• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
BONGO LA BIASHARA: Mbinu za kushamiri katika uchuuzi wa vazi aina ya suti

BONGO LA BIASHARA: Mbinu za kushamiri katika uchuuzi wa vazi aina ya suti

Na STEPHEN DIK

“BIASHARA haigombi” na “Riziki haivutwi kwa kamba” ni methali mbili ambazo zinalenga biashara.

Unapoingia sokoni utapata wachuuzi wengi, wengine wanauza bidhaa za aina moja na wamezipanga upande mmoja. Licha ya hivi, kila mchuuzi hupata riziki yake ya kila siku.

Jared Juma anafanya kazi ya kuuza nguo, kazi ambayo inafanywa na watu wengi si haba.

Jared, anayefahamika zaidi kama “Nyang’ori”, ni mzaliwa wa kijiji cha Mudembi, eneo bunge la Budalang’i kaunti ya Busia, anasimulia jinsi alivyoanza biashara yake ya kuuza nguo aina ya suti.

Anasema kwasababu wauzaji wa nguo huwa wengi, yeye huuza kwa soko mbali mbali za kaunti ya Busia bila kuzingatia soko moja pekee. Anasema mavazi ya suti ambayo anauza, huwa ni suruali ndefu iliyoshonwa pamoja na koti lake kando, kwa kawaida suti hufanana rangi na yaweza kuvaliwa na tai.

“Suti ni vazi ambalo linapendwa na watu wenye heshima, unapovaa suti watu wanakuheshimu kiasi kwamba hata kama huna senti mfukoni waonekana aliye nazo,” anasema Nyang’ori.

Anaeleza kuwa suti nzuri mpya huuzwa kwa zaidi ya Sh5,000 dukani lakini yeye huuza suti nzuri za mtumba kwa kati ya Sh700 na Sh1,200 pekee.

Alipokamilisha elimu yake ya shule ya msingi mwaka wa 2001, alienda Port Victoria kuvua samaki.

Aliajiriwa ziwani kusaidia wavuvi kuvuta neti iliyorushwa majini wakati wa kuvua samaki, ambapo alifanya kazi hii kwa miezi kadhaa.

Nyang’ori anasema alipoona kazi hii ya kuvua samaki ilikuwa ngumu na malipo ni duni, mwaka wa 2002 aliiacha na kuenda kuajiriwa kwingine kufanya kazi ya kulinda boma.

Wakati alikuwa akifanya kazi ya kulinda boma, rafikiye waliyesoma pamoja naye alikuwa ameajiriwa kuuza nguo karibu na mahali hapo, aliuza aina ya nguo kama vile shati, suruali ndefu na makoti ya watu wazima, wake kwa waume.

Nyang’ori alikuwa akimtembelea rafikiye kila mara mahali alikuwa akiuzia nguo na hata kumsaidia kuuza. Kazi hii ilimfurahisha Nyang’ori, na kwa bahati mbaya mwaka wa 2006, kazi ya kulinda boma iliharibika na akasimamishwa kazi.

Aliajiriwa kuuza nguo pamoja na rafiki yake kwasababu alionekana kuwa mtu mwenye bidii zaidi katika biashara hiyo ya nguo. Baadaye 2013 alipopata mtaji wa kumtosha, akaacha na kujiajiri mwenyewe kwani alikuwa tayari amepata ujuzi wa biashara hiyo.

Yuajua mahitaji ya wateja

Akiwa na mtaji wa Sh11,000 alienda kununua suruali ndefu na makoti kwa sababu alijua mahitaji ya wateja.

Ilikuwa bahati mbaya kwake kwani robota aliyonunua mara ya kwanza ilikuwa na nguo zenye viuno vikubwa na makoti mapana zaidi na wateja wengi waliokuja kuulizia nguo walikuwa wembamba. Alipata hasara kubwa wakati huo.

Ilimbidi apeleke nguo hizo zote kwa fundi ili zipunguzwe ili zitosheleze wateja.

Kwa sababu hii, alijikokota kuuza nguo hizo kwa muda mrefu na zilipoisha akarudi kutafuta ushauri kwa yule mwajiri wake aliyemwajiri mwanzoni kumuuzia nguo.

Mwajiri huyo alimpeleka Nairobi, mahali ambapo alikuwa akinunua nguo zake za kuuza.

Alinunua nguo nyingi nzuri kwa urahisi, anasema badala ya kununua robota lililofungwa.

Walichagua nguo nzuri nzuri zilizoanikwa kwenye vibanda. Waliuziwa suruali ndefu kwa kati ya Sh120 na Sh500 na makoti kwa kati Sh200 na Sh800.

Kuanzia hapo biashara yake ilinoga ambapo huuza suti kwa bei ya jumla na kwa bei ya rejareja, huingiza kati ya Sh10,000 na
Sh20,000 kwa mwezi.

Anasema biashara hii huwa nzuri kuanzia Oktoba hadi Desemba. Nyang’ori anashauri kwamba uuzaji wa nguo hutegemea uzuri wa nguo hizo na wingi wake, wateja hupenda kununua nguo nzuri na wanahitaji kuona nguo nyingi tofauti ili wachaguwe zinazowafaa, nguo zikiwa chache wanashindwa kuchagua na kununua.

Anaongeza kusema ni muhimu kuwa na ujuzi katika biashara ya nguo ndipo uweze kuuza kwa sababu Desemba ambapo wanunuzi ni wengi, wauzaji wa nguo pia huwa wengi zaidi.

You can share this post!

Ripoti yafichua ‘serikali mbili’ Kenya

Kauli ya Ndindi Nyoro kwa Raila Odinga

adminleo