• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
UCHUNGUZI: ‘Nduma’ za Nairobi hukuzwa kwa maji ya vyoo

UCHUNGUZI: ‘Nduma’ za Nairobi hukuzwa kwa maji ya vyoo

Na SAMMY WAWERU

VIAZI vikuu maarufu kama nduma ni miongoni mwa vyakula vinavyothaminiwa na Wakenya wengi hasa wakati wa staftahi.

Vinaorodheshwa kati ya viazi asili, na hustawi maeneo yenye chemichemi. Ukizuru mashambani, hasa mashamba yaliyoko kwenye mitaro hutakosa kuona nduma zinazoendelea kukua.

Viazi hivi vinaandaliwa kwa njia ya kuchemsha au kupika kama kitoweo, kinachochanganywa na viazi mbatata ama ndizi.

Maeneo ya mijini, nduma zinaenziwa kwani mbali na mkate wa boflo, baadhi ya wakazi huvitumia kama staftahi.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya afya, vina ukwasi wa madini ya protini, wanga, copper na iron, na huaminika kusaidia katika mzunguko wa damu mwilini.

Pia vimesheheni Vitamini B, madini muhimu kwa mama mjamzito. Wanaoshuhudia shida ya asidi na kusokotwa na tumbo wanashauriwa kula nduma kwa wingi.

“Madini yake tele yanasaidia kukabiliana na shida za figo, moyo na hata kudhibiti ugonjwa wa msukumo wa damu,” anaeleza Maryanne Njeri, ambaye ni mtaalamu wa afya katika Hospitali ya Ladnan, jijini Nairobi.

Licha ya tija zake kiafya na kimapato, Je; Unafuatilia kujua vinakokuziwa, mazingira yake, mbali na dhana kuwa vinalimwa maeneo ya mashambani?

Ni suala muhimu, ambalo wewe kama mlaji unapaswa kutilia maanani hasa unapovinunua.

Vyombo vya habari vimekuwa vikiangazia mboga pekee zinazopandwa kwa kutumia majitaka jijini Nairobi na miji mingine nchini, na kwenye uchunguzi wetu imebainika kuwa viazi hivi pia vinakuzwa kwa maji machafu.

Taifa Leo Dijitali imefanya ziara ya uchunguzi katika mitaa kadhaa Nairobi, kama vile Kahawa West, Githurai, Zimmerman na Kasarani, na kugundua kuna baadhi ya wakulima wanaokuza nduma kwa majitaka.

Kwa mfano, eneo la Roysambu, katika kipande kimoja cha ardhi viazi vikuu vinavyoonekana kunawiri vinatunzwa kwa mkusanyiko wa maji yaliyoachiliwa kutoka kwa ploti kadhaa za makazi.

Mitaro ya majitaka imeelekezwa shambani, na kuundiwa mitaro midogo ‘inayolisha’ mimea kwa maji. ‘Maji’ tunayotaja hapa ni yatokayo katika majumba ya kuishi yenye vyoo, ikizingatiwa kuwa hutiwa kemikali ili kuzima uvundo baada ya haja.

Pia, ni maji ambayo yamejumuisha yaliyotumiwa na watu baada ya kuoga na kufua mavazi na kuosha vyombo kwa sabuni.

Katika kipande cha shamba eneo la Zimmerman, tunapata viazi vikuu vinavyoonekana vimeanza kuvunwa. La kutamausha mbali na kukuzwa kwa majitaka, vimepandwa nyuma ya choo kinachotumika!

Ni katika kisa hicho, tunakutana na mkazi mmoja na ambaye hatutataja jina lake kwa sababu za kiusalama anaeleza kwamba ukuzaji wa nduma katika kipande hicho umedumu kwa miaka kadhaa.

“Vinapovunwa, huona wakivipaka udongo mwekundu (red loam soil) ili vionekane kana kwamba vimetoka mashambani,” anasema.

Anafichua kuwa mkulima mmiliki huvivuna mchana hadharani, na bila wasiwasi wowote. “Ni shughuli inayofanywa mchana peupe,” asisitiza.

Hali kadhalika, ndizi ni miongoni mwa mimea inayozalishwa kwa kutumia majitaka eneo hilo.

Taswira hiyo si tofauti na ya mtaa wa Githurai na Kahawa West. Cha kushangaza zaidi katika mitaa hii, viazi hivi vimelimwa pembezoni mwa barabara kuu, na ambazo uhakika upo zinatumiwa na wadau kutoka sekta ya kilimo na Halmashauri ya Kitaifa ya Mazingira (Nema).

Katika mpito wa barabara inayounganisha Githurai 44, Kahawa West na Ruiru, rangi ya kijani inayolaki macho ni ya viazi asili hivi na ndizi.

Maji ni kiungo muhimu katika kufanikisha kilimo, lakini yale taka yakitumika ina maana kuwa mazao hayo yatakuwa na chembechembe zenye sumu katika mwili wa binadamu.

Wataalamu wa masuala ya kilimo wanahimiza umuhimu wa mimea kukuzwa kwa maji safi, ili kuepuka kuathiri usalama wa mazao.

“Chakula salama ni kilichokuzwa kwa maji safi na kuepuka utumiaji wa kemikali kudhibiti magonjwa na wadudu. Taasisi za utafiti wa kilimo zimeibuka na dawa ambazo ni salama kukabiliana na changamoto ibuka,” anafafanua Meshack Wachira, mtaalamu wa kilimo.

Baadhi ya magonjwa yanayoathiri binadamu, yanasemekana kusababishwa na lishe anayotumia. Viazi vikuu na mimea mingine ya kula inapolimwa kwa majitaka, ni wazi mazao hayo ni hatari kwa walaji.

Chini ya katiba inayotumika kwa sasa na iliyoidhinishwa 2010, sekta ya kilimo iligatuliwa na ni wajibu wa serikali za kaunti kupitia wizara husika kutathmini shughuli za kilimo zinavyoendeshwa.

Nema, pia ndiyo taasisi iliyotwikwa majukumu na serikali ya kitaifa kuangazia mazingira hivyo basi ina kibarua kujua kinachoendelea katika mazingira.

You can share this post!

Wilfred Ndidi afunga pingu za maisha

Wakenya kulipa mamilioni kurembesha makazi ya Ruto

adminleo