• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
UBABE: Google yaizima Huawei kutumia huduma za Android na Google Play Store

UBABE: Google yaizima Huawei kutumia huduma za Android na Google Play Store

PETER MBURU na BERNARDINE MUTANU

UHASAMA wa kibiashara baina ya Amerika na Uchina kuhusu kampuni ya kutengeneza simu ya Huawei unazidi kutokota, baada ya kampuni ya Alphabet Inc (awali Google) kuzuia ile ya Huawei kutotumia  huduma muhimu kwenye simu zake, hatua ambayo ni pigo kwa kampuni hiyo ya Uchina.

Simu mpya za Huawei ambazo zitatengenezwa sasa hazitakuwa na apu zinazotolewa na kampuni ya Alphabet, hatua inayokuja baada ya Rais Donald Trump kuorodhesha Huawei kati ya kampuni ambazo kampuni za Amerika hazitaruhusiwa kufanya biashara nazo, hadi zipewe leseni.

Kupitia ujumbe rasmi, Alphabet ilisema kuwa ilikuwa ikifuata amri na kuwaza kuhusu matokeo ya kutotii, ikisema huduma za Google Play Store na nyingine zitakosekana kwa simu za Huawei.

Kampuni ya Huawei, hata hivyo, haijazungumza kuhusu hatua hiyo.

Kufuatia hatua hiyo, Huawei aidha haitapokea mawasiliano ya usalama kutoka kwa Google, misaada ya kiufundi, na simu zake mpya hazitakuwa na apu kama Youtube, Google Maps, Google Photos, Google Sheets, Google Contacts wala Google Assistant.

Hata hivyo, wanaotumia simu za Huawei kwa sasa wataendelea kuzipokea huduma hizo, lakini Google ikisasisha muundo wake wa Android, simu za Huawei hazitaweza kupokea huduma hizo.

Wadadisi wa masuala ya biashara wamesema kuwa hatua hiyo itakuwa pigo kubwa kwa kampuni ya Huawei kwani huenda ikapoteza wateja wengi.

Jumatano wiki iliyopita, serikali ya Rais Trump iliorodhesha Huawei kati ya kampuni ambazo haziwezi kushirikiana na US katika biashara za kiteknolojia, bila kuruhusiwa na serikali.

Lakini Afisa Mkuu Mtendaji wa Huawei baada ya hatua hiyo alisema kuwa “tumekuwa tukijiandaa kwa hili.”

Alisema kampuni hiyo itaanza kujitengenezea vifaa vyake, wakati mataifa ya magharibi yanazidi kususia bidhaa zake.

Kampuni hiyo imesisitiza kuwa utendakazi wake ni huru na kuwa hauingilii na serikali ya China.

Uingereza, hata hivyo, bado haijatangaza rasmi kupiga marufuku bidhaa za kampuni hiyo.

Hatua hii ya punde inaweza kuathiri bishara ya Huawei kwani wateja wengi hawatakubali kununua simu ambazo hazina apu kama Google Play Store kati ya apu nyingine nyingi ambazo watumizi huzipenda, ikiwa ni baadhi ya zitakazokosekana.

Lakini Huawei inasema ilikuwa tayari kwa hatua ya aina hiyo, na huenda imejipanga kukabiliana na hali.

Majuzi, Huawei ilizindua msururu wa simu mpya katika soko la Kenya. Huawei imezindua simu aina ya P30 ambazo ni P30 Pro, P30 na P30 Lite, katika ajenda ya kampuni hiyo ya kuimarisha mawasiliano ulimwenguni kupitia kwa ubunifu.

Simu aina ya P30 Pro itauzwa kwa Sh99, 999 ilhali P30 itauzwa kwa Sh72,999 na P30 Lite itauzwa kwa Sh29,999.

Simu hizo zina uwezo mkubwa wa kamera na zinaweza kupiga picha za ubora wa juu zaidi.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa simu hizo, rais wa Huawei Kenya Steven Li alisema simu za Huawei P30 ni mafanikio makubwa tangu baada ya simu za kamera dijitali kuzinduliwa nchini.

Simu hizo zina sensa ya uwezo wa juu na lenzi iliyo na uwezo wa kuvuta kitu karibu na kamera ya kisasa.

“Tangu zilipozinduliwa, simu za Huawei P Series zimekuwa na lengo moja tu kwa wateja: Kwamba simu inaweza kuwa na uzani wa chini, ya kuvutia na inaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kupiga picha. Simu za P30 Series zinaunganisha teknolojia na ubunifu na zina ushindani mkubwa hata kwa kamera kubwa, bila kuhitaji usaidizi wa vifaa vya nje,” alisema Bw Li.

Wateja Wakenya wanaweza kununua simu hizo mtandaoni kupitia Jumia, Kilimall na Masoko, kabla ya simu hizo kufika madukani.

Lakini wadadisi wa masuala ya kiteknolojia aidha wanasema kuwa huenda hatua ya kuizima Huawei  ikaishia kuathiri kampuni ya Google, kwani inaweza kuzipa kampuni za kutengeneza simu sababu ya kuanza kuwaza aidha kujitengenezea huduma ambazo zinauziwa na kampuni hiyo ama kutafuta kampuni nyingine za kuwapa.

Hata hivyo, mataifa kadhaa yameeleza wasiwasi kuwa bidhaa za Huawei zinaweza kutumiwa na China kuwa ikipata habari za kiujasusi kutoka mataifa mengine, japo kampuni hiyo imepinga madai hayo vikali.

 

You can share this post!

Microsoft kushirikiana na vyuo vikuu kuvumisha teknolojia

Breki kwa marufuku ya matangazo ya kamari

adminleo