• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
RIPOTI: Wazee wa zaidi ya miaka 50 walitia mimba wasichana 6,700 Murang’a

RIPOTI: Wazee wa zaidi ya miaka 50 walitia mimba wasichana 6,700 Murang’a

Na PETER MBURU

RIPOTI ya kusikitisha imeonyesha kuwa wasichana 6,710 walipata uja uzito Kaunti ya Murang’a mwaka 2018.

Utafiti huo ambao ulifanywa na serikali ya kaunti hiyo ulionyesha kuwa wasichana hao walikuwa wa umri kati ya miaka 10 na 19.

Vilevile, utafiti huo ulishtua kuonyesha kuwa asilimia 70 ya wanaume ambao walifanya ngono nao ni wa zaidi ya miaka 50.

Ni asilimia 30 pekee ya wavulana ambao walifanya ngono nao ambao walikuwa wa umri sawa na wao, ripoti hiyo ikasema.

Baadhi ya waliowafanyia hivyo walitumia vivutio kama kuwabeba wasichana kwa Boda Boda, kuwanunulia chipsi, vinywaji na soseji, ili ‘kulala’ nao.

Wasichana 140 wa umri kati ya miaka 10 na 14 walitiwa mimba, huku wengine 25 wa umri kati ya 10 na 19 wakiziavya.

Utafiti huo ulifanywa katika vituo vya afya kaunti hiyo, wanaume 22 baadhi yao wa umri zaidi ya miaka 50 wakihusishwa na visa hivyo.

Takwimu aidha zilionyesha kuwa wasichana 6,570 wa umri kati ya miaka 15 na 19 walijifungua, nao 679 wa umri kati ya miaka 10 na 14 wanatumia mbinu za kupanga uzazi.

Baadhi ya wadhulumiwa wa kingono walidai kuwa walidhulumiwa kingono na watu wa familia, marafiki wa karibu, nao wengine wakabakwa na watu wasiowajua.

Wahudumu wa afya walisema kuwa wasichana wengine 4,477 wa umri kati ya miaka 15 na 19 walikuwa wakitumia mbinu za kupanga uzazi.

Wasichana wengine wa umri kati ya miaka 20 na 24 wanatumia mbinu za kupanga uzazi, wakiaminika kuwa katika vyuo ama vyuo vikuu.

“Tuna timu ambayo inafuatilia visa hivi,” waziri wa afya Joseph Mbai akasema.

You can share this post!

Asamoah Gyan astaafu soka ya kimataifa

Arsenal kufagia wachezaji waliosalia na miaka miwili kwenye...

adminleo