• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Nikishindwa 2022 nitajiunga na upinzani – Ruto

Nikishindwa 2022 nitajiunga na upinzani – Ruto

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto amesema kuwa yuko tayari kujiunga na Upinzani ikiwa atashindwa kwenye uchaguzi wa urais mnamo 2022.

Kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Kameme FM Alhamisi, Dkt Ruto alisema kuwa atatii uamuzi ambao Wakenya watafanya kuhusu kiongozi watakayemtaka kuongoza.

“Sitaenda mahakamani kulalamikia kushindwa wala sitaitisha maandamano. Nitajiunga na Upinzani na kumpa nafasi kiongozi atakayechaguliwa kuhudumu. Asiyekubali kushindwa si mshindani,” akasema, kwenye kauli iliyoonekana kumlenga kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Ingawa ingali haijabainika ni nani atakayepeperusha tiketi ya urais ya Chama cha Jubilee (JP) katika uchaguzi huo, Dkt Ruto ndiye amekuwa akipigiwa upatu zaidi kumrithi Rais Kenyatta kipindi chake kitakapoisha.

Dkt Ruto alisema kuwa viongozi wanapaswa kuheshimu uamuzi ambao unafanywa na wananchi, badala ya kuwashinikiza kushiriki katika maandamano, ambapo baadaye baadhi yao hupoteza maisha yao.

Tayari, baadhi ya viongozi kutoka ukanda wa Mlima Kenya wametangaza kubuni vuguvugu liitwalo #StopRutoMovement, linaloongozwa na aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa JP, David Murathe, linalolenga kumzuia Dkt Ruto kuwania urais.

Kundi hilo pia limekuwa likiungwa wanasiasa wanaoegemea mrengo wa ‘Kieleweke’ linalosisitiza kuwa Dkt Ruto anahujumu utendakazi wa Rais Kenyatta kwa kuendeleza kampeni za mapema.

Hata hivyo, Dkt Ruto alipuuzilia mbali juhudi hizo, akizitaja kama “mbinu za kisiasa zilizopitwa na wakati.”

“Mimi na Rais Kenyatta tumekuwa marafiki kwa zaidi ya miaka 20. Nimesimama naye, hata wakati ambapo ilikuwa dhahiri ingekuwa vigumu kwake kushinda urais. Je, wanasiasa hao walikuwa wapi wakati huo?” akashangaa.

Akaongeza, “Kundi hilo ni la wanasiasa wachache katika Jubilee, ambapo mwisho wao litajiunga na ODM. Ni hadaa tupu kwao kudai kutumwa na Rais Kenyatta kufikisha jumbe mbalimbali kwa Wakenya ilhali mimi ndiye Naibu Rais aliyechaguliwa.”

Alisema kuwa dhana ya mgawanyiko katika JP imekuwa ikiendelezwa na wanasiasa hao, kwa ushirikiano na upinzani. Kundi la ‘Kieleweke’ linaongozwa na mbunge maalum Maina Kamanda, Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Muturi Kigano (Kangema) kati ya wengine.

Kwa mara nyingine, Dkt Ruto alitetea vikali ziara zake katika maeneo mbalimbali nchini kuzindua miradi ya maendeleo, akisisitiza huwa anatekeleza majukumu anayopewa na Rais Kenyatta.

Alisisitiza kuwa ndiye “mtu wa mkono” wa Rais Kenyatta, kinyume na madai ya baadhi ya viongozi kama Odinga na Kalonzo Musyoka, ambao wamenukuliwa wakidai kumwakilisha Rais katika baadhi ya hafla.

“Mimi ndiye naibu rais wa Kenya. Wengine wanaodai kumwakilisha Rais Kenyatta ni matapeli wa kisiasa wanaopiga kelele tu,” akasema.

Ruto vilevile alimlaumu Odinga kwa kudai kutakuwa na mabadiliko ya katiba mwaka huu, akishikilia kuwa lazima mageuzi yoyote yawahusishe Wakenya wote.

“Katiba si mali ya mtu binafsi eti itabadilishwa vivi hivi tu bila kufuata taratibu zifaazo. Binafsi, ninaunga mageuzi hayo, lakini ni lazima yawe ya manufaa kwa kila Mkenya bali si viongozi wachache,” akasema.

Mnamo Februari, Bw Odinga alieleza uwezekano kuandaliwa kwa kura ya maoni mwaka huu, kauli ambayo amekuwa akisisitiza.

You can share this post!

Mwekezaji ataka Joho atupwe jela miezi 6

Wavuvi 24 wa Kenya wabambwa na polisi UG

adminleo