• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 9:50 AM
Kenya taifa bora zaidi kwa maisha ya kidijitali Afrika

Kenya taifa bora zaidi kwa maisha ya kidijitali Afrika

Na PETER MBURU

KENYA imeorodheshwa kuwa taifa bora zaidi barani Afrika ambapo maisha mazuri zaidi yanapatikana, katika ulimwengu wa kidijitali.

Hii ni kulingana na ripoti ya hivi punde zaidi kutoka shirika la InterNations, ambayo iliorodhesha Kenya nambari 31 duniani, mbele ya Afrika Kusini (nambari 49), Morocco (58), Uganda (59) na Misri (69).

Katika ripoti hiyo, Kenya inaonekana kutoa huduma nzuri za kidijitali, kwa kuwa watu tisa kati ya kumi nchini (asilimia 89) wanaridhishwa na huduma za mitandaoni bila vizuizi.

“Kufanya malipo ya bila kutumia pesa taslimu Kenya aidha kunaonekana kuwa rahisi kukiwa asilimia 94, ikilinganishwa na kiwango cha kawaida duniani cha asilimia 78.

Ripoti hiyo aidha iliorodhesha Kenya nambari tano duniani kwa urahisi wa kupata nambari ya kibinafsi ya humu nchini. Mataifa yaliyoongoza ni Myanmar, New Zealand, Israel na Estonia.

Afrika Kusini iliorodheshwa kati ya mataifa kumi ambapo kupata nambari ya simu ya kibinafsi ni vigumu sana.

Aidha, ripoti hiyo ilisema taifa hilo halipati huduma nzuri za mitandaoni kutoka kwa serikali, likiorodheshwa nambari 58 kati ya 68 duniani.

Uganda nayo iliorodheshwa kati ya mataifa mabovu zaidi katika maisha ya kidijitali, ambapo hakuna intaneti ya kuridhisha, na pia ambapo kulipa sharti mtu awe na pesa taslimu.

“Asilimia 12 ya watu walisema ni vigumu sana kununua kitu bila pesa taslimu Uganda,” ripoti hiyo ikasema.

Utafiti huo huangazia maisha ya kidijitali, kwa kuangazia masuala tofauti kama kujiburudisha, afya, maslahi na usafiri.

You can share this post!

Mwanamume ataliki mkewe ili aishi na mamaye mzazi

Mbunge wa zamani akwepa majukumu ya malezi

adminleo