• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
DAU LA MAISHA: Digrii anayo lakini auza ndizi mtaani

DAU LA MAISHA: Digrii anayo lakini auza ndizi mtaani

Na PAULINE ONGAJI

NYAKATI hizi ambapo viwango vya ukosefu wa ajira vimekuwa vikiongezeka kila kuchao, vijana wengi wamekuwa wakipoteza matumaini hasa baada ya kukamilisha masomo ya vyuo vikuu.

Lakini kwa Risper Kerubo, 28, licha ya kusaka ajira kwa muda bila mafanikio, hajafa moyo na badala yake ameamua kujitafutia mbinu mbadala kujisakia riziki.

Bi Kerubo alikamilisha elimu ya chuo kikuu mwaka wa 2015 na kuhitimu kwa kupata daraja la kwanza katika masuala ya usimamizi wa huduma za afya.

Ni matokeo ambayo yangemhakikishia nafasi ya usimamizi katika hospitali.

Lakini lo! Matarajio yake kuwa matokeo mazuri yalimhakikishia ajira mara moja, yaligonga ukuta.

“Niliangalia huku na kule nisione mwanya wa mwangaza na hapo nikagundua kwamba itanibidi kufanya angalau ya kijungumeko la sivyo nitumbukie kwenye lindi la umaskini,” aeleza.

Mwaka wa 2016 aliamua kujitosa katika biashara huku akifungua duka la kuuza matunda mtaani Imara, jijini Nairobi.

“Katika duka hili nauza ndizi za kijani na parachichi kwa jumla ambazo huagiza kutoka Kisii, kisha kusambazia wafanyabiashara wengine,” asema.

Wateja wake wanajumuisha wachuuzi wadogo wa vibanda mtaani, vile vile wateja binafsi wanaonunua kwa matumizi yao nyumbani.

Kwa siku anaweza kuuza kati ya magunia 11/2 na 2 ya kilo 90 za ndizi na hata kreti tano za parachichi.

Siku yake ya kawaida huanza saa kumi alfajiri ambapo hufululiza hadi soko la Muthurwa kupokea mzigo wake kisha kuusafirisha hadi mtaani Imara.

Baada ya hapa hutenga na kuchambua ndizi hizo, huku akihakikisha zinafikia wateja wake wakuu. Ni shughuli inayochukua hata masaa matano.

“Kisha muda uliosalia mimi huuzia wateja dukani na kumshughulikia binti yangu, kabla ya kurejea nyumbani jioni kusubiri keshoye,” aongeza.

Kupitia biashara hii anaweza kupata faida ya Sh1,000 kwa siku baada ya kutoa gharama zikiwa ni pamoja na nauli ya usafiri, mtaji na mshahara wa mfanyakazi wake mmoja anayemlipa Sh500 kila siku.

Huu ukiwa takriban mwaka wake wa tatu tangu alipoanzisha biashara hii, anasema kwamba mapato yake hapa yameweza kuimarisha kiwango cha maisha cha familia yake.

“Kutokana na ukosefu wa ajira, mume wangu ambaye amehitimu na shahada ya uhasibu, anafanya kazi ya kufunza somo la hisabati katika shule moja ya kibinafsi hapa mtaani. Tukiongeza mapato yake na yangu, tunakidhi mahitaji ya familia yetu vyema,” anaeleza.

Ukakamavu

Hatua yake ya kujihusisha katika biashara tena kwa ukakamavu ni hatua nzuri ya kuwapa matumaini vijana wanaohangaika huko nje katika harakati za kusaka ajira, huku wakidinda kujihusisha na shughuli zingine za kujitafutia riziki eti kwa sababu wana kisomo.

“Kazi hii inahusisha bidii na mara nyingi uchafu. Wengi walio na digrii hawawezi kutaka kuonekana wakifanya kazi inayohusisha uchafu huku wakihofia kusimangwa. Ni fikra potofu wanayofaa kutupilia mbali na badala yake kujihusisha katika shughuli zingine halali za kujieletea riziki huku wakiendelea kusubiri kupata ajira ya somo walilosomea chuoni,” aeleza.

Kwa Bi Kerubo, japo anatumai wakati mmoja kupata kazi aliyosomea, anasema kwamba biashara hii imempa matumaini na kumpanua kimawazo, na hana nia ya kuiacha.

You can share this post!

SOKOMOKO: Wasichana wala hela

Vijana wa Murunga waanza kwa ‘mguu mbaya’...

adminleo