• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
Pasta ndani miaka 25 kwa kunajisi na kuua msichana mjamzito

Pasta ndani miaka 25 kwa kunajisi na kuua msichana mjamzito

Na GERALD BWISA

PASTA mwenye umri wa miaka 30, Alhamisi alifungwa jela miaka 25 baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi na kumuua mwanafunzi wa kidato cha nne aliyekuwa mjamzito.

Charles Nyanchwara Okere, alimnajisi na kumuua mwanafunzi wa kidato cha nne, Scolastica Mmbihi, 17, mnamo Julai 7, 2011 katika eneo la Naisambu, Kaunti ya Trans Nzoia.

Jaji Hillary Chemitei wa Mahakama Kuu ya Kitale, alisema upande wa mashtaka ulithibitisha kwamba mshtakiwa alimuua msichana huyo.

“Nimepata kwamba kesi hii ilithibitishwa kikamilifu. Mshtakiwa amehukumiwa kufungwa jela miaka 25,” alisema Jaji Chemitei.

Awali kabla mauaji hayo kutokea, Nyanchwara, ambaye alikuwa mhubiri katika Kanisa la Yuya Pentecostal Assembly of God alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la unajisi na akaachiliwa kwa dhamana.

Alipoachiliwa kwa dhamana alimtafuta mlalamishi ambaye alikuwa na mimba ya miezi mitano na kumuua.

Bw Mathew Kipkeu, ambaye ni mwalimu mstaafu, aliambia mahakama kwamba siku ya kisanga alishuka matatu na kuelekea nyumbani kwake mwendo wa saa kumi na moja na nusu jioni, alipomuona mshtakiwa na marehemu kando ya barabara.

Alieleza kuwa mshtakiwa alikuwa ameshika kibeti cha msichana huyo. Baada ya kutembea mita 50 alisikia msichana akipiga nduru na alipotazama nyuma alimuona mshtakiwa akimpiga msichana huyo.

“Alikimbia nilipoenda kumuokoa msichana huyo lakini akakamatwa na mpita njia mwingine aliyemkimbiza. Msichana huyo alikufa kabla ya gari kuwasili kumpeleka hospitali,” Bw Kipkeu alieleza mahakama.

Paul Mmbihi, baba ya marehemu, alieleza mahakama kwamba alimfahamu mshtakiwa kama pasta wa kanisa moja kijijini, ambaye alikuwa amemnajisi na kumtunga mimba binti yake.

“Alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la unajisi na kesi ilikuwa ikiendelea. Baadaye aliachiliwa kwa dhamana na familia yake ikitaka tupatane lakini hakukubali,” alisema.

Ripoti ya mtaalamu wa kuchunguza maiti ilisema kwamba msichana huyo alikufa kutokana na majeraha aliyopata shingoni.

You can share this post!

Hatimaye Ingwe yapata mnyonge wa kunyonga

Mvua yazua maafa Pwani

adminleo