• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 11:05 AM
Waititu na Nyoro wasisitiza kumuunga Ruto 2022

Waititu na Nyoro wasisitiza kumuunga Ruto 2022

Na NDUNG’U GACHANE

MBUNGE wa Kiharu Ndindi Nyoro amesema kuwa hakuna lolote ambalo litamzuia yeye binafsi na ukanda wa Mlima Kenya kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto katika azma yake ya kuwania urais mnamo 2022.

Bw Nyoro alisema kuwa ataendelea kumuunga mkono Dkt Ruto kutokana na rekodi yake ya maendeleo, hasa katika ukanda huo.

Mbunge huyo alisema kuwa Dkt Ruto ndiye ataibuka mshindi kwenye uchaguzi huo, iwapo atashindana na kiongozi wa ODM, Raila Odinga au Seneta wa Baringo Gideon Moi.

Bw Nyoro alisema kuwa wakazi wa eneobunge lake pia watamuunga mkono kiongozi huyo, kwani amezindua miradi mingi ya maendeleo ambayo imewafaidi.

“Kutokana na mchango wa Dkt Ruto, shule kadhaa katika eneobunge langu zimefaidika na mamilioni ya pesa za maendeleo. Je, ni maendeleo yapi waliyoleta Mabw Odinga na Moi katika Kaunti ya Murang’a na Mlima Kenya kwa jumla?’” akauliza.

Akaongeza: “Hatumfuati kwa upofu tu bila kujua tuelekeako. Tunajua hali ya mustakabali wetu ni nzuri chini ya uongozi wake.”

Msimamo ni uo huo

Alisema kuwa hawatabadilisha msimamo wao hata kidogo.

Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu alisema kuwa eneo hilo litamuunga Dkt Ruto kwenye uchaguzi huo, kwani aliitetea jamii ya Agikuyu, wakati ilihitaji usaidizi wake.

“Dkt Ruto alichangia pakubwa katika kuchaguliwa kwa Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2013 na 2017. Tutalishinikiza eneo hili kumuunga mkono kwani alitusaidia sana kushinda urais,” akasema.

Kwa upande wake, George Kimani, ambaye ni mchanganuzi wa kisiasa, alisema kuwa Dkt Ruto ndiye amekuwa akionekana sana kuitetea serikali ya Jubilee hasa katika uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

You can share this post!

Operesheni yapata miili 14 mito ya Nairobi

Mrengo wa Ruto wataka Raila aandikishe taarifa kuhusu...

adminleo