• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
NDOA: Sababu ya mume na mke kuandamana kwa baa kila siku

NDOA: Sababu ya mume na mke kuandamana kwa baa kila siku

NA MWANGI MUIRURI

KWA miaka mitano sasa, Bw James Kiai na mkewe (pichani) katika Kaunti ya Murang’a wamekuwa wakionekana ndani ya baa pamoja na kuzua mijadala wa hapa na pale kuwahusu, huku wengi wakiwadhania kuwa makachero.

Wao ni mume na mke na ambao huandamana katika vilabu. Mume akiagiza pombe, mke naye huletewa soda lakini bili hulipwa na mke.

Bi Kiai ana miaka 36 huku mumewe akiwa na miaka 63 na wanasema kuwa bora tu wako na vitambulisho vya kitaifa na pia wamejisajili katika mpango maalum wa Huduma Namba, na wameafikiana kuwa katika uhusiano rasmi wa mume na mke, wewe bakia papo hapo ukiwazia kuhusu tofauti hiyo ya miaka yao.

Ukitaka kuwachukulia kama binti na babake ni sawa, lakini wao wakisema “hali yetu rasmi ni kuwa huyu ni mke wangu nami ni mume wake.”

Kwa pamoja wako na watoto wawili wa kati ya miaka minne na mitatu, lakini familia hii ikiwa na watoto wanane kwa ujumla kwa kuwa ndoa ya awali ya huyu mzee ilikuwa na watoto sita.

Maisha ya mzee Kiai anayataja mwenyewe kama matamu, pesa ako nazo na mapenzi ako nayo na anakiri kuwa “huyu mke wangu wa pili huwapenda sana watoto alionipata nao na wao wanampenda kama mama yao.”

Lakini yule mkubwa katika familia hiyo katika safu ya watoto ako na miaka 34, basi huyu Bi Kiai akiwajibikia jina mama wa kambo kwa mtoto ambaye tofauti ya miaka kati yao wawili ni miwili tu….

“Angekuwa wangu halisi, ina maana kuwa nilimpata nikiwa na miaka miwili tu…lakini hiyo ndiyo raha ya familia yangu mseto.. yeye hunitambua kama mama yake na mimi humtambua kama mtoto wangu licha ya kuwa yeye ni wa rika yangu,” asema.

Taifa Leo Dijitali ilipata fursa nadra ya kuwahoji wawili hawa kuhusu uhusiano wao wa karibu kwenye vilabu na maeneo ya burudani.

“Hivi ndivyo katiba yetu iko ya ndoa. Mume wangu hunywa pombe na huwa ananiambia niandamane naye. Huwa namlinda dhidi ya ushawishi usiofaa akishalewa. Ni jukumu langu kuhakikisha halipishwi bili visivyo, hachumbiwi na wengi wa kutaka kuvuna wasipopanda na hatimaye, anafika nyumbani salama,” asema Bi Lucy Kiai.

Anasema kuwa haoni shida yoyote katika mpangilio huo kwa kuwa “ni maelewano yetu pamoja chini ya uthabiti wa majadiliano.”

Wanawake Murang’a waandamana wakipinga ulevi kiholela wa waume zao. Picha/ Mwangi Muiruri

Anasema kuwa kabla ya wao wawili waoane, akiwa mke wa pili baada ya wa kwanza kuaga dunia, maisha yake yalikuwa ya kujisahau ndani ya baa.

“Alinieleza kuwa alikuwa akiingia ndani ya baa akiwa na Sh30,000 kwa mfano, zinaisha zote na hatimaye anaachwa akiwa na madeni…Leo hii, ndani ya baa atatumia Sh500 peke yake. Kisha tunafululiza hadi nyumbani na huwa anafurahia sana mpangilio huu kwa kuwa ameanza kujijenga kimaisha na pesa zake ambazo hupata kama dalali wa vifaa vya ujenzi,” asema.

Bw Kiai anasema kuwa hali hii sio ya kipekee kwa maisha yake, bali ni kiungo thabiti cha utulivu wake.

“Wengine husema kuwa nimezoeesha mke wangu vibaya kwa kuandamana nami kwa baa, wengine wakiashiria kuwa atakuja kuvutiwa na ulevi au na wanaume wengine walio na mihela…Lakini hayo ni maoni tu ya walio na uhuru wa kutuchambua, sisi tuko sawa,” asema.

Bi Kiai anatoa ucheshi anaposema kuwa “ninyi husema kuwa wanaume wanaobugia pombe huwa na upungufu wa nguvu za kiume…isipokuwa ni vile haiwezekani, ningekuojesha huyu wangu kiduchu tu!”

Haya yanajiangazia katika mazingira ambapo wanawake wengi katika Mlima Kenya wamekuwa wakiandamana kuteta kuwa wanaume wao wamezama ndani ya mtindi na wamegeuka kuwa mabwege.

Kwa mfano, Krisimasi iliyopita, wanawake wengi Murang’a waliandamana kupinga mabaa kufunguliwa mapema na pia kutoa onyo kwa waume zao kuwa hawangepewa nafasi ya kubugia pombe bila kuthibitiwa.

Wanawake hao wakiongozwa na diwani wa Murang’a Mjini Bi Jacinta Ng’ang’a walisema kuwa wanawake watakuwa wakishika doria mjini humo ili kuwafurusha mabwana hao kutoka kwa mabaa na lojing’i.

Waliwasilisha tetesi zao kwa Kamishna wa Kaunti hiyo wakati huo, Jiohn Elung’ata.

“Tunaomba ushirikiano wa utawala wa kaunti kuhakikisha kuwa visa ambavyo hujitokeza katika misimu ya sikukuu ya wanaume kunywa kupindukia na kisha kulala na viruka njia katika lojing’i za mji huu vimezimwa,” akasema Bi Eunice Wanjiku wa Murang’a County Women Empowerment Forum.

Alisema kuwa wanawake wengi hubakia wakisononeka baada ya waume wao kufuja hela zote katika anasa za mji huo na ndiyo sababu kwa mwaka mzima wamekuwa wakiandamana kupinga unywaji wa pombe kupindukia na pia visa vya makahaba kujazana mjini humo.

Alisema wanawake wako tayari kuandamana na mabwana zao ndani ya baa ili kuwakalisha na kuwachunga dhidi ya wizi wa hela na mahaba unaojitokeza ndani ya baa haswa wakati mtu amelewa.

Badala ya kuiangazia kwa kelele ya maandamano, Bi Kiai anasema “wangeketi chini kama sisi, wasikizane na waanze kuandamana pamoja ndani ya baa.” Ama kweli ndoa ni kufaana.

You can share this post!

Jaji aagiza wakili wa Burundi akamatwe

Shuja wajiandaa kwa duru ya London

adminleo