• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Arsenal kufagia wachezaji waliosalia na miaka miwili kwenye kandarasi

Arsenal kufagia wachezaji waliosalia na miaka miwili kwenye kandarasi

NA CECIL ODONGO

USIMAMIZI wa Arsenal umetoa amri kwa wachezaji waliosalia na chini ya miaka miwili kabla kandarasi zao kukamilika kama Mesut Ozil na Emerick Aubameyang kuzirefusha au wapigwe mnada kwa klabu nyingine.

Mkurugenzi Mkuu wa Arsenal Vinai Venkatesham amewaonya wachezaji hao kwamba lazima warefushe kandarasi zao kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Uingereza(EPL) kuanza mwezi Agosti la sivyo klabu haitakuwa na budi ila kuwauza.

“Lazima tuhakikishe tuna nidhamu. Wachezaji kwenye kikosi cha kwanza waliosalia na miaka miwili kabla ya kandarasi zao kutamatika lazima wasaini kandarasi nyingine ili kutupa fursa nzuri ya kujiandaa kwa msimu mpya. Hatutaki kufanya uamuzi mgumu kipindi cha mchezaji kinapokamilka kisha wao huhama na kutuachia hasara kubwa,” akasema Venkatesham kupitia mtandao wa klabu.

“Tumeamua tunarefusha kandarasi za wachezaji au kuwauza. Hili ni jukumu zito na lazima tulitekeleze bila kuzingatia hadhi ya mchezaji. Hatutaki tujipate kwenye hali ya kuwaacha wachezaji kusajiliwa na klabu nyingine bure ila iwapo tu wanaagana na taaluma yao ya soka,” akaongeza afisa huyo.

Mienendo ya Arsenal kuwaachilia wachezaji kukamilisha kandarasi zao kisha kuondoka bila kulipiwa chochote kumewaponza hasa baada ya kiungo Aaron Ramsey kuagana na klabu hiyo ili kujiunga na Juventus ya Italia kama mchezaji huru msimu ujao wa 2019/20.

Mnamo mwaka wa 2018, Arsenal haikupata hata peni baada ya Alexis Sanchez kuhamia Manchester United kama mchezaji huru sababu kuu ikiwa kukamilika kwa kandarasi yake.

Arsenal sasa yaonekana kuerevuka ili matukio hayo yasijirudie na pia kuwapa sajili wao wapya muda wa kunawiri hadi kuwa wachezaji tajika.

You can share this post!

RIPOTI: Wazee wa zaidi ya miaka 50 walitia mimba wasichana...

Mfadhili wa nishati ya upepo Lamu atisha kujiondoa

adminleo