili hao,” akasema Bw Mwambire.

Mbunge wa Taveta Dkt Naomi Shaban pia alikana kwamba wawili hawa hawasikilizani.

“Mimi niko nao hapa bungeni na ninawaona kama wadogo zangu ambao wako pamoja. Hii stori ya kwamba wamekosana ama hawaelewani ni mtizamo wa vyombo vya habari,” akasema mbunge huyo.

Aidha Dkt Shabaan alisema kuwa huenda hatua ya Bi Jumwa kukosa kumtambua Bi Mboko mazishini haikufanyika kimaksudi ila kulikuwa na utaratibu fulani au labda kughafilika tu kwa mbunge huyo.

“Mara nyingine hutokea. Mimi ni mbunge wa miaka mingi na mara nyingine huwa ninaenda katika hafla kisha hakuna mtu ambaye ananitambua. Mimi ninaamini hili hufanyika mara kwa mara na huwezi kutumia kigezo kama hicho kusema kwamba hawa hawapatani,” akahoji Dkt Shaban.

Hata hivyo, alisema yuko tayari kuongea na wawili hao kama dada yao mkubwa endapo atahisi kuna tatizo.

Hata hivyo baadhi ya wataalam wa siasa wanaamini kwamba viongozi hawa wawili wametofautiana kabisa kisiasa na uhasama wao unaendelea kupanda wakati uchaguzi wa 2022 unapokaribia.

Akiongea na Jamvi la Siasa, Prof Hassan Mwakimako alisema kuwa viongozi hao kwa sasa wana malengo tofauti na ni chama pekee ambacho kinaonekana kuwaweka pamoja.

“Hawa wawili wako katika mirengo tofauti ya kisaisa licha ya kuwa katika chama kimoja. Mmoja anaunga mkono upande wa Bw Ruto na mwingine anaunga mkono Gavana Joho. Sasa basi ni wazi siasa za kitaifa zimeleta uhasama katika siasa za Pwani,” akasema Prof Mwakimako.

Alisema kuwa Bi Mboko yuko karibu sana na Gavana Joho ilhali Bi Jumwa anaegemea mrengo wa Ruto ambao unapingana na ule wa Bw Joho.

“Pili, kuna tetesi kuwa ikiwa Bi Jumwa ataondolewa kwa mfano katika ODM, atakayefaidika zaidi kwa upande wa mama ni Bi Aisha Mboko.

Kuna uwezekano ya kuwa pengine ODM wakafikiria kwamba vile vyeo ambavyo wamempa Aisha Jumwa, wakimuondoa basi vile vyeo vitachukuliwa na Bi Mboko, zaidi katika kamati za bunge la Kitaifa. Hii ni mojawpao ya suitafahamu kubwa kati ya viongozi hawa wawili,” akasema Prof Mwakimako.

Aidha mtaalam huyo alisema kuwa uhasama wa viongozi hawa wawili ni hatari ya kimaendeleo ya siasa za Pwani.

“Inahatarisha kwa sababu ikiwa hawataelewana, hawataweza kuleta umoja kwa wananchi kwa sababu kila mmoja ana wafuasi wake. Ni hatari kwa sababu kila viongozi wanapozozana, wafuasi nao huwa wanafuatilia viongozi wao wanasema nini. Kuweza kuleta kauli moja ya kipwani itakuwa changamoto,” akasema Prof Mwakimako.

“Siasa za vyama zinaingiliana na maisha yao kwa hivyo ni wazi kwa vile wako na misimamo tofauti ya kisiasa, basi lazima tofauti za kibinafsi bado ziko,” akaongeza Prof Mwakimako.

Kulingana na Bw Kazungu Katana ambaye ameandika na kuchunguza siasa za Pwani kwa miaka mingi, uhasama umekuwa wazi miongoni mwao.

Aidha Bw Katana alisema kuwa Bi Mboko na Bi Jumwa walikuwa pamoja kwa sababu wote walikuwa katika chama cha ODM. Lakini sasa wametofautiana kimawazo na kisera hivyo basi kila mmoja anaenda kivyake.

Alisema kuwa uhasama wa wabunge hao wawili pia huenda umechangiwa na maslahi yao ya kibinafsi.

“Hatugawanywi na siasa za kutoka nje bali tunagawanywa na siasa za kibinafsi. Bi Jumwa anafuta maslahi yake ya kibinafsi akiwa na Ruto, na Bi Mboko anafuata maslahi yake ya kibinafsi akiwa na Gavana Joho,” akasema Bw Katana.

Aliongeza kwamba hata wakati viongozi hawa wawili wanapokosana, sio kwa sababu ya misingi ya vyama vya kisiasa ila misingi ya kibinafsi.

“Bi Mboko haongei kuhusu wakazi wa Pwani, naye Bi Jumwa pia haongei kuhusu maslahi ya wakazi wa Pwani. Wote wanaongea kuhusu maslahi yao ya leo na kesho na wanaongea kufurahisha wale vigogo wa siasa ambao wanawashabikia wao wenyewe,” akasema Bw Katana.

Ni wazi kwamba mgawanyiko huu wa Bi Jumwa na Bi Mboko utaendelea kuwa mojawapo ya masuala ambayo yatakuwa yakiangaliwa kwa makini katika mchakato mzima wa kujaribu kuwaleta viongozi wa Pwani pamoja.

You can share this post!

JAMVI: Kuzomewa kwa Raila ni dalili ‘Jakom’ hawiki...

JAMVI: Sababu kuu za Ruto kuhepwa na wandani

adminleo