• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 11:14 AM
Murigi moto wa kuotea mbali mbio za milimani, ashinda Ufaransa

Murigi moto wa kuotea mbali mbio za milimani, ashinda Ufaransa

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Lucy Wambui Murigi alifungua msimu wake wa Kombe la Dunia la mbio za milimani za mwaka 2019 kwa kushinda taji la Salomon Gore-tex Maxi-Race mjini Annecy nchini Ufaransa mnamo Mei 24.

Mbio hizi za umbali wa kilomita 16.5 zinazohusisha wakimbiaji kupanda mlima mita 945 na kuteremka mita 990, zilishuhudia Murigi akituma onyo mapema kwa wapinzani wake.

Alifungua mwanya wa dakika mbili kufikia katikati ya mbio akifuatiwa na raia wa Jamhuri ya Ireland Sarah McCormack, Mfaransa Iris Pessey na Mwingereza Emma Clayton.

Baada ya mteremko, uongozi wa Murigi dhidi ya McCormack ulikuwa umepunguka kidogo, lakini bado alikuwa katika nafasi nzuri akiingia kilomita ya mwisho.

Lucy Wambui Murigi. Picha/ Hisani

Murigi alikata utepe kwa saa 1:30:27 akijizolea alama 100 anazopata mshindi katika ligi hii ya mbio saba. McCormack alimaliza katika nafasi ya pili kwa saa 1:32:33.

Alivuna alama 90 naye Pessey akaridhika katika nafasi ya tatu kwa alama 85 baada ya kukamilisha mbio kwa saa 1:37:07.

“Nafurahia sana kuanza msimu kwa ushindi,” alisema Murigi, ambaye ni bingwa wa dunia mwaka 2017 na 2018.

“Eneo la mashindano halikuwa rahisi; ilikuwa kuenda juu karibu kilomita 9.5 na kisha kuteremka kilomita sita. Nilidhibiti kasi yangu ili niweze kukamilisha mbio,” Murigi alieleza tovuti ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF).

Nafasi tatu za kwanza kwa upande wa wanaume zilinyakuliwa na Muingereza Andrew Douglas (saa 1:15:10), Muamerika Andy Wacker (1:16:00) na Mkenya Robert Panin Surum (1:16:11) mtawalia.

Baada ya Salomon Gore-Tex Maxi Race (Annecy, kilomita 16.5) mwezi Mei, wakiambiaji wataelekea Broken Arrow Sky Race nchini Marekani kwa mbio za kilomita 26 mwezi Juni.

Duru zingine ni Grossglocknerlauf (Austria, kilomita 12.7) mwezi Julai, Snowdon (Uingereza, kilomita 15.5) mwezi Julai, Sierre-Zinal (Uswizi, kilomita 31) mwezi Agosti, Drei-Zinnenlauf (Italia, kilomita 17.5) mwezi Agosti na Smarna Gora nchini Slovenia inayojumuisha kilomita 10 mwezi Septemba.

You can share this post!

Shujaa yafufua matumaini ya kusalia Raga ya Dunia kwa...

Operesheni yapata miili 14 mito ya Nairobi

adminleo