• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
HUDUMA NAMBA: Baadhi ya watu kusajiliwa upya

HUDUMA NAMBA: Baadhi ya watu kusajiliwa upya

NA CECIL ODONGO

WALIOJISAJILI kwa Huduma Namba huenda wakahitajika kujisajili upya katika afisi za chifu endapo itapatikana habari walizotoa wakati wa usajili wa kwanza zina kasoro, serikali imesema.

Serikali Alhamisi ilitangaza kwamba itaanzisha shughuli ya kuchunguza rekodi za waliojisajili, kisha wale ambao watapatikana kuwa na kasoro watapigiwa simu kujisajili upya baada ya data yote kusafishwa katika muda wa miezi minne ijayo.

Msemaji wa Serikali, Kanali Cyrus Oguna, alisema usajili huo hauwezi kuwa safi kwa asilimia 100, na kuna uwezekano makarani walifanya makosa wakati wa kunasa habari za wananchi.

“Tutajumuisha data yote kisha kuisafisha na kuyaondoa makosa ambayo huenda yalitokea wakati wa usajili. Wakenya ambao maelezo kuwahusu hayakunakiliwa vizuri watapigiwa simu na nambari maalum na kutakiwa kujisajili upya katika ofisi za manaibu wa chifu,” akasema Kanali Oguna wakati wa kikao cha kila Alhamisi na wanahabari ofisini mwake.

Afisa huyo wa serikali pia aliwaomba Wakenya wote kumiminika katika vituo mbalimbali leo na kesho ili wasifungiwe nje kwenye shughuli hiyo itakayofungwa kesho.

“Ningependa kuwaomba wale ambao hawajajisajili kufika vituoni na kupata Huduma Namba. Baada ya hapo watakuwa na kibarua kigumu kuwarai manaibu wa chifu kuwasajili kwa sababu hata wao wana kazi zao za kuwajibikia kila siku,” akaongeza Kanali Oguna huku akifichua kwamba idadi ya Wakenya ambao wamejisajili hadi sasa ni milioni 36.

Usajili wa kupata Huduma Namba ambao utakuwa umedumu kwa siku 45 kufikia kesho umekuwa ukikumbwa na changamoto tele huku milolongo mirefu ikitarajiwa kwenye vituo vya kujisajili leo na kesho.

Usajili huo mwanzo ulipata pingamizi kutoka kwa Wakenya na baadhi ya viongozi wa kidini, ambao hadi leo wanadai hawajafafanuliwa sababu ya kuwa na nambari hiyo, huku serikali nayo ikisisitiza lengo lake hasa ni kuboresha utoaji wa huduma.

Wakati huo huo, Kanali Oguna alisema mpango wa utekelezaji wa Mtaala mpya (CBC) utaendelea, akidai malalamishi yanayotolewa na Chama cha Walimu(KNUT) hayana msingi wala mashiko.

“ Nakiri kwamba utekelezaji wa mtaala huo unakumbana na changamoto kama ukosefu wa vifaa vya kutosha shuleni, uhaba wa walimu na baadhi ya wakufunzi kutopata mafunzo ya kutosha. Hata hivyo, serikali imejitolea kupambana na matatizo hayo na tayari walimu 187,901 wamepokea mafunzo ambayo yataendelea mwezi Agosti,” akaongeza Kanali Oguna.

Msemaji huyo wa serikali pia alifichua kwamba mizigo 134 ya kundi la wafanyabiashara wa Nyamakima iliyokuwa ikizuiliwa bandarani imewaachiliwa baada ya kulipiwa ushuru huku mingine 32 ikiendelea kuzuiliwa baada ya wamiliki kukosa kujitokeza.

Kanali Oguna pia alishikilia kwamba marufuku ya kuagiza vipuri kutoka nje ya nchi itadumu, japo akasema sera inaendelea kubuniwa ili kuzuia uingizaji nchini wa magari yaliyotengenezwa kwa zaidi ya miaka mitano.

You can share this post!

Ruto awaonya Wachina wakora wanaovunja sheria Kenya

Nitazidi kutoa pesa, sijaiba za mtu- Ruto

adminleo